Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKATI deni la Taifa likifikia zaidi ya Sh trilioni 35, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema Tanzania ina mahitaji
makubwa ya maendeleo yanayoilazimu kuendelea kukopa, kwa kuzingatia
vigezo vya kimataifa vya uhimilivu wa deni.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati akihitimisha mjadala wa bajeti
ya wizara hiyo ya Sh trilioni 9.5, Dk Mpango alisema kwa kuwa lazima
taifa likope ili kuleta maendeleo, ni lazima taifa liwe na madeni.
“Nchi yetu ina mahitaji makubwa ya maendeleo hivyo lazima tukope na
ukikopa, unaingia katika madeni,” alisema na kufafanua mambo ya msingi
yanayozingatiwa na Serikali wakati wa kukopa.
Jambo la kwanza wanalozingatia kwa mujibu wa Dk Mpango ni masharti ya
mkopo, yanayojumuisha riba ambapo wanaangalia riba hiyo ni kiasi gani;
muda wa kuanza kulipa baada ya kuchukua mkopo (grace period) na
utaratibu wa malipo.
Suala la pili la msingi kwa mujibu wa Dk Mpango, ni mahali fedha hizo
za mkopo zinakopelekwa ambapo alifafanua kuwa ukopaji wa Serikali hauna
tofauti na ukopaji wa mtu binafsi, ambaye akielemea anakaribisha
matatizo.
Dk Mpango alisema Tanzania inakopa kwa ajili ya kutengeneza
miundombinu, akatoa mfano wa ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya
Kinyerezi na ujenzi wa barabara nchi nzima, ambao mafanikio yake
yasingefikiwa bila mikopo.
Uhimilivu wa deni Pamoja na kuendelea kukopa na deni kuwa kubwa, Dk
Mpango alisema Serikali hufanya tathimini ya kimataifa kuhusu uhimilivu
wa deni kila mwaka ili kujiridhisha na mpaka sasa pamoja na deni hilo
kuonekana kubwa kimataifa, Tanzania ina fursa ya kuendelea kukopa zaidi.
Tofauti na inavyoelezwa kila mara na wanasiasa ambao wamekuwa
wakichukua deni la taifa na kugawanya kwa idadi ya watu, ili kupata
fedha zinazodaiwa kwa kila Mtanzania ikiwemo mtoto aliyezaliwa leo, Dk
Mpango alitoa vigezo ambavyo ni vya kimataifa kupima uhimilivu wa deni.
Vigezo hivyo vinavyotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni, ni
tofauti na kigezo cha kugawanya deni kwa idadi ya watu ambacho ni cha
kisiasa na hakitumiki popote duniani isipokuwa kwa wanasiasa wa
Tanzania.
Kigezo cha kwanza cha kimataifa cha upimaji wa uhimilivu wa deni kwa
mujibu wa Dk Mpango, ni uwiano kati ya deni la taifa na pato la taifa,
ambapo kimataifa deni halipaswi kuzidi asilimia 50 ya pato la taifa na
kwa Tanzania, deni lipo asilimia 19 tu ya pato hilo.
Kigezo cha pili kinachotumika kupima uhimilivu wa deni la taifa ni
deni la taifa kwa uwiano wa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Kimataifa, deni la taifa halitakiwi kuzidi asilimia 200 ya mauzo ya nje
na kwa Tanzania, deni la taifa ni sawa na asilimia 97 tu ya mauzo ya
huduma na bidhaa nje ya nchi.
Kigezo cha tatu kinachotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni la
taifa kwa mujibu wa Dk Mpango, ni uwiano wa deni la taifa na mapato ya
ndani. Kwa sasa kimataifa deni la taifa linatakiwa lisizidi asilimia 300
ya mapato ya ndani na kwa Tanzania, deni hilo la taifa ni asilimia
145.3 tu ya mapato ya ndani.
No comments:
Post a Comment