Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi,
Prof. Idrissa Mshoro (katikati kulia) akiteta jambo na Kaimu Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga(katikati
kushoto), pembeni kulia ni Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho
(Mipango, Fedha na Utawala),Prof. Robert Kiunsi, pembeni kushoto ni
Maafisa Waandamizi wa chuo hicho. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini
Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Mmoja kati ya washindi wa jumla
wenye alama za juu, Anyighwile Lwijiso akipokea zawadi kutoka kwa mmoja
wa wafadhili ambao ni Kampuni ya Hightech System mara baada ya
kutangazwa kuwa mshindi. Shughuli hizo zimefanyika leo Jijini Dar es
Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi,
Prof. Idrissa Mshoro akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa chuo
na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma wakati wa shughuli za ugawaji
wa vyeti na zawadi kwa wanafunzi waliofaulu masomo mbalimbali
uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
…………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo Kikuu cha Ardhi kimetoa
zawadi na tuzo kwa wanafunzi 104 waliofanya vizuri kitaaluma ili kutoa
hamasa kwa wanafunzi wengine kuweka juhudi katika masomo.
Zawadi hizo zimetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ambaye
ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi wanne kati ya waliofanya vizuri
wamepata alama sawa hivyo kuibuka washindi wa jumla kwa mwaka 2016.
Akisoma hotuba wakati wa sherehe
hizo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma), Prof. Gabriel
Kassenga amesema kuwa sherehe hizo zimekuwa zikiwezeshwa na wadau
mbalimbali waliojitoa kwa hali na mali kutoa zawadi na tuzo kwa
wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye vipengele mbalimbali vya taaluma
hivyo amewasihi wadau hao kuendelee kuunga mkono jitihada zinazofanywa
na wanafunzi hao ili kuwashawishi wanafunzi wengine kufanya vizuri.
“Zawadi mbalimbali zinazotolewa na
wafadhili zimekua zikiwasaidia wanafunzi hawa kuongeza tija kwenye
maisha yao ya kielimu na kiuchumi kwani wengi wao wamekuwa wakizitumia
fedha hizo kama mitaji ya kufanyia biashara pindi wamalizapo masomo
yao,”alisema Prof. Kassenga.
Amefafanua kuwa mwaka huu umekuwa
wa tofauti kwani idadi ya wanafunzi wanawake na wanaume waliopata tuzo
hizo iko sawa tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo wanawake walikua
wakiongoza kwa asilimia 3.7 kwa kupata tuzo nyingi wakati wanaume wakiwa
ni asilimia 2.2.
Prof. Kassenga ametaja baadhi ya
zawadi zilizotolewa na wafadhili walioshiriki katika shughuli hiyo kuwa
ni vyeti, Kompyuta mpakato (laptop),vifaa vinavyotumika katika kupimaji
wa ardhi pamoja na fedha taslimu.
Aidha, Prof. Kassenga ametoa rai
kwa kwa wanafunzi wote waliomaliza chuoni hapo kuwa juhudi walizokuwa
wakizionyesha wakati wa masomo waende wakaziendeleze katika jamii
zinazowazunguka pamoja na kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa
ili wakawe mfano bora kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Emily Elandogo
ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliopewa zawadi hizo amewashukuru
walimu wa chuo hicho kwa elimu wanayoitoa ambayo itakua ni chanzo cha
kuwaletea maendeleo sehemu yoyote watakapokuwa pia ametoa ushauri kwa
wanafunzi wenzake kuitumia vizuri elimu waliyoipata ili iweze kuwasaidia
katika maisha yao.
Mahafali ya Kumi ya chuo hicho
yanategemewa kufanyika Disemba 3 mwaka huu katika viwanja va chuo hicho
ambapo wahitimu wa shahada mbalimbali watatunukiwa stahili pamoja na
vyeti vyao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment