Mkurugenzi Msaidizi Mifumo ya
TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Bw. Mtani Yangwe akifafanua
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam namna
mfumo wa wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki unavyorahisisha
ulipaji wa kodi mbalimbali kwa kuhusisha mifumo ya kielektroniki ya
malipo na mifumo ya kibenki. Kulia ni Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano
Serikalini wa ofisi hiyo Bi. Rebecca Kwandu.
…………………………………………………………………………………
NA Jovina Bujulu-maelezo- Dae es salaam
Mfumo wa malipo kwa njia ya
miamala ya kielektroniki umeweza kudhibiti, kupunguza na kuondoa mianya
ya ufujaji wa mapato na kuongeza uwazi katika ukusanyaji kodi kwa baadhi
ya miji hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar
es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Bwa. Mtani Yangwe.
“Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
iliamua kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato ya mamlaka
za serikali za mtaa ili kusaidia mamlaka katika kuongeza mapato ya ndani
na kuondokana na utegemezi wa ruzuku kutoka serikali kuu” alisema Bwa.
Yangwe
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo
huo halmashauri nyingi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto za kutofikia
malengo ya makusanyo ya kodi ukilinganisha na makisio waliyopanga.
Bwa. Yangwe aliendelea kusema
kwamba changamoto walizokuwa wanakutana nazo ni pamoja na kutokuwa na
orodha ya kumbukumbu za walipa kodi, uwazi katika makusanyo, uwajibikaji
wa watumishi na upotevu wa mapato yaliypkuwa yanakusanywa.
Aidha, alisema kwamba malengo
mengine ya kuanzisha mfumo huo ni pamoja na kupata taarifa za walipa
kodi wa Mamlaka za Serikali za mitaa na kuhifadhiwa kwa usahihi katika
kanzi data ya mfumo.
Mfumo huu pia hutoa hati za
madai umetengenezwa kuwa na dirisha linaloruhusu matumizi ya mifumo
mingine ya miamala ya kielektroniki kuwezesha ukusanyaji wa mapato
katika eneo la ndani ya halmashauri husika ama eneo lolote nchini pale
mlipa kodi anapopaswa kulipa kodi zinazomuhusu.
“Tamisemi imedhamiria
kuboresha huduma ya makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali za mamlaka ya
serikali ya mitaa ili iwafikie wananchi mahali walipo na kuondoa kero za
kufuata huduma na kupanga foleni muda mtefu” aliongeza Bwa. Yangwe
Mifumo ya kielektroniki
inayotumika katika ukusanyaji huo ni point of sale, huduma za kampuni ya
simu za m-pesa, Tigo-pesa, Airtel Money, Zpesa, mabenki na Maxmalipo.
Bwa, Yangwe alitaja faida za
mfumo huo kuwa ni pamoja na kutambua walipa kodi na eneo walipo,
kupunguza mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato na makisio sahihi
ya makusanyo.
Mradi huu wa malipo kwa njia ya
elektroniki uko chini ya Benki ya dunia na umeanzia katika miji ya
Dodoma, Mwanza-manispaa ya ilemela, Kigoma ujiji Manispaa, Arusha,
Mbeya, Tanga na Mtwara- manispaa ya Mikindani.
No comments:
Post a Comment