WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa uhakika ili
kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo.
Alitoa agizo hilo jana jioni
(Jumanne, Januari 3, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha Milkcom
kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha
maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe II wilayani Kigamboni akiwa
katika ziara yake ya kikazi.
“Waziri wa Nishati ahakikishe
eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi
kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi
wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati
hiyo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema amefarijika
na jitihada za muwekezaji huyo za kuungamkono mkakati wa Serikali ya
awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda
utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka
2025.
Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo,
Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema
moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa
uhakika jambo linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.
“Punde umeme unapokatika
tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko
la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani
kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.
Faraji alisema changamoto
nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo usababisha wateja wengi
kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba
Serikali kuwatatulia kero hilo.
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda
hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali
itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa
asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.
Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi
ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe II iliyojengwa kwa ufadhili wa
kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia
akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo
No comments:
Post a Comment