TAARIFA KWA UMMA
UONGOZI
wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC),na baadhi ya
waandishi wa habari wilayani Kahama,wamekutana na mkuu wa wilaya ya
Kahama Fadhili Nkurlu ili kupata muafaka wa tatizo la kukamatwa na
kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa kujitegemea Paul Kayanda.
Kikao
hicho cha usuluhishi kilichofanyika leo Jumamosi Desemba 31,2016 katika
ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,kimehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa
kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Kahama.
Kayanda
alikamatwa jana Desemba 30,2016 na kufikishwa mahakamani kwa agizo la
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimtuhumu kuandika habari za
kumdhalilisha na kuzisambaza kwenye barua pepe mbalimbali za vyombo vya
habari.
Katika
kikao ,Uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga
,ulimuomba mkuu wa wilaya Nkurlu kutaka kufahamu kilichomsukuma kuchukua
maamuzi hayo,na nini ushauri wake juu ya suala hilo lakini pia
kumsikiliza mwandishi Paul Kayanda.
Baada
ya kusikiliza pande zote mbili,kikao kilibaini kuwepo kwa mapungufu
katika habari iliyoandikwa na Kayanda kuhusu habari ya laptop mbili
zilizoibiwa nyumbani kwa mkuu huyo wa wilaya.
Mkuu
huyo wa wilaya alikiri kuwepo kwa tukio la wizi nyumbani kwake lakini
mwandishi huyo aliandika habari kwa kuingilia uhuru binafsi wa kiongozi
huyo akielezea watu wanaoingia na kutoka nyumbani kwake lakini maisha
anayoishi na kijana wake.
Kwa
kuangalia maslahi mapana ya umma kutokana na kutegemeana katika
kusukuma maendeleo ya jamii baina ya uongozi wa serikali na waandishi wa
habari ,kikao kimemtaka Kayanda kumwomba radhi mkuu huyo wa wilaya kwa
kuingilia uhuru wake binafsi na kuuhusisha na habari ya wizi wa laptop
badala ya kujikita kwenye tukio la wizi wa laptop pekee.
Kikao
pia kimebaini kuwa pamoja na mapungufu ya mwandishi, ni ukweli ulio
wazi kuwa mkuu huyo wa wilaya aliibiwa kompyuta mpakato (lap top) mbili
nyumbani kwake na kuagiza vijana watatu wakamatwe kwa mahojiano polisi
akiwemo mmoja anayeishi nyumbani kwake japo ameelezea kuwa hakujua
walishikiliwa kwa siku ngapi.
Mkuu
huyo wa wilaya pia alieleza kukerwa na ujumbe mfupi wa maandishi kwa
njia simu ya mkononi (sms) alizodai kutumiwa na Kayanda kwa kutumia simu
nyingine (tofauti na anayotumia) zenye lugha ya kumtuhumu na
kumdhalilisha.
Hata
hivyo kikao hakikuona kuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha
kama ni za mwandishi huyo kweli au la huku kikao kikiomba sms hizo
zifuatiliwe ili wamiliki wa namba hizo wajulikane .
Baada
ya kujadiliana kwa kina katika kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa
mbili,Kayanda amemwomba mkuu wa wilaya msamaha kwa mapungufu
yaliyojitokeza katika habari hiyo aliyoiandika, na mkuu wa wilaya ambaye
ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama amekubali
kumsamehe mwandishi huyo akiahidi kufuata taratibu zingine kuondoa kesi
mahakamani na kutaka kusafishwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii
ilikoandikwa habari hiyo.
Nkurlu
amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na waandishi wa habari wilaya
ya Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla katika kuandika habari
zinazohusu serikali na akaomba kudumishwa kwa ushirikiano uliopo baina
ya viongozi wa serikali na waandishi wa habari ili kusaidia kuharakisha
maendeleo ya wananchi huku akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia
weledi katika kazi zao.
Aidha
Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga imewasisitiza waandishi
wa habari kuzingatia weledi na kufuata maadili katika kutekeleza
majukumu yao ili kuepuka migongano isiyokuwa na tija kwa umma.
Pia
tunawashauri wadau wote wa habari pindi inapotokea kuingia katika
mgogoro wowote ama na waandishi wa habari au chombo cha habari si vyema
kwenda mahakamani moja kwa moja bali wawasiliane na viongozi wa klabu za
waandishi wa habari katika mkoa husika ili kusuluhishana na kuwekana
sawa.
Imetolewa na
Kadama Malunde
MWENYEKITI –SPC
Mkuu
wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,waandishi wa habari na baadhi ya
wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa katika
kikao cha usuluhishi
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama
Kikao kinaendelea
Waandishi wa habari wakiondoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya baada ya kikao kumalizika
No comments:
Post a Comment