Thursday, June 13, 2019

Hotuba Ya Waziri Wa Fedha Akiwasilisha Bungeni Taarifa Ya Hali Ya Uchumi Wa Taifa Kwa Mwaka 2018 Na Mpango Wa Maendeleo Wa Taifa Wa Mwaka 2019/2020

Tokeo la picha la hotuba ya waziri wa fedha
UTANGULIZI
1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20. Pamoja na hotuba hii nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20, ambapo taarifa hizi ndio msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20 itakayowasilishwa Bungeni leo jioni.


2.            Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uzima na afya. Kipekee nimshukuru sana kwa jinsi anavyoendelea kulijalia Taifa letu amani na utulivu na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.

3.            Mheshimiwa Spika, Taifa letu limebarikiwa kuwa na kiongozi shupavu, mchapakazi, mwenye maono, na uthubutu wa kimaendeleo. Naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kuliongoza vema Taifa letu. Kwa kipindi hiki cha Miaka mitatu na nusu ya utawala wake

tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi ambapo ukuaji umefikia asilimia 7.0, mfumuko wa bei umedhibitiwa na kuwa katika tarakimu moja, miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa, uwajibikaji katika utumishi wa umma unaimarika na kero za wanyonge zinatatuliwa. Mimi na wenzangu Serikalini tunaahidi kuendelea kumpatia Mheshimiwa Rais ushirikiano wa hali ya juu. Aidha, ninamshukuru kwa kuendelea kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango.

4.            Mheshimiwa Spika, kipekee naomba niwapongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, kwa uongozi wao mahiri katika kumsaidia Mheshimiwa Rais. Aidha, naomba kumpongeza Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

5.            Mheshimiwa Spika, hoja ninayoiwasilisha hapa imetayarishwa kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa jamii ambapo tumepata maoni na ushauri kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii na Taasisi za Serikali. Siwezi kuwataja mmoja mmoja wale wote waliotoa

maoni na ushauri hadi kufikia hapa, lakini ni vema nitambue mchango mkubwa wa Bunge hili kupitia kwako Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, nichukue fursa hii adhimu kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb) na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki (Mb) pamoja na wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa ushauri makini waliotupatia wakati wa uandaaji wa kitabu cha Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20. Ushauri wao umetumika kikamilifu katika uandaaji wa hotuba na vitabu ninavyowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu.

6.            Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 vimeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili kuleta mchango wa haraka katika maendeleo ya uchumi wa Taifa; umuhimu  wa kumalizia miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa; kuweka msukumo mkubwa katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini ili kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi na kujenga uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu.

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2018

Uchumi wa Dunia

7.            Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, uchumi wa dunia ulikua kwa asilimia 3.6 ikilinganishwa na ukuaji  wa asilimia 3.8 mwaka 2017. Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kulitokana na kushuka kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: kupungua kwa mahitaji ya bidhaa  na huduma kutoka nje; hali ya wasiwasi kuhusu madhara ya Uingereza kujitoa Jumuiya ya Ulaya (Brexit); kushuka kwa kasi ya uwekezaji; mvutano wa kibiashara baina ya China na Marekani; kudorora kwa soko la fedha katika nchi za Argentina na Uturuki, na mvutano wa kisiasa Mashariki ya Kati.

8.            Mheshimiwa Spika, Mwaka 2018, mfumuko wa bei wa dunia uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 3.8 kutoka wastani wa asilimia 3.1 mwaka 2017. Ongezeko hilo lilitokana na kupungua kwa uzalishaji viwandani hususan, katika nchi zinazoendelea, majanga ya asili, na kulegezwa kwa sera za bajeti na fedha kwa baadhi ya nchi. Mfumuko wa bei kwa nchi zilizoendelea uliongezeka na kuwa asilimia 2.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2017. Katika kipindi hicho, mfumuko wa bei kwa nchi zinazoendelea za Asia uliongezeka hadi asilimia 2.6 ikilinganishwa na asilimia 2.4 mwaka 2017.

Uchumi wa =Afrika na Kikanda

9.            Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wastani wa kasi ya ukuaji wa uchumi iliongezeka hadi asilimia 3.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 2.9 mwaka 2017. Ukuaji huu ulitokana na ongezeko la mahitaji ya bidhaa pamoja na marekebisho ya sera za kiuchumi. Mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 8.5 kutoka wastani wa asilimia

11.0 mwaka 2017. Mwenendo huo wa mfumuko wa bei ulitokana na kuimarika kwa sera za fedha ikiwemo viwango imara vya kubadilisha fedha na kuimarika kwa sera za matumizi.

10.          Mheshimiwa Spika, mwenendo wa uchumi  wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaonesha kuwa uchumi wa Rwanda ulikua kwa asilimia 8.6 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 6.1 mwaka 2017. Uchumi wa Uganda ulikua kwa asilimia 6.1 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 5.9 mwaka 2017. Uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia 6.3 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2017.

11.          Mheshimiwa Spika, hadi Desemba 2018, mwenendo wa mfumuko wa bei katika nchi za Jumuiya ya Afrika

Mashariki uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulipungua hadi wastani wa asilimia 2.9 kutoka wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2017. Katika kipindi hicho, wastani wa mfumuko wa bei kwa Tanzania ulikuwa asilimia 3.5, Kenya asilimia 4.6, Rwanda asilimia 1.4, Uganda asilimia 2.6, na Burundi asilimia 2.3. Mwenendo huu ulitokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Uchumi wa Taifa Pato la Taifa

12.          Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, Serikali kupitia

Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilifanya maboresho ya takwimu za Pato la Taifa kwa kutumia mwaka 2015 kama mwaka wa kizio kutoka mwaka wa kizio wa 2007. Kufuatia maboresho hayo, mabadiliko kadhaa yalijitokeza ikiwa ni pamoja na mfumo na ukubwa wa Pato la Taifa; viwango vya ukuaji  wa Pato la Taifa kisekta; mchango wa sekta mbalimbali katika Pato la Taifa; na uwiano wa viashiria mbalimbali kwa Pato la Taifa.

13.          Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu mpya za mwaka wa kizio wa 2015, Pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2017. Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, reli, na viwanja vya ndege; kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; na hali nzuri ya hewa iliyopelekea uzalishaji mzuri wa chakula na mazao mengine ya kilimo. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi kubwa ni pamoja na: sanaa na burudani (asilimia 13.7); ujenzi (asilimia 12.9); uchukuzi na uhifadhi mizigo (asilimia 11.8); Shughuli za kitaaluma, Sayansi na Ufundi (asilimia 9.9); na habari na mawasiliano (asilimia 9.1). Sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 5.3. Sekta zilizotoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa ni kilimo (asilimia 28.2), ujenzi (asilimia 13.0) na biashara na matengenezo (asilimia 9.1).

 14.          Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa kwa bei za mwaka husika lilikuwa Shilingi trilioni 129.4 mwaka 2018 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 118.7 mwaka 2017. Aidha, mwaka 2018, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu 52,619,314 ambapo Pato la wastani la kila mtu lilifikia shilingi 2,458,496 kutoka shilingi 2,327,395 mwaka 2017 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 5.6. Kiasi hicho cha Pato la wastani kwa kila mtu kwa mwaka 2018 ni sawa na dola za Marekani 1,090 ikilinganishwa na dola za Marekani 1,044 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 4.4.

Mwenendo wa Bei

15.          Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, mfumuko wa bei uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja na kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka wastani wa asilimia 5.3 mwaka 2017 hadi wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Hadi mwezi Aprili 2019, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Kiwango hicho cha chini cha mfumuko wa bei kilitokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

(i)            Kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani. Uzalishaji wa chakula nchini uliofikia tani milioni 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.3 kwa kipindi hicho, hivyo kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124; na

(ii)           Utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti.

