Abdul-wakil H. Hafidh Mkurugenzi mkuu wa ZSSF
Christian Gaya, Majira Septemba 30, 2014
Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii wa Zanzibar ulianzishwa chini ya kifungu cha sheria Namba 2 ya mwaka 1998
na baadaye ilirekebishwa chini ya kifungu cha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
Zanzibar, Sheria Namba 9 ya mwaka 2002 na Sheria Namba 2 ya mwaka 2005. Kabla
ya kifungu cha Sheria na uanzishwaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar,
kulikuwa hakuna rasmi mpango wa kinga ya hifadhi ya jamii katika nchi ya
Zanzibar. Wala hapakuwa na umuhimu kwa sekta isiyo rasmi kupatiwa kinga ya
hifadhi ya jamii
Kabla ya kuanzishwa kwa
mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar, wafanyakazi wa umma katika serikali ya
mapinduzi ya Zanzibar walipata pensheni chini ya Sheria Namba 2 ya 1990
Dira ya mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar yaani ZSSF
unalenga kuwa ni taasisi ya mfano ya utoaji wa hifadhi ya jamii katika ukanda
wa Afrika Mashariki inayojumuisha nchi zilizo chini ya jumuiya ya Afrika
Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Katika kutekeleza dira hii, mkurugenzi mkuu wa ZSSF
anasema dhima ya mfuko ni kwamba umedhamiria Kutoa mafao ya hifadhi ya Jamii endelevu kwa
kutumia wafanyakazi mahiri na wenye ujuzi walionao.
Abdul-wakil
H. Hafidh ambaye ndiye Mkurugenzi mkuu wa ZSSF anasema lengo kubwa la mfuko ni kuhakikisha ya kuwa
linawarejeshea kipato wanachama wake kutokana na majanga kama vile uzee,
ugonjwa, kupoteza sifa ya kufanya kazi na kifo.
“Hifadhi ya Jamii ni haki ya kila
mtu.
Haki hii imeanishwa katika Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1). Haki
hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka
1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka
1952” mkurugenzi mkuu anasisitiza.
Anaongeza
kwa kusema ya kuwa idadi kubwa ya nguvukazi ya Wazanzibar inashughulika na
sekta isiyo rasmi na wote wako katika hali hatarishi kwa vile hawana kinga
yeyote ya hifadhi ya jamii. Kuziba pengo hilo Abdul Wakil-Haji Hafidhi ambaye
ndiye mkurugenzi mkuu anasema Sheria
ya Mfuko inaruhusu wanachama kutoka katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi
kujiunga na Mfuko yaani. Mfuko unawaandikisha wanachama kutoka sekta isiyo
rasmi kwa kupitia mfumo wa hiari unaojulikana kama ZVSS.
Hafidh anataja majukumu makuu ya Mfuko huu wa hifadhi ya jamii
Zanzibar ya kuwa ni, Kuandikisha
wanachama; Kukusanya michango kutoka kwa wanachama hao; Kuwekeza michango hiyo
kwa kufuata sera ya uwekezaji ya Mfuko ambayo inazingatia Mwongozo wa Uwekezaji wa Kimataifa na kulipa mafao kwa wanachama pale wanapotimiza masharti
ya kustahili mafao hayo.
“Kutokana na
mikakati tuliyokuwa tumejiwekea na
kuitumia ipasavyo kwa mwaka 2012/2013 mfuko uliweza kuandikisha wanachama wapya
wapatao 2,927 na hivyo kufikisha jumla
ya wanachama wapatao 67,584 kwa mwaka 2012/2013 kutoka wanachama wapatao 64,657
kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 ambayo hii ni ongezeko wa asilimia 4.5”
anabainisha mkrugenzi mkuu.
Anasema ili kuweka usawa wa njinsia zote mfuko wa
hifadhi ya jamii Zanzibar ili kuhakikisha ya kuwa kunakuwepo na usawa wa kutoa
kinga ya hifadhi ya jamii kwa wazanzibar wote kwa mwaka 2011/2013 mfuko ulikuwa
na jumla ya wanawake wapatao 26,733 na wanaume 37,924 kama wanachama hai
wachangiaji wa mfuko, wakati kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 mfuko una jumla ya idadi ya wanawake wapatao
27,984 na jumla ya wanaume wapatao jumla ya 39,600 wote wakiwa wanachama hai
wachangiaji wa mfuko.
