Na Joyce Mmasi na Kelvin Matandiko, Mwananchi
Kwa ufupi
- Vyama hivyo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kiti cha urais hadi udiwani, lakini kazi ya kugawana majimbo imekuwa ikivisumbua na ilitarajiwa kuwa ingemalizika juzi baada ya viongozi kukutana kwa siku mbili kuanzia Jumanne.
Dar es Salaam. Saa 48
zilizotumika kikaoni kutafuta muafaka wa majimbo yenye utata ndani ya
umoja wa vyama vya upinzani vilivyo chini ya Ukawa, zimekatika bila
mafanikio na mvutano unaonekana kubakia kwenye majimbo 12 kati ya 239
waliyopanga kugawana.
Vyama hivyo vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kiti cha urais
hadi udiwani, lakini kazi ya kugawana majimbo imekuwa ikivisumbua na
ilitarajiwa kuwa ingemalizika juzi baada ya viongozi kukutana kwa siku
mbili kuanzia Jumanne.
Lakini habari kutoka ndani ya kikao hicho
kilichofanyika jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa wajumbe walishindwa
kufikia muafaka kwenye majimbo 12.
Hata hivyo, viongozi hao wa vyama hivyo walikataa kutaja majimbo hayo yaliyosalia.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi
za makao makuu ya CUF, viongozi wa vyama vinne vinavyounda Ukawa, James
Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba
(CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD) walisema tayari wamefikia muafaka katika
majimbo 227 kati ya majimbo 239 yaliyopo nchini.
“Tangu juzi tupo hapa tukijadili namna ya kuwapata
wagombea wa Ukawa wa ngazi zote za udiwani, ubunge na urais. Kwa kiasi
kikubwa tumekamilisha kazi ya kupata wagombea ubunge kwa zaidi ya
asilimia 95 ya majimbo yote ya uchaguzi, majimbo 12 yaliyobaki
tunaendelea kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda si mrefu,”
alisema Mbatia aliyezungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake.
Viongozi hao, kila mmoja kwa nyakati tofauti,
walijigamba kuwa umoja wao huo upo imara na kwamba wale wanaopiga ramli
kuwa utavunjika, wataendelea kusubiri lakini kamwe jambo hilo
halitatokea.
Mbowe
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Mbowe alisema
hatua iliyofikiwa kwa sasa inatia matumaini ya kufanikiwa kwa mpango wa
kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge, udiwani na urais.
“Kwa wale wanaopiga ramli ya kuvunjika kwa Ukawa
hawatafanikiwa. Tutasimamisha mwakilishi mmoja kuanzia udiwani, ubunge
mpaka urais. Tunajua hitaji la Watanzania kwa sasa ni kuwaondoa kwenye
kifungo cha CCM,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kuhusu mvutano wa majimbo hayo 12,
Mbowe alisema siyo jambo la kushangaza kwa vyama vinne kutovutana katika
mgawanyo wa majimbo hayo kwani kila chama kinajiamini na kinahitaji
kupata mwakilishi.
“Tuko vyama vinne, itakuwa ajabu kama mvutano
utakosekana, lakini tumepata asilimia 95. CCM wenye chama kimoja
hawajatangaza mgombea hata mmoja.”
No comments:
Post a Comment