Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Jumla ya vijana 1376 wa Wilaya ya
Ifakara mkoani Morogoro wamenufaika na mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) na kuratibiwa na
Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Plan International.
Takwimu hizo zimetolewa leo
mkoani humo na Meneja wa Shirika hilo Wilaya ya Ifakara, Majani Rwambali
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya
maendeleo ya mradi huo unaotarajia kuisha mwaka 2018.
Rwambali amesema mradi huo
umeanza tangu mwaka 2015, unatekelezwa katika Mikoa mitano ikiwemo ya
Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro ambapo vijana wanaoishi
katika mazingira magumu wanapewa elimu ya mafunzo ya ufundi katika fani
mbalimbali ili waweze kujitegemea na kujikwamua kimaisha.
“Kwa wilaya yetu mradi huu
unatekelezwa katika Kata 9 zikiwemo za Mwaya, Mkula, Mchombe, Kibaoni,
Mgeta, Kiberege, Ifakara, Lumemo na Mbongo ambapo hadi sasa jumla ya
vijana 1376 kati ya vijana 1490 waliokuwa kwenye lengo la mradi
wameshapatiwa mafunzo na wengi wao wameshajiajiri”alisema Rwambali.
Meneja amefafanua kuwa mafunzo
hayo hufanyika kwa awamu ambako mpaka sasa awamu zilizofanyika ni nne
huku ikibaki awamu moja itakayohusisha vijana waliosalia kukamilisha
lengo la mradi huo ambao inategemewa kuanza miezi michache ijayo kwani.
Aidha, Rwambali ameongeza kuwa
mradi huo umekua na changamoto katika kuwapata vijana wenye ulemavu kwa
sababu jamii bado haijatambua kuwa vijana hao wana uwezo wa kufanya kazi
na kujipatia vipato sawa na vijana wengine hivyo ametoa rai kwa vijana
hao kujitokeza kwa wingi katika awamu hiyo ya mwisho ya mradi huo.
Kwa upande wake Katibu wa watu
wenye ulemavu wa ngozi wilayani Kilombero, Hamis Liundi ameishukuru
Umoja wa Ulaya kwa kuwaletea mradi huo uliowafikia hadi vijana wenye
ulemavu na kuboresha maisha yao ingawa bado kuna changamoto za vifaa
vya kufanyia kazi pamoja na maeneo kwa ajili ya ofisi.
“Mradi huu ulianza wakati wa
kampeni hivyo watu hawakuufatilia kutokana na kuhusisha mradi huo na
mambo ya kisiasa, uchaguzi umeshapita hivyo ninawaomba vijana wenzangu
hasa walemavu kujitokeza kwani fursa kama hizi zinatokea mara chache,”
alisema Liundi.
Nae mmoja wa walemavu wa viungo
aliyenufaika na mradi huo, Elia Limota amesema kuwa mradi huo
umemuwezesha kutambulika katika jamii na kumfanya awe kijana anayeweza
kujitegemea kwani baada ya mafunzo hayo yeye pamoja na walemavu wenzie
wameweza kuunda kundi na kuvumbua miradi mbalimbali ikiwemo ya uchomaji
wa matofali, ukodishaji wa baiskeli pamoja na kilimo cha mpunga.
No comments:
Post a Comment