 Utekelezaji wa Sera za Fedha 2018/19

 16.          Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iliendelea kutekeleza sera ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kuna utoshelevu wa ukwasi kwenye uchumi kuendana na malengo mapana ya uchumi ya kuwa na utulivu kiuchumi na ukuaji endelevu na jumuishi.

17.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 malengo ya sera ya fedha yalikuwa ni:

(i)            Ukuaji wa wastani wa fedha taslim usiozidi asilimia 11.5;

(ii)           Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) usiozidi asilimia 12.2;

(iii)          Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi usiozidi asilimia 10.2; na

(iv)         Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

18.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi kinachoishia Aprili 2019, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ili kuziwezesha benki na taasisi za fedha kuongeza utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hatua hizo ni pamoja na: kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki; kununua fedha za kigeni kutoka katika benki za biashara na taasisi za Serikali; kushusha kiwango cha riba ya mikopo kwa benki kulikofanyika mwezi Agosti 2018 kutoka asilimia 9.0 hadi asilimia 7.0; na kulipa malimbikizo ya madai mbalimbali ya wakandarasi, watoa huduma na watumishi ambapo takribani Shilingi bilioni

598.4 za madai yaliyohakikiwa zililipwa kati ya Julai 2018 na Mei 2019.

19.          Mheshimiwa Spika, hatua hizi zilisaidia kuongeza ukwasi kwenye benki na taasisi za fedha pamoja na kushusha riba katika masoko ya fedha ambapo katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019, riba ya siku moja katika soko la fedha baina ya benki za biashara (overnight interbank cash market rate) imeendelea kuwa tulivu katika wastani wa asilimia 3.18 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.67 katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18. Riba za dhamana za Serikali zilifikia wastani wa asilimia

8.07 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019 ikilinganishwa asilimia 7.75 katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18. Vile vile, riba za mikopo inayotolewa na benki za biashara zilishuka kidogo na kufikia wastani wa asilimia 17.15 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019 kutoka wastani wa asilimia 17.93 katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18.

20.          Mheshimiwa Spika, wastani wa riba za mikopo umeendelea kupungua kwa kasi ndogo kutokana na benki za biashara kuendelea kuweka tahadhari kubwa  kwa wateja wanaoshindwa kurejesha mikopo kwa wakati. Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinakuwa nafuu ili kuendana na hali halisi ya uchumi. Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa sekta ya benki na taasisi za fedha zinapata taarifa sahihi za wakopaji kwa kutumia

kanzidata ili kupunguza athari za mikopo chechefu pamoja na kuendelea na marekebisho ya sheria katika usimamizi wa sekta ya fedha nchini.

Ujazi wa Fedha na Karadha

21.          Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2019 ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 4.9 na kufikia shilingi bilioni 25,629.1 kutoka shilingi bilioni 24,433.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Ukuaji huu ulikuwa sawia na mahitaji ya uchumi kutokana na kuongezeka kwa kasi ya mzunguko wa fedha kufuatia ongezeko la matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo ambayo imechochea kupungua hitaji la kubeba sarafu.

Amana katika Benki za Biashara

22.          Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2019, amana katika benki za biashara ziliongezeka na kufikia shilingi bilioni 21,322.7 kutoka shilingi bilioni 20,298.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Hii ilitokana na jitihada za benki za biashara kuhamasisha wananchi kuweka fedha benki kwa kutumia vivutio mbalimbali vya akaunti, kuongeza matawi ya benki pamoja na matumizi ya wakala wa benki.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi

23.          Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2019 mikopo kwa

sekta binafsi iliongezeka kwa wastani wa asilimia 10.6 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 0.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulichangiwa na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuboresha mazingira ya biashara; usimamizi thabiti wa sera ya fedha; pamoja na kupungua kwa mikopo chechefu kwenye benki za biashara kulikotokana na matumizi ya kanzidata ya taarifa za wakopaji katika kuidhinisha mikopo. Mikopo hii imesaidia kuanzisha na kuimarisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara, ujenzi na kilimo.

