Waziri wa Fedha na Mpiango Dkt.
Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2017/2018.
………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
Serikali imeainisha maeneo ya
kipaumbele kwa mwaka 2017/2018 kulingana na mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.
Waziri wa Fedha na Mpiango Dkt.
Philip Mpango amesema hayo leo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa
akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018 na
Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.
Dkt. Mpango amevitaja vipaumbele
hivyo kuwa ni pamoja na miradi ya kielelezo ya maendeleo ambayo
inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 ni pamoja na miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mchuchuma
Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es salaam, Tabora hadi
Kigoma yenye urefu wa km 1,251 kwa “Standard Gauge” pamoja na matawi
yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa km 379, Isaka
hadi Rusumo km 371, Kaliua kupitia Mapanda hadi Karema km 321, Keza hadi
Ruvubu km 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati yenye urefu wa
km 203.
Miradi mingine ya kielelezo ni
uboreshaji wa Shirika la Ndege TAanzania (ATC), ujenzi wa mitambo ya
kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda Maalum za
Kiuchumimkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma, uanzishwaji wa kituo cha
biashara cha Kurasini, kusomesha vijana katika stadi za mafuta na gesi,
uhandisi na huduma za afya.
Waziri Dkt. Mpango ameyataja
maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi
wa msingi wa kukuza uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo y
uchumi na maendeleo ya watu, mazingira ya wezeshi kwa uendeshaji
biashara na uwekezaji, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi
pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa.
Dkt. Mpango amesema kuwa shabaha
ya uandaaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 unaongozwa Serikali
kusimamia mambo ya uchumi kwa ujumla ikiwemo kuongeza kasi ya ukuaji wa
pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.5 kwa mwaka 2017, asilimia 7.9
mwaka 2018 na asilimia 8.2 mwaka 2019, kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei
na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kufikia
asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wakati, kuwa na pato ghafi la taifa
la sh. trilioni 123.9 kwa mwaka 2017/18, sh. trilioni 139.7 kwa mwaka
2018/19 na sh. trilioni 165.4 mwaka 2019/20 pamoja na mapato ya kodi
kufikia asilimia 14.6 ya pato la taifa mwaka 2017/18, asilimia 15.5
mwaka 2018/19 na asilimia 15.8 mwaka 2019/20.
Aidha, ametaja misingi ya mpango
na bajeti kuwa ni amani, usalama, utulivu na utangamano wa ndani ya nchi
na nchi jirani ambavyo vitaendelea kudumishwa nchini.
Kuhusu mwongozo wa kuandaa Mpango
na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018, Dkt. Mpango amesema
amewaagiza Maafisa Masuuli kuzingatia masuala muhimu wakati wa uandaaji
wa mipango na bajeti za mafungu yao ili kutekeleza Sheria ya Bajeti Na.
11 ya mwaka 2015.
Zaidi ya hayo, Dkt. Mpango
amesisitiza uwepo usimamizi na udhibiti wa matumizi, ulipaji na ongezeko
la madeni ya Serikali, ukusanyaji wa mapato pamoja na mfumo wa utoaji
taarifa za utekelezaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Bajeti Hawa Ghasia alipokuwa akitoa taarifa ya kamati
yake amesema kuwa Kamati yake inardhishwa na hatua zinazochukuliwa na
Serikali katika kusimamia Sheria ya Bajeti na kanuni zake ambayo
inahakikisha usimamizi na uwajibikaji katika hatua zote za mchakato wa
bajeti unazingatiwa.
Naye Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni Halima Mdee alipokuwa akiwasilisha hotuba yake
amesema kuwa Kambi Rasmi inaunga mkono hatua za kisheria zinazochukuliwa
na Serikali kwa wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine
kuhujumu uchumi wa nchi.
Mkutano wa Tano wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 11
mwaka huu huku shughuli mbalimbali za kuishauri Serikali zikiwasilishwa
kupitia mijadala ya Wabunge.
No comments:
Post a Comment