Pages

Monday, October 31, 2016

MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI UTAIPA HADHI TASNIA YA HABARI

bwee
Na Ismail Ngayonga-Dar es Salaam.
BUNGE la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho (leo) linatarajia kuanza mkutano wake wa tano, ambapo macho na masikio ya wadau na wananchi mbalimbali yataelekezwa katika mjadala wa miswada mbalimbali ikiwemo ule wa huduma za habari wa mwaka 2016.
Tangu muswada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza Bungeni tarehe 16 Septemba mwaka huu, wadau mbalimbali wa habari na wasomi, vyama vya kitaaluma ya habari wamekuwa na mitazamo na misimamo tofuati kuhusu muswada huo.

Miongoni mwa hoja zilizotawala katika mijadala ya wadau ni pamoja na kuongezwa muda wa kujadili muswada huo kwa kina zaidi ili kutoa fursa kwa wadau kuelewa kwa usahihi vipengele vilivyopo katika muswada huo.
Itakumbukwa  mwaka 2006, Serikali iliwasilisha kwa wadau miswada miwili ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Habari ili kuwawezesha kupitia kwa kina vipengele hivyo ili kuboresha uendeshaji na usimamizi wa vyombo vya habari nchini.
Maoni na mapendekezo ya wadau wa habari juu ya muswada wa haki ya kupata habari wa mwaka 2006 yalikamilika na kuwasilishwa Serikalini mwaka 2007 na mapendekezo ya muswada wa huduma za habari uliwasilishwa mwaka 2008.
Kwa kuzingatia uhitaji wa muda mrefu wa sheria hizo, mwezi septemba mwaka huu Serikali iliwasilisha Bungeni muswada wa sheria ya haki ya kupata taarifa, ambayo ilisomwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Pamoja na dhamira ya dhati ya Serikali ya kuharakisha mchakato wa kutungwa kwa sheria hizo, inasikitisha kuona wadau wa habari wakiwemo baadhi ya wamiliki, wahariri, vyombo vya habari na waandishi wa habari wakibishana katika majukwaa na mitandao ya kijamii.
Inashangaza kuona miongoni mwa wadau wanaobishana kuhusu muswada huo ni miongoni mwa taasisi za kisheria ambazo ziliusoma muswada huo, kuujadili na kuwasilisha maoni yao mbele ya Kamati ya Bunge kabla muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni mwezi septemba mwaka huu.
Muswada umeweka wazi wajibu, haki na maslahi ya wamiliki, wahariri, vyombo vya habari na waandishi wa habari ambayo kwa kipindi kirefu yameshindwa kutambuliwa kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kisheria.
Sura ya nne ya muswada imeainisha uanzishaji wa Baraza huru la Habari, ambalo wadau wa habari wamekuwa wakilihitaji kwa ajili ya kuanzisha chombo huru cha wanahabari kinachosimamia haki, wajibu usalama na maslahi ya waandishi wa habari.
Kipengele hicho cha muswada kimekusudia kuongeza na kuimarisha wajibu wa vyombo vya habari katika jamii, na kuifanya tasnia ya habari kuaminika na kudhaminiwa na jamii.
Katika katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, vyombo vya habari vimekuwa chachu ya ujenzi wa maadili ya jamii, nguzo ya amani, mshikamano na utulivu, sambamba na kitovu cha mabadiliko ya kifikra na mawazo ndani ya jamii.
Ili kutekeleza wajibu huo wa msingi ni vyema vyombo vya habari  wajibu kuzingatia miiko, maadili na usalama wa nchi kama ilivyobainishwa katika sheria mbalimbali za nchi ikiwemo sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanisha haki na uhuru mawazo:   “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi”.
Waandishi wa habari wanakumbushwa pia kusoma Ibara ya 31 ya Katiba inayosisitiza kuhusu  madaraka ya  pekee ya mamlaka ya nchi kuhusu ukiukaji wa haki na uhuru.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani zina zimeanisha taratibu za ukomo wa kuzuia utangazaji na uchapishaji wa habari zinazohatarisha usalama wa taifa ikiwemo vita, uasi, mapigano na kadhalika.
Sheria na mikataba ya mbalimbali za kimataifa ikiwemo ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa, umeainisha ukomo wa vyombo vya habari katika masuala ya usalama wa taifa, kashfa na maadili ya taifa.  
Wakati tukielekea katika utungaji wa sheria hiyo, ni wajibu wa wadau wa habari kuwa katika mlengo mmoja, kwa kuwa sheria kiasi kikubwa imekusudia kumkomboa mwandishi wa habari wa Tanzania kuondokana na maslahi duni yaliyopo katika vyombo mbalimbali vya habari.
Aidha kutungwa kwa sheria hizo mbili haki ya kupata habari na sheria ya huduma ya habari ni moja ya dhamira za mipango ya kuendesha shughuli za Serikali kwa uwazi, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Jijini London Uingereza wakati wa mkutano wa OGP mwaka 2013 na 2014.

No comments:

Post a Comment