24.          Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi/kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 28.8 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizokuwa na wastani wa asilimia 18.5 na shughuli za uzalishaji viwandani asilimia 11.3. Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha benki za biashara zina ukwasi wa kutosha na kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha masoko ya fedha na utendaji wa benki, kuboresha mazingira ya kufanya biashara na upatikanaji wa taarifa za wakopaji ili kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa mikopo.

Ukuzaji Rasilimali

25.          Mhemishiwa Spika, ukuzaji rasilimali kwa bei za miaka husika ulifikia shilingi bilioni 50,383.14 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 40,427.43 mwaka 2017. Uwiano wa ukuzaji rasilimali kwa Pato la Taifa kwa bei za miaka husika uliongezeka kufikia asilimia 39.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia

34.0 mwaka 2017. Ukuzaji rasilimali za kudumu kwa bei za miaka husika uliongezeka kwa asilimia 19.4 kutoka Shilingi bilioni 42,141.92 mwaka 2017 hadi shilingi bilioni 50,316.24 mwaka 2018. Aidha, thamani ya limbikizo la rasilimali kwa bei za miaka husika iliongezeka kwa Shilingi bilioni 66.9 mwaka 2018 ikilinganishwa na punguzo la Shilingi bilioni 1,714.49 mwaka 2017. Ukuzaji rasilimali katika sekta ya umma ulifikia Shilingi bilioni 15,265.61 mwaka 2018 kwa bei za miaka husika, sawa na ongezeko la asilimia 17.2 wakati ukuzaji rasilimali katika sekta binafsi uliongezeka kwa asilimia 20.4 kufikia Shilingi bilioni 35,050.63.

Sekta ya Nje

26.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka ulioishia Aprili 2019, urari wa jumla wa malipo ulikuwa na nakisi ya dola za Marekani milioni 1,089.2 ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 299.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Hali hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa nakisi kwenye akaunti ya

bidhaa, huduma, kipato cha msingi na cha pili (primary and secondary income account) ambapo nakisi iliongezeka kwa dola za Marekani milioni 423.1 na kufikia dola za Marekani milioni 2,132.6 mwezi Aprili 2019.

27.          Mheshimiwa Spika, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019 ilifikia dola za Marekani milioni 7,210.6 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 7,291.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18.

28.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje ya nchi zilifika dola za Marekani milioni 9,024.9 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,464.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2017/18, sawa na ongezeko la asilimia 6.6. Ongezeko hili, kwa kiasi kubwa, lilitokana na uagizwaji mkubwa wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya reli, viwanja vya ndege, bandari na barabara. Thamani ya mafuta yaliyoagizwa kutoka nje nayo iliongezeka hususan kutokana na kupanda kwa bei katika soko la dunia kutoka wastani wa dola za Marekani 52.81 kwa pipa mwaka 2017 hadi wastani wa dola za Marekani

68.33 kwa pipa mwaka 2018. Aidha, uagizaji wa bidhaa za chakula ulipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka  kwa  mavuno  kipindi  cha  msimu  wa mwaka

2018/19. Kwa upande wa huduma, thamani ya malipo kwenda nje ya nchi ilipungua na kufikia dola za Marekani milioni 1,709.3 mwezi Aprili 2019 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 1,848.5 Aprili 2018.

Akiba ya Fedha za Kigeni

29.          Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kuendelea kukidhi mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi, na pia kuongeza imani kwa wawekezaji katika uchumi. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 4,395.2 Aprili 2019, kiasi ambacho kinatosha uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi

4.3. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kuwa na akiba ya kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4.0.

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi

30.          Mheshimiwa Spika, thamani ya Shilingi imeendelea kuwa imara ambapo katika kipindi kinachoishia Aprili 2019, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Shilingi 2,300.9 ikilinganishwa na shilingi 2,270.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2018. Utulivu katika mwenendo wa thamani ya Shilingi umetokana na utekelezaji wa sera  ya fedha, usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi ya Serikali, matumizi ya gesi asilia badala ya mafuta katika

kuzalisha umeme, na baadhi ya viwanda kuzalisha bidhaa ambazo awali zilikuwa zikiagizwa kwa wingi kutoka nje ikiwemo vigae na marumaru.

