NA JUMA FARID, ZANZIBAR.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na baadhi ya Jumuiya za wanafunzi wa
Vyuo Vikuu nchini zinazoonyesha nia ya kuthamini fani ya Ujasiriamali
kama chanzo mbadala cha kupunguza tatizo la Ajira nchini.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa
Viwanda Zanzibar, Saleh Suleiman Hamad kwa Niba ya Waziri wa
Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali Wakati akifunga warsha
ya Mashindano ya miradi ya Ujasiriamali kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar
yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar ( ZU) huko
Kampasi Kuu ya Chuo hicho Tunguu.
Amesema ubunifu ulionyeshwa na wanafunzi hao katika
uandishi, mikakati na bidhaa za miradi ya Ujasiriamali waliyoiwasilisha
katika Mashindao hayo inajenga ushawishi kwa serikali na mashirika mengine ya
kimataifa kuwaunga mkono ili wafikie malengo yao ya kujiajiri na kuwaajiri
vijana wengine wasiokuwa na ajira.
Amesema bado wanafunzi wengi wanaohitimu elimu ya
ngazi ya vyuo vikuu nchini hawajatumia fursa zinazopatikana katika fani ya
Ujasiriamali ambayo imekuwa ikitegemewa na mataifa mbali mbali duniani
kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana.
“ Nasaha zangu kwenu kabla ya kuanzisha mradi wowote
fanyeni tathimini na utafti wa kitaalamu kubaini aina ya ujasiriamali unaotaka
kufanya una maslahi gani na wateja wako wahitaji bidhaa za aina gani sambamba
na kuwa wabunifu wa kufanya miradi isiyofanana.”, alisema Katibu huyo.
Aidha alieleza kwamba kwa niaba ya Waziri wa Viwanda
na Masoko, Balozi Amina Salum Ali serikali itaendelea kudhamini miradi
itakayoonyesha ustawi na maendeleo endelevu.
Pia katika juhudi za kuwajengea uwezo
wajasiriamali hao alieleza kwamba serikali itashawishi makampuni na mashirika
ya kimaita ya kibiashara kufanya kazi kwa karibu na jumuiya hizo ili zipate
soko la uhakika la kuuzia bidhaa zao.
Hata hivyo ametoa nasaha zake kwa wajasiriamali
hao kutengeneza bidhaa bora zitakazokubalika katika soko la kimataifa pamoja na
kujiongeza kitaaluma kupitia mafunzo mbali mbali ya fani hiyo.
Mapema akizungumza Mlezi wa Jumuiya ya
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar(ZU), Bw. Juma Rashid Khamis ambaye
pia ni Mhadhiri wa Chuo hicho aliwasihi washiriki wa mashindao hayo kuendelea
kujifunza zaidi kupitia kwa wajasiria mali wakongwe ili wapate ujuzi wa ziada
wa kukabiliana na ushindani wa bidhaa na miradi ya ujasiriamali ndani na nje ya
Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya SISI Consultants,
Mohamed Wario aliwataka Wasomi hao kutumia vizuri fursa
hiyo ya ujasiria mali kwa kuangazia sehemu tofauti ambazo bado
hazijatumiwa vizuri kibiashara zikiwemo Sekta ya
Utalii, Uvuvi na Ufugaji ili kuzalisha bidhaa bora zinazotokana na rasilimali
hizo na kuzishindanisha katika soko la ndani na nje ya nchi.
“ Kampuni ipo tayari kushirikiana na
nyinyi wakati wowote lakini lazima mjiongeze zaidi kufikia lengo la
kufanya miradi bora na inayoendana na mahitaji ya sasa ili mpate mafanikio
zaidi”, alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake mshiriki wa mashindano hayo
aliyeshindanisha mradi wa usindikaji wa bidhaa aina ya Jam inayotumia kwa
chakula cha mkate iliyotengenezwa kwa matunda ya Maembe, Ehlam Ali Khamis
alisema wazo la kutengeza bidhaa hizo ni kutokana na kukosekana kwa matumizi
mazuri ya matunda hayo hasa wakati wa msimu wake hali inayosababisha kuharibika
kwa kukosekana kwa viwanda vya kusindika matunda hayo.
Akitoa ufafanuzi juu ya Warsha hiyo,
Mwanzilishi na Msimamizi wa Mashindano hayo Jumuiya ya
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Zanzibar ZANUSO, Mohamed Omar
alifafanua kwamba awali mchakato huo ulishirikisha jumla ya vyuo Sita na
ulipopita mchujo vikabaki vitatu ambavyo ni Zanzibar University (ZU), State
University of Zanzibar(SUZA) na Summait University.
Mashindano hayo wamepatikana washindi saba ambao
wamepewa Zawadi mbali mbali zikiwemo simu za Adroid, lakini nafasi ya kwanza
ambayo imeshikiliwa na Issah Eugenio kwa mradi wa Handbags Made in Jeans,
nafasi ya pili ni Ehlam Ali Khamis kwa mradi wa Mango Jam na Tatu Ibrahim ahmad
abdalla na Sabrina Khamis Machano wa mradi wa Teke knowlge solutions
company wote kutoka vyuo tofauti vilivyoshiriki kwa awatua hiyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya SISI Consultants, Mohamed
Wario ambayo ni miongoni mwa wadhamini akitoa nasaha zake kwa wanafunzi
walioshiriki katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na jumuiya ya
Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar(ZANUSO) huko ZU kampasi kuu ya Tunguu.
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Viwanda Zanzibar, Saleh
Suleiman Hamad akiutubia wakati wa kufunga mashindano yaliyoandaliwa na
jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar(ZANUSO) huko ZU kampasi kuu ya
Tunguu.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mashindano hayo
Picha ya pamoja ya washiriki wa mashindano hayo pamoja
na Viongozi wa ZANUSO na ZU pamoja na mgeni rasmi.
No comments:
Post a Comment