WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
ameugiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpelekea
nyaraka zote zilizotumika katika kumuhamisha faru maarufu kwa jina la
John katika hifadhi hiyo ifikapo Desemba 8, 2016.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne,
Desemba 6, 2016) alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko
wilayani Ngorongoro mkoa Arusha wakati akizungumza na watumishi wa
mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu
ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
“Nina taarifa zenu kuwa
mlimuhamisha kwa siri faru John kreta na kumpeleka V I P Grumet
Serengeti Disemba 17, 2015 na mliahidiwa kupewa sh. milioni 200 ambapo
mkapewa sh. milioni 100 kwa ahadi ya kumaliziwa sh. milioni 100
nyingine baadaye,”.
“Naomba niletewe nyaraka zote
zilizotumika kumuomba na kumuondoa faru huyo na barua zilizotumika
kujadili suala la faru John. Nasikia amekufa naomba pembe ziletwe
ofisini na iwapo itathibitika aliondoka bila ya kufuata taratibu
wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria,”.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
apega marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambao
wanawakabidhi watoto kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta. “ Watumishi wa
Ngorongoro ndiyo wanaopeleka ng’ombe ndani ya kreta na si wenyeji. Sasa
marufuku na tutakayemkuta hatutakuwa na msamaha naye,”.
Amewataka watumishi hao
kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa kufuata misingi ya
kiutumishi na kuacha tabia za kuendekeza rushwa na wizi.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary Simfukwe kutokana na
tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari anahojiwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
“Haiwezekani mtumishi awe
anachunguzwa na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si atavuruga
uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi
utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,”
alisema.
Pia Waziri Mkuu alimtaka
Mkurugenzi Mkuu wa NCAA, Fred Manongi kueleza zilipo sh. bilioni moja
zilizotolewa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete kwa ajili ya
kujengea ranchi ya wafugaji wa tarafa ya Ngorongoro.
Akijibu swali hilo Manongi alisema
wakati Rais Kikwete anatoa fedha hizo alikuwa bado hajateuliwa kushika
washifa huo, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi huyo kufanya
uchunguzi juu ya fedha hizo na kasha kumpelekea tarifa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, DESEMBA 6, 2016.
No comments:
Post a Comment