Baadhi ya wasanii wa filamu Tanzania
Tasnia ya filamu, kama ilivyo muziki wa kizazi kipya, ni miongoni
mwa fani zilizofanya mapinduzi makubwa katika miaka ya hivi karibuni
hapa nchini.
Pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili tasnia hii, biashara ya
utengenezaji,usambazaji na uoneshaji wa picha jongevu (filamu ama sinema
kama wengi tulivyozoea) imezidi kukua kwa kasi sambamba na fursa za
ajira kwa mamia ya vijana, ongezeko la vipato kwa wahusika, mapato kwa
serikali na faida nyinginezo.
B. CHANGAMOTO KATIKA TASNIA YA FILAMU
Kama tulivyodokeza hapo juu, taaluma ama biashara hii ya filamu
Tanzania imenufaisha wengi lakini wakati huo huo kumekuwepo na matatizo
lukuki ambayo yamelazimisha uhitaji wa mabadiliko ya lazima katika sera,
sheria, taratibu na miundo-mbinu ya kitaasisi inayohusiana na tasnia
hii.
Mathalani, baadhi ya changamoto zilizo dhahiri ni kuendelea kuwepo
kwa mitizamo hasi miongoni mwa Watanzania walio wengi kuwa wasanii wa
hapa nyumbani hawana ubunifu, umahiri na uwezo wa kuburudisha ipasavyo
kama wenzao wa Hollywood (Marekani), Bollywood (India) ama Nollywood
(Nigeria) na kwingineko ama soko la filamu ni kubwa zaidi na la siku
nyingi.
Matatizo mengine yanayoikabili tasnia ya filamu nchini na ambayo
hayajapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu ni uwepo wa mikataba mibovu baina
ya wasanii kwa upande mmoja na waandaaji, watengenezaji ama wasambazaji
kwa upande mwingine, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kwa wasanii
walio wengi kuendelea kuishi maisha ya kubahatisha huku wakiwatajirisha
wenzao wachache kupitia migongo ya juhudi na umaarufu wao katiki skrini.
Mwiba mwingine katika kuongeza maumivu ya soko lisilodhibitiwa na
unakilishaji usioidhinishwa na wizi unaoendelea kufanywa waziwazi kwa
kazi za sanaa za filamu na muziki hapa nchini.
Zaidi ya hayo, hakujafanyika juhudi madhubuti kupitia serikali,
asasi zisizo za kiserikali, taasisi binafsi na hata miongoni mwa wasanii
wenyewe kuweka msimamo wa dhati katika uboreshaji wa bajeti, teknolojia
na uhamasishaji katika kile wanachokifanya, kwa faida yao na taifa
zima.
SHERIA, KANUNI NA TAASISI ZINAZOHUSIKA NA FILAMU
Baada ya kutambulisha maendeleo yaliyojiri, fursa zilizopo na
changamoto zinaoikabili tasnia ya filamu nchini, turejee sasa katika
mada iliyokudiwa kuwasilishwa hapa leo-kuuelimisha umma na
kuwakukumbusha wahusika wa tasnia ya filamu kuhusiana na sheria na
taratibu muhimu zilizopo na zinazopaswa kuzingatiwa katika masuala ya
leseni, utengenezaji, usambazaji ama uonyeshaji wa picha jongevu (filamu
na sinema).
Kanuni Kuu na zilizo muhimu zaidi zinazohusika na Tasnia ya Filamu
Tanzania zinatambulika kisheria kama ‘Kanuni za Sheria ya Filamu na
Michezo ya Kuigiza za Mwaka 2011’. Kanuni hizi zimeandaliwa na
kuchapishwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 156 la mwaka 2011.
Muhimu kuzingatia ni kwamba Kanuni za zilizopo za filamu
ziliandaliwa na kuchapishwa na Waziri mwenye Mamlaka ya kusimamia Sheria
ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (Sura ya 230 ya Sheria za Nchi), Toleo
la mwaka 2002).
Katika hili ni vema pia kwa msanii na yeyote yule anayehusika na
biashara ya filamu nchini kutofikiria kuwa Kanuni hizi (tangazo namba
156 la mwaka 2011) ndizo pekee zinazoongoza tasnia hii.
Mathalani, Chini ya Sheria hii ya Filamu na Michezo ya Kuigiza
(hujulikama kimombo kama Films and Stage Plays Act) kumetolewa Kanuni
mbalimbali tangu sheria hii ilipotungwa na Bunge mwaka 1976 na ni jukumu
basi la mhusika mwenyewe kufuatilia ili kuelewa ni kanuni zipi
zinaendelea kutumika na kwa mambo gani anayohusika nayo.
Uelewa wa mambo haya ni muhimu kwa sa sababu utakufanya wewe msanii
ama unayehusika na biashara hii kufanya maamuzi kwa kujiamini katika
kusimamia maslahi yako na pia kuelewa wajibu wako kwa mujibu wa Sheria
za nchi.
Kwa mfano, zaidi ya Tangazo namba 156 la mwaka 2011, kumekuwepo pia
na Kanuni nyingine chini ya Sheria hii ambazo zimechapishwa kupitia
Matangazo ya Serikali namba 435 la mwaka 1995, 315 la mwaka 1999 na
Tangazo la Serikali namba 73 la mwaka 2004.
Tukirejea katika Kanuni za Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka
2011, baadhi ya mambo muhimu yaliyomo humo ni matumizi ya maneno ya
Kisheria. Chini ya Sheria hii neno muhimu sana kulifahamu ni ‘Picha
Jongevu’.
