Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Dk Phillip Mpango, amemtaka Mbunge wa Tabora
Kaskazini, Almas Maige (CCM) kumpa ushahidi ikiwemo majina ya
wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliowatuhumu kufanya
biashara na mwajiri wao.
Dk Mpango alisema hayo Jumatano usiku alipokuwa akijibu hoja za
wabunge kuhusu Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango na kuongeza kuwa
akipewa ushahidi huo, ataufanyia kazi.
Awali katika mchango wake, Maige alisema anao ushahidi wa maandishi
(huku akiwa ameushika), unaoonesha kuwa kati ya mashirika ya umma
yanayovunja Sheria ya Manunuzi, BoT ipo.
Alidai kuwa Sheria ya Manunuzi imetoa fursa ya kuanzishwa kwa vitengo
na idara za manunuzi (PMU), lakini fursa hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya
na vijana wa vitengo, hivyo kuiibia Serikali.
Kwa mujibu wa madai ya Maige, katika benki hiyo kuna vijana
wamefungua makampuni ambao wamekuwa wakiyatumia kuomba zabuni za benki
hiyo na kuyalipa.
Mbali na tuhuma hiyo, Maige ambaye alitangaza maslahi kuwa yeye ni
mkandarasi wa daraja la kwanza, alidai pia kuna vijana wengine wamekuwa
wakitoa zabuni kwa kampuni za nje ya nchi, ili watumie zabuni hiyo
kupata safari za nje.
Alidai kuwa vijana hao baada ya kutoa zabuni kwa kampuni za nje,
hutengeneza safari za kwenda kufanya uhakiki (due diligence) katika nchi
zinakotoka kampuni hizo, ambako huko hupokea rushwa.
Katika kuthibitisha hilo, Maige alidai kuwa vijana hao wamediriki
kutoa zabuni kwa kampuni iliyofungiwa na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma
Tanzania (PPRA).
Akijibu hoja hiyo, Dk Mpango alisema tuhuma hizo ndio kazisikia
bungeni, hivyo hana uhakika ila akipewa ushahidi ataufanyia kazi kwa
kuwa, utumbuaji majipu umesaidia kuongeza mapato na kutoka mfano wa
makusanyo ya Sh trilioni moja kila mwezi.
Hivi karibuni, Serikali ilisitisha utoaji wa Sh bilioni 925
zilizokuwa zimeidhishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni
ya Serikali.
Mbali na hilo, Serikali iliagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho
awali kilikuwa chini ya BoT na baadaye kupelekwa wizarani, kirejeshwe
mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.
Kabla ya agizo hilo, ilielezwa kuwa malipo hayo yalikuwa
yameidhinishwa na BoT kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni
mbalimbali lakini Serikali ikaagiza fedha hizo zirejeshwe Wizara ya
Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki upya
No comments:
Post a Comment