Na. Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali itaendelea kutoruhusu
uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous kutokana na ukiukwaji
wa taratibu zilizokuwa zimewekwa wa kuingia ndani ya hifadhi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhandisi Ramo Makani ameyasema hayo leo Bungeni,
Mjini Dodoma
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa juu ya
hatua ambazo Serikali inazichukua kutoa ridhaa kwa wananchi waishio
maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria kuweza kuvua samaki.
“Mwaka 1994, wananchi wa Kata ya
Mwaseni, Mloka, Ngoroka na Kipungila Wilaya ya Rufiji waliruhusiwa
kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua Samaki. Hata hivyo,
baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia
ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha
sheria,” alifafanua Mhandisi Makani.
Aliendelea kwa kusema kuwa baadhi
ya wavuvi walibainika kujihusisha na vitendo vya ujangili wa
wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa ajili
ya kukausha samaki na kutengeneza mitumbwi pamoja na uharibifu wa
mazingira uliotokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.
Mhandisi Makani amesema kuwa kwa
kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori,
Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika
ndani ya Pori la Akiba Selous.
Aidha Wizara inawashauri wananchi
wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo jirani kutumia mabwawa
mengine yaliyoko nje ya Pori hilo yenye fursa kubwa kwa kufanya shughuli
za uvuvi.
Mabwawa ambayo wananchi
wameshauriwa kuyatumia ni Bwawa la Zumbi lililoko vijiji vya
Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe lililopo Mkongo, Lugongo
lililopo kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini lililopo Mji wa Kibiti.
Mabwawa hayo ya Mto Rufiji yatatoa fursa ya shughuli za uvuvi hivyo kusaidia kuinua kipato cha wananchi.
Vile vile Mhandisi Makani amesema
kuwa, Wizara hiyo kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo hayo
ya kufanyia kazi na kujiletea maendeleo kiuchumi na kijamii. Wizara hiyo
inaendelea kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kuhusu namna
ya kutekeleza mpango wa kuwajengea mabwawa ya samaki ili pamoja na
mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe kufanya shughuli za uvuvi
endelevu.
No comments:
Post a Comment