Msamiati huu si maarufu sana mitaani lakini chini ya Sheria hii una
maana ya ‘mpangilio wa picha zinazoonekana na zilizorekodiwa katika
kifaa chochote kwa mfumo wa digitali, seluloidi au kwa namna yoyote
ambayo picha hiyo inaweza kujongea na inajumuisha picha zilizoko katika
filamu, video, katuni na picha zinazofanana na hizo’.
Ndiyo kusema basi picha, sauti na mitiririko iliyomo katika filamu
zilizozoeleka za akina hayati Kanumba, Wema Sepetu na nyinginezo ni
‘picha jongevu’ na ambazo uandaaji, utengenezwaji, usambazaji, uuzwaji
na uonyeshwaji wake ulipaswa ama unapaswa kuzingatia kanuni
tunazozifafanua hapa.
Jambo jingine muhimu ni kuhusiana na eneo la Kijiografia katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo Sheria hii inahusika. Kanuni
namba 2 iko wazi kabisa kwamba Sheria hii hutumika Tanzania Bara tu.
Hivyo, basi, mtengenezaji wa filamu ama ‘picha jongevu’ aliyeko
Tanzania Bara na ambaye anataka kurekodi akiwa Tanzania Visiwani
(Zanzibar ama Pemba) tukio fulani ndani ya filamu hiyo atapaswa
kuzifahamu Sheria zinazohusiana na filamu zinazotumika huko ili kwamba
asije akafanya jambo ambalo ni halali chini ya Sheria za Bara lakini
likawa ni haramu chini ya Sheria za Zanzibar kwa sababu, kama
tulivyoona, iwapo anashtakiwa huko, haitarajiwi kwamba atatumia Kanuni
hizi kujitetea huko.
Ukweli huu ni ule ule kwa Msanii kutoka Zanzibara anayekusudia
kufanya hivyo Tanzania Bara. Ni muhimu basi kwa wasanii na
wafanyabiashara wa filamu nchini na hasa wanaofanya biashara pande zote
za Muungano kuzifahamu vilivyo sheria zinazohukika kote.
Jambo la tatu muhimu kulielewa ni taasisi zilizopewa dhamana katika
masuala mbalimbali ambayo msanii ama mfanyabiashara wa filamu anapaswa
kuzifahamu kwa sababu aghalabu atapaswa kufika katika ofisi husika ama
kufanya mawasiliano nazo katiika masuala muhimu kama utoaji wa leseni na
vibali, kupata miongozo, uwasilishaji malalamiko, utatuzi wa migogoro,
ukataji wa rufaa na kadhalika. Chini ya Sheria ya Filamu na Michezo ya
Kuigiza ya mwaka 1976 na Kanuni zake za mwaka 2011 taasisi muhimu zaidi
ni pamoja na Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza;
Bodi Kuu ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza na Waziri
mwenye dhamana ya mambo yanayohusiana na Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya
Kuigiza.
Kwa utaratibu wa sasa. Waziri anayehusika na mambo haya ni Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali namba 494A la mwaka 2010 (Angalia Tangazo la Serikali
liitwalo‘The Ministers (Discharge of Ministeria Functions), Notice, 2010
lililotolewa Chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Wajibu wa Mawaziri (Sura
ya 299).
Taasisi, Asasi na Wadau wengine muhimu katika usimamizi na
utekelezwaji wa Sheria na Kanuni za filamu ni pamoja na Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA),Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Utamaduni Tanzania, Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni Bagamoyo(TaSUBa), ZIFF (Zanzibar), Bodi ya Filamu
Zanzibar, Ofisi ya Rais, Wizara za Serikali na kadhalika.
Kulingana na maelezo hapo juu ni mambo mawili yanweza kuzua maswali kuhusiana na Kanuni hizi.
Mosi, Kanuni namba 2 ya Kanuni za filamu inaainisha kuwa Kanuni
hizi zitatumika Tanzania Bara tu lakini katika Jedwali la Tano
lililotengenezwa kupitia Kanuni namba 51, Bodi ya Filamu Zanzibar na
ZIFF (Zanzibar) mi miongoni mwa asasi 17 zilizotamulishwa kuwa
zitashirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania. Hili linaweza lisilete
mgongano kwa sababu linazungumzia ‘kushirikiana’.
Pili, inaweza kuzua swali kubwa kwamba hakuna asasi yoyoye ya
vyombo vya habari iliyotajwa katika jedwali hili miongoni mwa asasi hizo
za ushirikiano.
*Juma lijalo tutamalizia kwa kuangalia taratibu husika kama uombaji
vibali, ada na masharti ya utengenezaj, uonyeshaji na usambazaji filamu
Tanzania.
Kumbuka kuwa maelezo haya ni ya ujumla tukulingana na ufinyu wa
nafasi hii ukilinganisha na wingi wa kanuni husika na kwa kuzingatia
kwamba maelezo haya lengo lake ni kutoa elimu ya msingi na si kuwa
mbadala wa ushauri wa kitaalam wa kisheria, jambo ambalo ni la hatari na
lisiloshauriwa kwa mhusika kulifanya kwa sababu uelewa wa sheria
huhitaji elimu ya kina, uzoefu wa muda mrefu na umakini wa hali ya juu.
*Denis Maringo ni Mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. dnmaring
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment