Pages

Friday, August 5, 2016

Bima ya afya ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania




Wakinamama wajawazito wakiwa wamelala vitandani na wengine chini kutokana na uhaba wodi na vitanda katika moja ya kituo cha huduma ya afya nchini.

Christian Gaya, Majira Ijumaa Agosti 5, 2016 

Moja kati ya haki ya msingi za kila binadamu ni kufurahia viwango vya juu vya afya viwezekanavyo. Serikali zina majukumu ya kitaifa na kimataifa kutoa huduma bora za afya zinazofikika kwa gharama nafuu na zinazopatikana kwa watu wote bila ubaguzi.

Hata hivyo, uhalisi huu katika nchi zinazoendelea kama vile katika Afrika Mashariki ni matakwa ambayo bado hayajatimika.  Kanuni kuu ni kwamba haki ya afya inategemea upatikanaji wa rasilimali za serikali.
Ingawa serikali katika kanda hii zimeweza kuzongwa na ukosefu wa rasilimali na kushindwa kutoa huduma jumuishi  za afya kwa watu wote, huduma za afya kwa maskini na wale walioathirika si hiari bali wajibu.
Aidha, serikali zina jukumu la kuendelea kupanua utoaji wa huduma ya afya kila mwaka na ni mzigo uko begani mwa serikali kuonesha kwamba inafanya hivyo na kwa upeo wa rasilimali zilizopo.
Aidha lazima uwepo uwajibikaji na uwazi zaidi kutoka kwa serikali katika huduma ya afya.
Baadhi ya sauti za vyama vya kiraia vinavyoongoza  katika ukanda wa Afrika Mashariki katika kuanzisha shughuli bunifu na za ujasiri za haki za afya ili kukuza, miongoni mwa mambo mengine, upatikanaji wa dawa muhimu kwa watu wote, uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya, na kuboresha huduma za mwisho wa maisha kwa wagonjwa wenye magonjwa ya chungu ya muda mfupi. 
Ni kwa bahati mbaya ya kuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu kwa ajili ya raia wake. Hivyo na ndio maana kuna taasisi zisizo za kiserikali, za watu binafsi, za kidini na za hifadhi ya jamii ambazo zina wajibu wa kushughulikia mambo kama haya kwa niaba ya serikali kama vile mashirika ya akiba ya wafanyakazi wa makampuni binafsi ambayo yanaweza kuanzishwa na kuendeshwa na waajiri wenyewe.
Zingine ni taasisi za bima za serikali kama vile mfuko wa Taifa wa bima ya afya na taasisi za bima zingine za watu binafsi zilizoko nchini, pamoja na mashirika ya umma yanayotoa pensheni za hifadhi ya jamii na bima ya afya zinazoendeshwa kwa utaratibu wa kanuni za kibima.
Kwa vile haki ya afya ni haki ya kila mtu  ndiyo maana mfuko wa pensheni PSPF wana mpango wa uanachama wa hiari kama mkakati wa makusudi juu ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kuhakikisha ya kuwa hata wale waliojiajiri kujiunga na  PSPF ili kunufaika na huduma ya bima ya afya kwa gharama nafuu ya shilingi za kitanzania zipatazo 76,800 tu kwa mwaka, na mwanachama anaruhusiwa kuingiza wategemezi watano kwa kumlipia kila mmoja ada ya shilingi 76,800 kwa mwaka
PSPF kupitia mpango wake wa uchangiaji hiari imeanzisha fao la matibabu kwa ajili ya wanachama wake walioko katika sekta isiyo rasmi. Mpango huu ni wa ushirikiano kati ya PSPF na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Kwa kupitia mpango huu wanachama wa PSPF walioko katika sekta isiyo rasmi watanufaika na upatikanaji wa huduma za afya kote nchini kwa njia rahisi na kwa uchangiaji nafuu zaidi
Ni Mfuko wa kwanza wa hifadhi ya jamii nchini kuingia na mfuko wa NHIF ambayo yanamwezesha mtanzania aliye katika sekta isiyo rasmi kunufaika na mpango wa bima ya matibabu kupitia NHIF kwa mwanachama aliyechangia kipindi kisichopungua miezi mitatu.
