Mmojawapo wa wafanyakazi wa majumbani ambao wengi wao hawana habari juu ya haki zao kuhusiana
na masuala ya afya na usalama ikiwemo ya kinga ya hifadhi ya jamii
Christian
Gaya Majira Ijumaa, 1Julai 2016
Wamiliki wa nyumba
ambapo wafanyakazi wa majumbani wanafanyia kazi zao wanaweza kufikiri nyumba
zao ni maeneo salama, lakini nyumba hizo hizo zinaweza kuwasilisha matatizo
kadhaa ya kiafya na ki-usalama kwa watu wanaofanya kazi ndani mwake.
Utafiti uliofanywa
nchini Salvador na Brazil, kwa mfano, uligundua kwamba wanawake wanaofanya kazi
za majumbani wanakabiliana na viwango vya juu vya kuumia na kuambukizwa
magonjwa kuliko wanawake wanaofanya kazi zingine. Wafanyakazi wa majumbani
wanatambua kwamba kazi zao zinaweza kuwa hatari kwa afya zao.
Wafanyakazi wengi wa
ndani hawajui haki zao, hivyo hawawezi kudai ulinzi au haki zao kutoka kwa
waajiri wao kama vile kuandikishwa na mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii.
Mapato ya chini na
ukosefu wa ulinzi au uzingatiwaji wa haki unamaanisha kwamba wafanyakazi wa
majumbani wapo katika mazingira magumu na hivyo hatarishi kwa afya zao.
Endapo itatokea
wakaugua au kuumia na hivyo kushindwa kuja kazini, wanaweza kupoteza mishahara
au ujira wao au kufukuzwa kazi.
Tanzania zikiwemo
Brazil na nchi kadhaa, zimeanza kuwahusisha wafanyakazi wa majumbani katika
sheria za kazi ili kuwapatia kinga au haki za msingi kama vile likizo ya uzazi,
likizo ya ugonjwa na ruzuku ya serikali pindi wanapokuwa hawana kazi.
Hata hivyo, inaweza
kuwa vigumu sana kutekeleza sheria hii katika nchi yetu ambayo wasimamiaji wa
sheria za kazi hawana vitendea kazi au rasilimali za kutosha za kufanyia kazi
zao na mifumo ya taarifa/habari ni duni.
Wanaweza kuwa hawana
hifadhi ya jamii ya aina yeyote au akiba ili kulipa bili za matibabu au
kuwafanya waendelee na maisha mpaka watakapopata kazi mpya.
Hali hii inaweza
kuonekana isiyo ya haki kabisa hususani kwa wafanyakazi ambao awali ya yote,
chanzo cha ugonjwa au kuumia ni hiyo kazi yenyewe.
Taratibu au sheria
za Afya na Usalama katika Maeneo ya Kazi yaani Occupational safety and health
(OSH), ambazo zimelenga katika kuzuia hatari za kuumia au kupata ugonjwa katika
sehemu za kazi, mara nyingi zimeonekana kuwalinda wafanyakazi rasmi waliopo
katika mazingira rasmi ya kazi kama vile migodini, viwandani, ofisini na
madukani ingawa bado kiwango kinachotakiwa hakijafikiwa.
Kanuni hizi
haziwalindi wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika nyumba binafsi, kitu
ambacho kinamaanisha kwamba japokuwa kazi za nyumbani ni chanzo muhimu cha
ajira, na ingawa kuna hatari nyingi za kiafya na kiusalama katika kazi hizo, na
japokuwa wafanyakazi wa majumbani wapo katika mazingira magumu ya umasikini
endapo wataugua au kuumia, taratibu au sheria za OSH katika nchi yetu hii
haziwazingatii.
Nchini Tanzania
watafiti pia mara nyingi wanatumia njia au mbinu inayoitwa “orodha ya kukagulia
afya” yaani health checklist. Tatizo ni kwamba mara nyingi watu huwa wanasita
kuongelea juu ya miili yao na matatizo ya kiafya wakiwa wanahojiwa na kundi la
watu ambao hawawajui vizuri.
