KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM,
Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, (kulia), akizungumza na uongozi wa
Kampuni ya New Habari kwenye makao makuu ya kampuni hiyo Sinza jijini
Dar es Salaam, leo Jumanne, Desemba 1, 2015.
NA
BASHIR NKOROMO
Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kimesema, kitampa ushirikiano mkubwa, Rais Dk. John
Magufuli, ili aweze kwa ufanisi zaidi mapambano yake dhidi ya mafisadi na
mikakati mingine ya kuinua uchumi wa Watanzania.
Kimesema, kitampa ushirikiano huo Rais Dk. Magufuli,
kwa sababu, aliyoanza kuyafanya na atakayoyafanya baadaye katika uongozi wake
wa Urais anatekeleza yale yaliyomo katika ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
2015-2020.
Hayo yalisemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye alipokuwa akijibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na baadhi ya
wahariri, aliokuwa akizungumza nao, katika ziara aliyofanya leo, katika
Kampuni ya New Habari Corporation, Sinza jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahariri, waliohoji ni kwa nini CCM
haijitokezi kumpongeza Dk. Magufuli katika juhudi ambazo ameanza kuonyesha
katika kupambana na ufisadi ikiwemo kubana fedha za walipa kodi ambazo
zingepotea bure katika masuala yasiyo ya lazima na wakati huohuo kuanza
kuwabana wafanyabiashara wanaodaiwa kukwepa kulipa ushuru.
"Yapo mengi tuliyoanisha katika ilani yetu ya
Uchaguzi, na yote yahahusiana sana na haya mnayoyaona yanafanywa na Rais Dk.
John Magufuli, tena Ilani hii tumeitunga hata kabla ya kumteua kugombea Urais,
Sasa anachofaya ni kuitekeleza ilani hii, isipokuwa mbinu anazotumia ni ubunifu
wake na hili hatuna tatizo nalo kama Chama maana kiongozi wa aina hii ndiye
tuliyemtaka", alisema Nape.
"Najua wapo wanaojaribu kutengeneza magingira ya
kumtaka kumtenganisha Dk. Magufuli na CCM, nawambieni Dk. Magufuli ni zao la
CCM na mwana CCM Kindakindaki, hivyo ni upotoshaji wa hali ya juu kujaribu
kuuaminisha umma kwamba anayofanya Dk. Magufuli hayana uhusiano na maelekezo ya
CCM", aliongeza Nape.
Alisema, baada ya kutengeneza ilani yake, CCM,
ilidhamiria kwamba, awamu hii ya tano ni ya kutafsiri uchumi katika nyanja za
huduma za Jamii, ikiwemo miundomboni, maji, afya na elimu.
"Ni kutokana na lengo hili, ndiyo sababu tukakaa
kwa makini na kuhakikisha ilani hii ya sasa tunamkabidhi mwana CCM ambaye
utekelezaji wake hautakuwa wa mashaka mashaka, Ndiyo huyo Dk. Magufuli, bila
shaka sasa na ninyi ni mashahidi mmeanza kuuona utekelezaji wake wa
ilani", alisema Nape.
Akizungumzia
kuhusu Rais Dk. Magufuli kuchelewa kutangaza Baraza lake la Mawaziri, Nape
alisema, Chama Cha Mapinduzi kimeshaunda serikali kwa kumpata Rais, kilichobaki
sasa ni kwa Rais mwenyewe kuteua watendaji wake, lakini katika kufanya hivyo
hakuna mda aliopangiwa kuanza kufanya hivyo na hashurutishwi na Chama wala
sheria.
Nape
alisema, Dk. Magufuli hachelewi kuteua Baraza la Mawaziri kwa sababu anakosa
wakuwateua, isipokuwa, anayo namna na mda ambao mwenyewe Kama Rais amejipangia,
na mda huo ukijiri wa kuamua kufanya hvyo atafanya.