Huduma ya matibabu katika mpango huu inapatikana nchi nzima kwenye vituo vyote vilivyosajiriwa na NHIF kuanzia hospitali ya Taifa, rufaa, hospitali za mkoa, vituo vya afya na zahanati zote za serikal, vituo vya mashirika ya dini na hospitali binafsi pamoja na maduka ya dawa yaliyosajiriwa na NHIF zaidi ya vituo 6,043 nchi nzima.
Na ndiyo maana mfuko wa pensheni wa PSPF unakaribisha wananchi wote wenye umri wa kufanya kazi, kuanzia miaka 18 na zaidi waliojiajiri kwenye sekta isiyo rasmi kama vile Wakulima, wafanyabiashara, ndogondogo, wasusi, vinyozi, mamalishe, mafundi cherehani n.k. kuwa wote wana haki ya kujiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari wa mfuko wa pensheni wa PSPF.
Lengo ni kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kufungua milango kwa kundi kubwa la Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa na uhakika wa matibabu kwa kuwa hawakuwa wanachama PSPF.
Mwanachama aliyechangia kwa kipindi cha miezi 6 na zaidi anaweza kuomba kwa ridhaa yake sehemu ya michango yake itumike kulipia ada ya bima ya afya ili mradi tu kiwango cha mipango yake kitakachosalia katika akaunti yake kisiwe chini ya kiwango kilichotolewa kwa ajili ya bima ya afya.
Uanachama wa bima ya afya utadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu alipojiunga na utauhishwa kila baada ya mwaka mmoja.
Mwanachama mpya atakayehitaji kujiunga na huduma hii mara tu anapojiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari wa PSPF anatakiwa kuchanga kiasi ambacho ni mara mbili ya ada ya mwaka ya bima ya afya, ambapo sehemu ya mchango huo wa awali itatumika kama mchango wa uanachama wa mpango wa hiari na kiasi kinachobaki kitalipwa NHIF kama ada ya mwaka kwa ajili ya bima ya afya.
Tofauti na bima zingine za matibabu, fao la matibabu kwa mwanachama wa mpango wa uchangaji wa hiari wa PSPF halina kiwango cha kikomo cha gharama za matibabu kwa ajili ya huduma zilizoainishwa.
Mwanachama wa mpango wa uchangiaji wa hiari  wa PSPF  anayejiunga na fao la matibabu atanufaika na mafao yote ya bima ya afya sawasawa na mwanachama mwingine yoyote wa mfuko wa bima ya afya (NHIF).
Lengo kubwa ni kumjengea uwezo mjasiliamali mdogo awekeze kwa ajili ya afya yake huku akiendelea na shughuli nyingine za kujitafutia kipato
Kupitia mpango wa hiari mfuko wa pensheni wa PSPF wajasiriamali wote wanaojiunga na mfumo huu watanufaika na Bima ya Afya. Mfuko wa pensheni wa PSPF una uhakika kuwa  wajasiliamali wanaojiwekea akiba kwa ajili ya pensheni watapata fursa ya kupata huduma za matibabu zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na kuwa na uhakika na usalama wa afya zao wakati wanapojishughulisha na  shughuli mbalimbali za ujasiliamali
Mpango huu wa hiari ni mahususi kwa ajili ya kuwapatia huduma ya hifadhi ya jamii wale wote ambao awali kutokana na matakwa ya kisheria hawakuweza kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
PSPF imeamua kuongeza fao hili muhimu la matibabu kwa upande wa mpango wa uchangiaji hiyari ili kuchangia katika huduma za afya kwa watanzania na pia kutekeleza lengo lake la kuwafikia watanzania wengi zaidi na kufungua milango kwa kundi kubwa la watanzania ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa na uhakika wa matibabu kwa kuwa hawakuwa wanachama wa PSPF.
Itakuwa ni jambo jema kuwahimiza wastaafu wengine popote walipo  kujiunga na PSPF ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote hata kama hawana fedha mfukoni.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa gayagmc@yahoo.com www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments:

Post a Comment