Mkulima mdogo mdogo wa nyanya ambaye ni mwanachama wa mfuko wa
pensheni wa hifadhi ya jamii ambao humwezesha mwanachama kupata mikopo ya riba
nafuu sana kwa ajili ya kununulia pembejeo, kusomesha watoto wao,na shughuli
nyingine za maendeleo. Kilimo ndio sekta mama ya uchumi wa Tanzania na
mpaka sasa inaajiri zaidi ya asilimia
70 ya wananchi.
Christian Gaya Mwananchi, Alhamisi, Novemba 12, 2015
Kwa mujibu wa takwimu za hivi
karibuni zinaonyesha kuwa wastani wa nguvukazi hasa vijana wasomi wanaotafuta
ajira kwa mwaka ni takriban 800,000 hadi 1,000,000. Hata hivyo, ajira rasmi
zinazopatikana nchini katika sekta ya umma na sekta binafsi ni kidogo, takriban
ajira 80,000 hadi 100,000 kwa mwaka.
Takwimu pia zinaonyesha kuwa kundi la
vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanakadiriwa kufikia milioni 8.3,
sawa na asilimia 19.8 ya watanzania.Vijana wasomi ndiyo wapo kwenye kundi hili.
Vijana wengine watarajiwa ni wale walio kwenye umri chini ya miaka 15.
Taarifa za idadi ya watu nchini
zinaonesha kuwa asilimia 44.4 ya Watanzania wote wana umri chini ya miaka 15.
Hili ni kundi lingine kubwa mno la Vijana watarajiwa ambao inabidi kuwaandaa
kama nguvukazi ya Taifa letu. Pamoja na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa, vijana
na wanachama inatakiwa wawezeshwe na kuwekewa mifuko ya uwezeshaji yenye
utaratibu maalum ulio wazi na mwepesi wa kupatikana kwa mikopo.
Miongoni mwa changamoto kubwa ambayo Vijana wengi wajasiriamali
wanaopenda kujiajiri wanakumbana nayo ni ukosefu wa mitaji na mikopo yenye
masharti nafuu. Taasisi nyingi za fedha nchini na benki za biashara zinatoa
mikopo kwa riba kubwa na masharti mengi, ambayo vijana na wanachama wa mifuko wengi
hawawezi kuyamudu.
Mifuko inatakiwa kusaidia kuleta
maendeleo kwa nchi kwa kuchangia kuanzisha miradi mbalimbali ambayo inaweza
kuajiri vijana ambao kama asilimia 90 ya vijana wa kitanzania hawana kazi na
kusaidia vijana wajasiriamali kuanzisha miradi yao ambayo baadaye husaidia tena
kuajiri baadhi vijana wengine. Idadi ya watanzania mpaka sasa imefikia milion
45 na asilimia 63 ya nguvukazi ni vijana.
Tatizo kubwa linalowasumbua
vijana ni ukosefu wa ajira. Hivyo mifuko inatakiwa kuwa na malengo ya makusudi
ya kuhakikisha kuwa inakuwa na miradi mbalimbali ambayo itasaidia vijana wa
kitanzania kupata kazi kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. Vijana wanatakiwa kuwa
wajasiriamali wazuri wenye ujuzi mbalimbali, na kuwa wavumbuzi na wabunifu wa
vitu mbalimbali vitakavyoweza kukuza uchumi wetu.
Lakini ieleweke wazi ya kuwa
lengo la mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni kwa ajili ya kumsaidia mfanyakazi
kumudu mahitaji yake ya uzeeni pindi anapostaafu ili kumsaidia uzeeni kwani
ilibainika kuwa wakati wa ujana, wafanyakazi wengi hushindwa kujiwekea akiba ya
kutosha wao wenyewe. Mifuko ni kama
ilivyo sera ya bima yaani mtu hulipwa pale anapopatwa na janga, na mahususi
kumsaidia mfanyakazi kununua vitu vya thamani kama vile viwanja au kujenga
nyumba anapostaafu au anapoelekea kustaafu.
Kutokana na umuhimu huo mifuko
inatakiwa kuwasaidia vijana na wanachama jinsi ya kuanzisha miradi mbalimbali
wakati bado wapo kazini kwa kutoa mikopo ya gharama nafuu kabla na pale wanapostaafu
na ndio maana mifuko inatakiwa kutoa kwanza malipo ya mkupuo wa pensheni ya
miezi kadhaa ili kuanzisha miradi ya aina mbalimbali kwa kusaidiwa na wataalamu
kutoka katika mifuko hiyo hiyo ya hifadhi ya jamii hasa kwa kutoa ushauri wa
kitaalamu juu ya uanzishwaji na uendesheshaji wa miradi. Lengo iwe kutoa huduma
zote muhimu pale wanachama na familia zao wanapopatwa na majanga ya aina
mbalimbali ambayo kwa sasa yamekuwa yakitokea mara kwa mara yakiwemo majanga
yanayosumbua wanachama kiuchumi na kijamii.
Mifuko hii inatakiwa
kuhahakikisha kuwa vijana na wanachama wake wanaopatiwa mikopo ya gharama nafuu
wanapata elimu ya ujasiriamali ya kutosha kwa kushirikiana na taasisi husika
ili wajue malengo ya mikopo ya biashara na hata pia kuelemishwa juu wajibu wao
kwenye mifuko, wajibu wa mwajiri, mafao yatolewayo na mifuko hii, jinsi ya
kuwekeza na kwa nini michango yao inawekezwa na faida ya riba wanayopata
kutokana uwekeza
Mifuko inatakiwa kuwa na mbinu za ubunifu wa hali ya juu hasa kwa
kufanya utafiti kwa kwenda mbele zaidi
kwa kuwatumia mawakala mbalimbali ambao wanaweza kutumika kuwaandikisha
wanachama kutoka katika sekta isiyo rasmi na walioko ughaibuni na hata katika
utoaji wa mikopo ya riba nafuu kwa wanachama wao kupitia waajiri wao kama
baadhi ya mifuko ilivyoanza kutekeleza mikakati, lengo kubwa likiwa kutaka
kuwafikia wanachama wengi zaidi kuliko kupitishia kwenye SACCOS ambapo wengi wa
wanachama sio wanachama wa SACCOS na hivyo kuwarahisishia kupata mikopo kwa
muda mfupi zaidi kuliko ilivyo sasa kwa mifuko mingi inavyotegemea SACCOS kama
chombo cha kuwafikishia mikopo wanachama wao ingawa kinaweza kuwa kivutia
kizuri cha kupata wanachama wapya kujiunga na mifuko
Hatimaye kwa kufanya hivyo itasaidia hata kujenga mshikamano zaidi
sehemu za kazi, na kuwasaidia waajiri kuongeza uzalishaji wenye tija zaidi na
hivyo kusaidia msukumo wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati
muafaka, kuwapunguzia ukali wa maisha wanachama na hivyo kupunguza umasikini
kama sio kuondoa kabisa, kinachotakiwa hapa ni mifuko kuweka utaratibu wa
masharti na kanuni nzuri zinatakazowavutia hata waajiri kutoa vibali vya
udhamini kwa wafanyakazi ambao ni wanachama wa mifuko hii kupata mikopo ya
gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment