Wanafunzi wa Shule wa Sekondari ya
Arusha wakimsikiliza Mkufunzi kutoka Taasisi ya Gemological Insitute
of America (GIA) , Elizabeth Bokaba (hayupo pichani). Wanafunzi hao
wamepata mafunzo kuhusu mafunzo ya Jimolojia.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Arusha wakifuatilia mafunzo kwa vitendo kuhusu elimu ya madini ya vito
yanayopatikana chini, wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya
Vito yanayoendelea jijini Arusha.
Mratibu wa Kituo cha Jemolojia
Tanzania (TGC), Eric Mpesa akiwaeleza jambo wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Arusha wakati wa mafunzo ya Jemolojia yaliyotolewa na Taasisi
ya GIA wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito Arusha yanayoendelea
jijini Arusha.
Mkufunzi kutoka Taasisi ya
Gemological Institute of America (GIA), Elizabeth Bokaba, akiwafundisha
elimu ya Jemolojia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Arusha.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Arusha wakiangalia madini ya Tanzanite katika Banda la Kampuni Gliters
Gems Limited wakati walipotembelea mabanda ya maonesho baada ya kupata
mafunzo ya Jemolojia.
Mfanyabiashara wa Madini wa
Kampuni ya Abdulhakim Mulla akiwaonesha wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Madini ya Tanzanite. Mulla alitumia nafasi hiyo kuwafundisha tofauti ya
madini yaliyonakishiwa na ambayo bado hayajakatwa.
……………………
Na Asteria Muhozya, Arusha
Jumla ya Wanafunzi 55 kutoka
Shule za Sekondari za Arusha Day, Arusha Sekondari na Wining Sprit
wenye umri kati ya miaka 12- 15 wamepatiwa mafunzo ya Jemolojia katika
Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yanayoendelea jijini
Arusha.
Mafunzo hayo yanayojulikana kama GemKids yametolewa na Wakufunzi kutoka Taasisi ya Gemological Institute of America (GIA) na kuratibiwa na Kituo cha Jimolojia Tanzania Cha Arusha, (TGC).
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo
hayo, Mratibu wa TGC, Erick Mpesa amesema kuwa, mafunzo hayo ya
Jemolojia, yanalenga kuwapa ufahamu wanafunzi ili kuwa na uelewa wa
madini ya vito, kujua matumizi yake, kuyatumia na baadaye kuwawezesha
kuingia katika biashara ya madini huku wakiwa na uelewa mzuri na
rasilimali hizo ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia mahusiano ya TGC na
Taasisi ya GIA, Mpesa amesema kuwa, TGC imelenga kuendeleza ushirikiano
na Taasisi hiyo kwa siku za baadaye hususani katika masuala ya utafiti
na mafunzo na kuongeza kuwa, uhusiano uliopo baina ya taasisi hizo,
umewezesha baadhi ya watumishi wa kituo hicho kupata mafunzo katika
taasisi hiyo.
Kuhusu mpango wa TGC kutoa
mafunzo kwa Watanzania, alisema kuwa, tayari kupitia Maonesho ya Vito
ya Arusha, kituo hicho kuanzia mwaka 2014 kimetoa mafunzo ya ukataji na
unga’rishaji wa madini ya vito kwa jumla wanawake 47 na kueleza kuwa,
hivi sasa jumla ya wanawake 18 wanaendelea na mafunzo hayo na
wanatarajiwa kuhitimu ifikapo tarehe 19 ya mwezi huu.
“Kutokana na changamoto ya ajira
wahitimu wetu tunawashauri kujiunga katika vikundi ili kuwawezesha
kupata ruzuku pale zinapotolewa na Serikali. Hii inawezesha rasilimali
inayotumika kuwafundisha kuwawezesha vijana hawa isipotee bure. Lengo
letu ni kuwawezesha waweze kujiajiri na kuajiriwa,” alisisitiza Mpesa.
Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Vito ya Arusha yalianza rasmi tarehe 3 Mei na yanataajiwa kufungwa tarehe 5 Mei,2017.
No comments:
Post a Comment