Mkurugenzi mkuu
anafafanua ya kuwa Mwanachama mnufaikaji yaani mwajiriwa ni yule mtu ambaye
amesajiliwa na analipia michango katika Mfuko huu wa ZSSF.
“Mwaajiriwa anaweza
kuwa ni mwanachama aliyesajiliwa na ZSSF kutoka Wizara na Idara za Serikali,
Mashirika ya Umma, Sekta binafsi ambazo zinajumuisha: Makampuni, taasisi
binafsi na asasi zisizo za Serikali pamoja na taasisi zisizo rasmi. Mwanachama
aliyechangia katika Mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi sitini atastahiki
kupatiwa mafao kutoka katika Mfuko huu” Hafidhi
anasistiza.
Mpaka kufikia mwaka wa fedha 2012/2013 mapato kutokana
na makusanyo ya michango yameongezeka kutoka shilingi za Kitanzania yaani
bilioni 19.81 kwa fedha ya kitanzania kwa mwaka 2011/2012 mpaka kufikia fedha
za kitanzania zipatazo bilioni 24.82 hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 25. Na
kwa upande mwingine mkurugenzi mkuu anasema mapato kutokana na vyanzo
mbalimbali vya uwekezaji yameweza kuongezeka kutoka shilingi za kitanzania
zipatazo bilioni 13.18 kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 mpaka kufikia shilingi
za kitanzania bilioni 16.07 kwa mwaka 2012/2013 ikiwa kama ongezeko la asilimia
22 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita.
Anasema ya kuwa katika mwaka wa fedha huo huo wa
2012/2013 malipo ya mafao ya wanachama yaliongezeka kwa asilimia 37 kutoka
shilingi za kitanzania zipatazo bilioni 4.75 kwa mwaka wa fedha wa 2011/2013
mpaka kufikia fedha za kitanzania zipatazo bilioni 6.50 na ongezeko hili la
malipo ya mafao yalitokana na ongezeko la idadi ya wastaafu na wakati shilingi
zipatazo million 440.21 zililipwa kwa wanachama wa kigeni au raia wa kigeni.
Mafao
ya uzeeni ni moja kati ya mafao ya muda mrefu yanayotolewa na Mfuko wa ZSSF na
kulipwa mwanachama aliyetimiza umri wa kustaafu kazi. Mwanachama anaweza
kustaafu kazi kwa hiari anapotimiza umri wa kuzaliwa wa miaka 55 hadi 59; au
kukastaafu kwa lazima anapotimiza umri wa kuzaliwa wa miaka 60 kwa mujibu wa
sheria ya ZSSF.
Anasema
Mafao ya uzeeni hujumuisha Kiinua
mgongo ambayo ni mafao ya mkupuo anayolipwa mstaafu aliyetimiza umri wa
kustaafu kwa hiari yaani miaka 55 hadi 59 au umri wa kustaafu kwa lazima yaani
miaka 60 na pia awe amechangia Mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 60. Wakati
Pensheni ya uzeeni
Ni malipo ya kila mwisho wa mwezi ambayo hulipwa mwanachama kila mwisho wa mwezi tangu alipostaafu mpaka atakapofariki dunia.
Mkurugenzi mkuu anataja ya kuwa thamani ya Mfuko wa
hifadhi ya jamii Zanzibar yaani ZSSF imekua kutoka shilingi bilioni 110.72 kwa
fedha ya kitanzania kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hadi kufikia shilingi bilioni
141.63 za kitanzania kufikia mwaka wa fedha wa 2012/2013, ikiwa ni ongezeko la
asilimia 28 ikiwa ni kutokana na ongezeko la .michango ya wanachama, adhabu ya
kuchelewesha michango kutoka kwa waajiri na mapato kutokana na vyanzo vya
uwekezaji.
Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 mkurugenzi anasema
mfuko uliendelea kuwaelemisha wanachama wake na wadau wengine, kuboresha
uhusiano, kuwaaandikisha wanachama wapya na kutoa kadi kwa wanachama wapya na
lengo kubwa likiwa ni kuwaandikisha wanachama zaidi ili kufikisha malengo
pamoja na kupanua wigo zaidi kwa Wazanzibar walioko kwenye sekta rasmi na wale
ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi na wazanzibar waishio ughaibuni kujiunga na
mfuko.
Mkurugenzi mkuu anasema misingi ya
maadili ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ni kutoa huduma zake kwa
wanachama na umma kwa ujumla chini ya misingi ya: Uadilifu; Uwajibikaji;
Umahiri; Heshima; Ufuatiliaji; Kwenda na wakati; Uwazi; Kuwajali wanachama wake
na Kufanya kazi kwa mashirikiano.
Anataja
sifa za ziada za mafao yatolewayo na ZSSF anasema malipo ya mafao ya mfuko wa
ZSSF ni makubwa kuliko Mfuko wa pensheni mwengine wowote wa Hifadhi ya Jamii
Tanzania, anaendelea kutaja ya kuwa mafao yanayotolewa na mfuko wa ZSSF hulipwa
katika kipindi kifupi sana tokea mwanachama kukamilisha taratibu husika.
Na
kwamba malipo ya mafao ya mfuko wa ZSSF hufanyika baina ya ZSSF na mwanachama mhusika
na hayapitii kwa mwajiri, taasisi nyengine au mtu mwengine yeyote. Mafao
yanayotolewa na ZSSF hayabagui; hutolewa kwa wanachama wote walio raia na wasio
raia wa Tanzania kama ilivyoainishwa katika tamko la Umoja wa Mataifa juu ya
Hifadhi ya Jamii, na kuongeza ya kuwa mfumo wa hifadhi ya jamii ambayo ni ya
lazima kisheria ambapo wafanyakazi pamoja na mwajiri wanatakiwa kuchangia
pamoja na kupeleka michango kwenye chombo cha mfuko wa pensheni au mfuko wa
akiba ya wafanyakazi. Na anamalizia kusema ya kuwa
taarifa za malipo ya mafao huwa siri baina ya ZSSF na mwanachama au mlipwaji
muhusika siyo vinginevyo.
Hafidh ambaye ndiye mkurugenzi
mkuu wa ZSSF anasema wanayo nia ya kutanua zaidi wigo wa maeneo ya uwekezaji
kwa kuongeza miradi ya ubia na miradi mingine inayolenga mapato na rasilimali
za mfuko na ili kuhakikisha kuwa mfuko unavutia zaidi, na wataendelea kuboresha
katika utoaji wa huduma na mafao yanayotolewa ili kuhakikisha ya kuwa muda wote
ZSSF inakuwa chaguo la kwanza kwa wananchi wanaotafuta huduma ya hifadhi ya
jamii nchini na kwa Afrika Mashariki nzima, wataendelea kujitangaza ili
wananchi wengi zaidi kuelelewa mfuko, pamoja na mafanikio hayo ya mfuko bado
unazo changamoto mbalimbali ambazo unakumbana nazo: changamoto hizo ni pamoja uelewo mdogo juu ya
mfumo wa hifadhi ya jamii, maeneo ya uwekezaji kuwa finyu, waajiri
kutowasilisha michango kwa wakati muafaka, mfumuko wa bei na kushuka kwa
thamani ya fedha, hata hivyo mfuko utaendelea kujipanga ili kuhakikisha kuwa
changamoto hizo hazileti athari katika uendelevu wake.
Mwisho mkurugenzi mkuu wa
mfuko wa ZSSF anatoa wito kwa wananchi wote waishio nchini na nje ya nchi walio
katika sekta rasmi na isiyo rasmi, pamoja na wageni waishio nchini kisheria
kujiunga na mfuko wa ZSSF ili wanufaike
na fursa mbalimbali zilizopo pamoja na mafao bora yanazozingatia thamani ya
fedha kwa wakati huo. Anasisitiza ya kuwa mtu yeyote mwenye umri usiopungua
miaka 18 anaweza kuwa mwanachama wa ZSSF awe ni mkulima, mfugaji, mvuvi,
msanii, mjasiriamali na hata wanafunzi. Anasema hata kwa wale watu ambao
wanapata ajira rasmi katika sekta yeyote wanaruhusiwa kujiunga na mfuko wa hifadhi
ya jamii ya ZSSF. Hivyo wewe mwajiriwa unafursa kuu ya kujiunga na mfuko wa
ZSSF ili utakapostaafu uje uishi maisha yenye kinga ya majanga kamili na ndio
maana kauli mbiu yetu inasema mfuko wa ZSSF ni ufunguo wa maisha ya baadaye.
No comments:
Post a Comment