"Tatizo
hapa ni kwamba mnayo kiu kubwa ya kutaka kujua nani atawateua, sasa kiu yenu
imepita kiasi, ndiyo maana mnaanza kuhoji, lakini mimi naamini Dk. Rais
Magufuli ataikata kiu yetu, wala msipate taabu ya kuhoji kila kukicha",
alisema Nape.
Nape
alisema, mbali na Chama kutengeneza ilani ambayo italeta mageuzi makubwa ya
kiuchumi hapa nchini, pia Watanzania watarajie kuona mageuzi makubwa ndani ya
CCM, kwa sababu yapo njiani kuwadia.
"Kama
ilivyo kawaida yetu, kila baada ya uchaguzi mkuu huwa tunafanya tathmini, baada
ya tathmini hiyo, huwa lazima tufanye mageuzi kwa yale ambayo tumebaini kuwa ni
kikwazo kwa uhai na maendeleo ya Chama katika nyanja mbalimbali, na mageuzi
haya tunayafanya kuzingatia mahitaji ya sasa na wakati ujao", alisema
Nape.
Kuhusu
Mwenyekiti wa sasa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumwachia Ueneyekiti Rais Dk.
Magufuli, Nape alisema, hayo si mambo mageni kwa CCM, imekuwa ikifanyika katika
awamu zote za Urais, hivyo Kikwete anaweza akaamua kumwachia kabla ya uchaguzi
mkuu wa CCM utakaofanyika mwaka 2017 au kabla ya hapo akiona inafaa.
Zanzibar
Akizungumzia mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa uchaguzi mkuu wa Rais wa
Zanzibar, Nape alikiri kamba ni mbaya na unaitia doa Tanzania, akisema, lakini
akasisitiza kwamba njia pekee ya kuumaliza ni kwa mazungumza baina ya viongozi
wa ndani bila kushirikishwa mataifa ya nje.
Alisema,
msingi wa mgogoro uliojitokeza Zanzibar, si wa kisheria, bali ni wa kisiasa
zaidi, hivyo juhudi ziwekwe kwenye mazungumzo kuutatua, na baada ya kuutatua
yaendelee kufanyika mazungumzo ambayo yataleta suluhisho la kudumu kwa kuwa
imekuwa ni kawaida kwa Zanzibar kuzuka migogoro kila baada ya uchaguzi mkuu
jambo linaloonyesha kuwa tatizo ni la asili zaidi kuliko inavyodhaniwa.
Katika mazungumzo yake na wahariri hao wa New Habari
Corporation Ltd, Wachapishaji wa magazeti ya Rais, Mtanzania na Dimba,
alivitaka vyombo vya habari nchini, sasa kushirikiana na Serikali kulijenga
taifa.
"Tunajua
wakati wa kampeni kulikuwa na mambo mbalimbali ambayo wakati mwingine vyombo
vya habari vililazimika kukampenia vinaowaona kuwa wanafaa kutokana na sababu
mbalimbali, lakini kama tulivyokuwa tukisema, kwamba baada ya uchaguzi maisha
yataendelea, sasa umefika wakati wa kuendelea na maisha tuwe kitu kimoja",
alisema Nape.
Alivitaka
vyombo vya habari, kusaidia kuishari Serikali na CCM, katika kutekeleza yaliyo
bora kwa taifa na hata pale vyombo hivyo vitakapoona kwamba Chama au serikali
vinaenda kinyume, visihofii kukosoa.
Kwa
upande wao, Mtariri Mtendaji wa Habari Corporation, Absalom Kibanda akimpongeza
Nape kwa ushirikiano ambao amekuwa akivipa vyombo vya habari, na kumtaka
aendelee kuwacha milango wazi kwa waandishi wa habari kama ambavyo amekuwa
akifanya.
Ziara hiyo ya Nape aliyoianza jana, kwenye vyombo vya
habari inatarajiwa kuendelea kesho kwa kutembelea vyombo vingine vya habari
vyenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahariri wa kampuni hiyo, kutoka kushoto, Asha Muhaji, Arodia, na Kimwanga
No comments:
Post a Comment