Na Christian Gaya Majira 23 Oktoba 2020
Mojawapo ya haki za mafao ya uzazi na wajawazito ni pamoja na haki zinazomwezesha mwanamke mwajiriwa kutimiza majukumu yake ya uzazi na ujauzito, na kufanya kazi au kuzalisha bila kubaguliwa, kubugudhiwa au kupoteza ajira.
Ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi katika kazi unawapa fursa wanawake kuchanganya kazi na majukumu yao ya kifamilia kama vile ujauzito na kadhalika, bila ya kuhatarisha mojawapo ya hivi vyote vinavyohusiana. Pia kwa kufanya hivyo inawasaidia wanawake wajawazito na wazazi dhidi ya ubaguzi katika soko la ajira.
Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilianza kushughulika na masuala ya ulinzi wa haki za uzazi au wajawazito toka lilipoanzishwa na maazimio ya kwanza juu ya ulinzi wa uzazi yalipitishwa tangu ILO ilianzishwa mwaka 1919.
Azimio hilo la haki za uzazi au wajawazito linaeleza pamoja na mambo mengine haki za msingi za wajawazito kama wiki 12 za likizo ya uzazi yenye malipo yaani kiwango cha malipo katika kipindi cha likizo hii kitapangwa na taasisi za serikali katika nchi husika kama vile mifuko ya hifadhi ya jamii, mapumziko ya kunyonyesha na ulinzi wa kazi kipindi cha ujauzito.
Ingawa azimio hili hasa linalenga wanawake walioajiriwa katika sekta binafsi na za umma za viwanda na biashara.
Ambapo azimio la pili lilipitishwa mwaka mwaka 1952 ambalo lilitanua wigo na kujumuisha wanawake wanaofanya kazi katika sekta zisizokua za viwanda pamoja na kilimo na wafanyakazi wa ndani.
Vile vile azimio hili la mwaka 1952 liliongeza likizo ya angalau wiki 12 ambazo zitatolewa pia kwa magonjwa yatokanayo au yanayosababishwa na mimba.
Azimio la 183 lililokubaliwa mwaka 2000 limetanua wigo wa ulinzi wa haki za wajawazito na uzazi kwa wafanyakazi wote na kutoa angalau wiki 14 za likizo ya uzazi yenye malipo.
Ulinzi wa haki ya wajawazito na wazazi ni muhimu kwa sababu inamuwezesha mwanamke kuchanganya majukumu ya uzalishaji kiuchumi na kujenga familia bila ya kuhatarisha kimojawapo kinachomhusu.
Vile vile humlinda mwanamke dhidi ya unyanyapaaji katika soko la ajira kutokana na majukumu yake ya kujenga familia.
Ulinzi wa haki ya wajawazito na wazazi inachangia katika afya ya uzazi na watoto na hivyo kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya millennia (MDGs) namba 4 na 5.
Pia ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi unalinda na kuongeza ajira za wanawake na uwepo wao katika soko la ajira na kuhakikisha ulinzi wa kipato kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha taslimu na mafao ya matibabu katika kipindi cha ujauzito na hivyo kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya millennia namba 1 na 3.
Na ndiyo maana mifuko ya hifadhi ya jamii inasisitizwa kutoa mafao ya uzazi kwa muda muafaka kwa wanachama wao wajawazito na wazazi ili iweze kuwasaidia kwa muda huo na siyo vinginevyo.
Malengo ya maendeleo ya millenia na makusudio ya suala la ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi ni kutaka kuongeza pato la taifa kwa mtu aliyeajiriwa na kuongeza wastani wa ajira na idadi ya watu na
Kusudio lingine ni kutaka Kufikia ajira za kudumu zenye kuzalisha na kazi za staha kwa wote, ikijumuisha wanawake na vijana na kutaka kupunguza idadi ya vifo vya watoto na lengo lingine likiwa ni kutaka kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake, na pia kuboresha afya ya uzazi
Kuna vipengele kadha wa kadha vya ulinzi wa haki za wajawazito na wazazi kimojawapo ni pamoja na likizo ya uzazi.
Vipengele vingine ni pamoja na ulinzi wa afya ya mama mjamzito na mwenye kunyonyesha, likizo ya uzazi, likizo inayouhusiana na magonjwa yatokanayo na ujauzito, utoaji wa fedha taslimu na mafao ya matibabu, ulinzi wa ajira na ubaguzi, kutoa ruhusa kwa mama anaenyonyesha.
Malengo haya yatafikiwa kama tu nchi husika itaamua kutengeneza sheria inayolinda haki za wazazi na wajawazito na kuzisimamia ili kuhakikisha zinafuatwa na makampuni husika yaliyoajiri hao wafanyakazi.
Ikumbukwae ya kuwa Azimio 183 la ILO linatambua haki za wajawazito na wenye kunyonyesha na kuzilinda. Taasisi za kitaifa zinatakiwa kutambua aina za kazi ambazo zinaweza kua na madhara kwa afya ya mama au ya mtoto. Hatua mojawapo muhimu ya kulinda afya ya mfanyakazi mwenye ujauzito ni mpangilio wa saa za kazi. Kwa kawaida wajawazito hupata unafuu na hivyo hulindwa na kazi za usiku na zile za muda wa ziada.
Awali maazimio ya ILO yalikataza kazi za usiku kwa wanawake. Hata hivyo kama kigezo cha usawa wanawake hawawezi kuzuiwa kufanya kazi za usiku. Hivyo hata wafanyakazi wajawazito hawakatazwi kufanya kazi za usiku ila wanaruhusiwa kuamua wenyewe. Maamuzi ya kukataa mfanyakazi mjamzito kufanya kazi za usiku au katika muda wa ziada yanaitajika yatolewe kutokana na ushauri wa daktari ukithibitisha kwamba kazi za usiku au katika muda wa ziada haziendani na mimba au kunyonyesha.
Kama kazi itakua na madhara kwa afya ya mfanyakazi mwenye ujauzito au mtoto basi mfanyakazi huyu atahitajika kupatiwa kazi mbadala, kama kumuhamishia katika nafasi salama. Hii pia inaweza kuwa ni pamoja na kubadilisha hali yake ya kufanya kazi na muda wa kufanya kazi.
Hata hivyo, kazi hiyo mbadala haitakiwi kumpelekea kupunguzwa mshahara au mafao yake. Uamuzi huu hufikiwa pale tu uchambuzi utakapoonyesha kwamba kazi ina madhara makubwa kwa afya ya mjamzito au mtoto.
Kutokana na azimio la 183 la ILO, mfanyakazi mwanamke ana haki ya mapumziko au punguzo la muda wa kufanya kazi kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto.
Taasisi za kitaifa ndizo zinazopanga kipindi na idadi ya mapumziko haya. Azimio la kwanza la ILO juu ya haki za ulinzi wa wajawazito na wazazi (Na.3), hata hivyo ilitoa mapumziko ya dakika 30 katika kila siku ya kazi.
Kama ilivyoelezwa na tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO), kunyonyesha mtoto mpaka umri wa miezi 6 na kidogo kidogo mpaka umri wa miaka 2 au hata zaidi ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto.
Mapumziko haya ya kunyonyesha ni tofauti na mapumziko ya chakula cha mchana na mapumziko ya kawaida. Pia lazima kuwepo na maelezo juu ya upatikanaji wa maeneo ambapo wafanyakazi wanawake wanaweza kunyonyesha watoto wao.
No comments :
Post a Comment