Utafiti juu ya Afya
na Usalama Katika Maeneo ya Kazi (OSH) na wafanyakazi wa majumbani unatakiwa
kufanyika na mara nyingi unakuwa na malengo makuu mawili.
Lengo la kwanza
unakuwa kuelewa matatizo ya kiafya na kiusalama ambayo wafanyakazi wa majumbani
wenyewe wanayapa kipaumbele. Wafanyakazi wa majumbani wanajua vizuri zaidi juu
ya matatizo wanayokabiliana nayo wao ni wataalamu wa hali ya juu kuhusu
mazingira yao ya kazi, na katika mradi wowote unaojaribu kuelewa mazingira
hayo, ni muhimu kwa kuanza kwa kuzungumza na wafanyakazi wenyewe.
Lengo la pili
inatakiwa kujua zaidi kuhusu sheria/taratibu za OSHA nchini Tanzania na kuona
ni aina gani ya mwingiliano wafanyakazi wa majumbani wanao na mamlaka za nchi
katika maeneo ya afya na usalama.
Nchini Brazil
watafiti walifanya kazi kupitia Sindoméstico, umoja wa wafanyakazi wa
majumbani. Nchini Tanzania, watafiti walifanya kazi na Chama Cha Wafanyakazi wa
Mahotelini na Majumbani (CHODAWU), umoja ambao pia unaratibu wafanyakazi wa
majumbani.
Orodha ya kukagulia
afya ni njia nyingine ya kuhamasisha washiriki katika mjadala wa pamoja
kuongelea kuhusu matatizo ya kiafya wanayokumbana nayo kutokana na kazi zao
bila kuongelea sana kuhusu matatizo yao binafsi.
Maeneo rasmi ya kazi
mara nyingi huweka orodha ya kukagulia afya, ambazo ni fomu zinazoorodhesha
matatizo ya kawaida ya majeraha na magonjwa ambayo hutokea katika eneo la kazi.
Ikitokea kwamba wafanyakazi wanaugua au kuumia, hutoa ripoti juu ya tukio hilo
katika sehemu zao za kazi na hurekodiwa au kuandikwa katika orodha ya kukagulia
afya.
Hii ina maana kwamba
viwango vya ugonjwa na kuumia katika sehemu ya kazi hufuatiliwa kwa makini na
endapo itatokea kwamba watu wengi wanaugua au kuumia katika sehemu fulani ya
kazi, vyama vya wafanyakazi au serikali inaweza kuingilia kati.
Wakati wa uchunguzi
katika makundi nchini Tanzania, watafiti walielezea dhana ya orodha rasmi ya
kukagulia afya mahali pa kazi kwa washiriki, ambao baadaye walitakiwa
kutengeneza orodha za kukagulia afya ambazo zitawasilisha matatizo ya kawaida
ya kiafya maalum kwa wafanyakazi wa ndani.
Njia hii pia
inahimiza majadiliano ya kutosha katika kundi au makundi kwa ajili ya kutafuta
mwelekeo au muongozo.
Taarifa za matokeo ya utafiti juu ya afya na usalama, mazingira mengine ya kazi
na mahusiano na mamlaka mbalimbali kuhusiana na afya na usalama zinasema nchini
Brazil, wafanyakazi wa ndani walisema matusi na udhalilishaji wanaokumbana nao
katika sehemu zao za kazi unawakilisha matatizo yao ya msingi ya kiafya na
kiusalama.
Walisema wanahisi
kama wanachukuliwa kama watumwa, ambao wametengenezwa kufanya kazi za
kiudhalilishaji, na mara nyingi wameonyeshwa kutoheshimiwa kama binadamu na
waajiri wao. Kama dondoo ifuatayo inavyoonyesha, matusi na udhalilishaji
umewaacha wakiwa na hisia za kutojithamini kabisa na hisia kwamba kazi
wanayofanya haina maana wala thamani:
“[Matatizo makubwa ni] kuitwa
majina yasiyofaa, kufedheheshwa na kusimama kwa vipindi au muda mrefu. Niliwahi kufanya kazi
katika nyumba fulani ambapo niliruhusiwa kuketi wakati wa kula tu. Endapo
ningekaa chini kupumzika kungetokea ugomvi au malalamiko, ilikupasa uwe
umesimama muda wote, hakuna ambaye aliweza kukaa katika nyumba yake
“... wanamnyonya msaidizi wao
wa nyumbani kwa kumfanya amhudumie mbwa wao pia, kwa kumuogesha. Sidhani kama
kuhudumia wanyama ni sehemu ya kazi za nyumbani...“ “Inatubidi tufanye vitu
ambavyo hatuna hata fununu ya jinsi ya kuvifanya, ambavyo hatujawahi kujifunza
jinsi ya kuvifanya, jinsi ya kuziba ukuta au jinsi ya kusafisha tanki la maji,
lakini tunalazimishwa kufanya vitu hivi na hii ni aina ya vurugu.“
Katika moja ya
makundi nchini Tanzania, wafanyakazi waliuchukulia unyanyasaji wa kijinsia kama
tatizo muhimu zaidi la kiafya na kiusalama linalowakabili. Mwanamke mmoja
alihusisha kisa cha jinsi alivyotoroka kutoka katika hali kama hiyo:
“Nilikuwa nimeajiriwa na mwajiri fulani katika mkoa wa Iringa kwa
takribani miaka 3...
nilikuwa na tatizo kubwa la unyanyasaji wa kijinsia ambapo baba na mwana walijaribu kunishinikiza
niwe na mahusiano ya kimapenzi nao, lakini mimi nikakataa!
Nilichokifanya, niliamua kumwambia jirani. Jirani akaniambia ni bora
kutoroka; akanisaidia kupata kazi Dar-es-salaam kwa ndugu yake. Ilikuwa ni kitu
cha hatari sana kwangu mimi nilipoamua
kutoroka bila hata ya kuwaambia wazazi
wangu ambao wanaishi Iringa vijijini...sifanyi kazi tena na mwajiri yule. Kitu
kibaya ni kwamba bado wazazi wangu wanafikiri nafanya kazi Iringa, kwa sababu
siwezi kuwasiliana nao.“
Usanisi wa Matokeo
ya Utafiti kutoka Brazil na Tanzania Ukosefu wa vifaa vya kujikinga pia ni
tatizo wakati wafanyakazi wa ndani wanapowahudumia wanafamilia ambao
wanaumwa-hususani kama wanaoumwa wana magonjwa yanayoambukiza kama vile VVU/
UKIMWI na/au TB.
Matatizo mengine
muhimu ambayo yalitajwa ni pamoja na kubeba vitu vizito na kulazimishwa kupanda
hadi mahali pa juu. Wafanyakazi wa majumbani wa Tanzania walikusanya pamoja
orodha ya kukagulia afya kwa wafanyakazi wa ndani ambavyo inaonesha baadhi ya
matatizo ya kiafya yanayotokana na hatari zilizotajwa hapo juu:
Hapa Tanzania
inaonesha wazi kwamba wafanyakazi wengi wa majumbani hawana habari juu ya haki
zao kuhusiana na masuala ya afya na usalama.Tatizo hili lipo kwa sababu
wafanyakazi wengi wa majumbani wanatokea katika mazingira ya kimasikini, mara
nyingi wana elimu kidogo, na wanatengwa kutoka katika makundi ya mengine ya
wafanyakazi.
Hii inamaanisha
kwamba, kwa pamoja, serikali na mashirika ya wafanyakazi wa majumbani
wanahitaji kufanya jitihada za makusudi kuwaelimisha wafanyakazi wa majumbani
kuhusu haki zao na kuhakikisha haki hizi zinazingatiwa.
inaendelea wiki ijayo.
Christian Gaya ni
mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala
ya hakipensheni au hifadhi ya jamii. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua
pepe: gayagmc@yahoo.com Au kwa habari
zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz
au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41
No comments:
Post a Comment