31.          Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa Fedha za Kigeni, mwezi Novemba 2018 Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa ghafla katika maduka ya kubadilisha fedha jijini Arusha na kuyafunga maduka yasiyozingatia taratibu na sheria za biashara hiyo. Vile vile, mwezi Februari 2019 Benki Kuu ilifanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam na kubaini kwamba maduka mengi yanaendesha biashara hiyo pasipo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni. Kufuatia ukaguzi huo, Benki Kuu ilianza utaratibu wa kufuta leseni za maduka yote yaliyokutwa yanaendesha biashara hiyo bila kuzingatia masharti ya leseni ambapo zoezi hili linaendelea. Hata hivyo, huduma ya ubadilishaji wa fedha za kigeni imeendelea kupatikana kwa ufanisi na baadhi ya benki za biashara zimeingia katika biashara hii na zinatoa huduma vizuri.

Deni la Serikali

32.          Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2019, deni la  Serikali lilifikia Shilingi bilioni 51,036.42 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 49,866.17 Aprili 2018, sawa na ongezeko la

asilimia 2.4. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilifikia shilingi bilioni 13,251.66 na deni la nje Shilingi bilioni 37,784.76. Ongezeko la deni lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya standard gauge, madaraja ya juu na miradi ya barabara. Aidha, kwa mujibu wa tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanywa Desemba 2018, nchi ina uwezo wa kukopa ndani na nje, na kulipa mikopo hiyo bila kuwa na athari hasi kwenye ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya fedha. Aidha, katika kuhakikisha kuwa deni linaendelea kuwa himilivu, Serikali itaendelea kukopa kutoka kwenye vyanzo nafuu na kuhakikisha mikopo inaelekezwa kwenye miradi ambayo itachochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2018/19

33.          Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 – 2018/19), yamepatikana mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo yakiwemo:

(i)            Ukuaji wa Uchumi: kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Taifa, ambapo kwa kipindi hicho cha miaka mitatu na nusu uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 6.9 na mfumuko wa bei kuendelea

kupungua na kuwa katika wastani wa kiwango cha tarakimu moja, chini ya asilimia 5.0.

(ii)           Reli: ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge unaendelea, ambapo kwa awamu ya kwanza ya Dar es Salaam – Morogoro (km 300) utekelezaji umefikifia asilimia 48.9 na Morogoro - Makutupora (km 422) asilimia 7.12. Vile vile, taratibu za ujenzi kwa sehemu za Makutupora - Tabora (km 294), Tabora - Isaka (km 133), Isaka - Mwanza (km 249), Isaka – Rusumo (km 371), Tabora - Kigoma (km 411), Keza - Ruvubu (km 36) na Kaliua – Mpanda - Karema (km 321) unaendelea. Mafanikio mengine ni kuendelea na ukarabati wa reli iliyopo katika sehemu ya Dar es Salaam hadi Isaka ambapo shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuboresha eneo la kupakia/kupakua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kukarabati vituo vya kuhudumia mizigo vya Ilala na Isaka, utekelezaji umefikia asilimia 13 na unatarajiwa kukamilika Juni 2020. Aidha, Serikali inaendelea na uboreshaji na ufufuaji wa reli ambapo Ufufuaji wa Njia ya Reli ya Tanga – Arusha (km 439) umefikia asilimia 80; vichwa 11 vya treni kwa ajili ya njia kuu vimenunuliwa na mabehewa 15 yamekarabatiwa; na ufungaji wa vipuri kwenye mitambo ya mgodi wa kokoto wa Tura umekamilika.

Kwa upande wa Ukarabati wa Reli na Uimarishaji wa TAZARA, ununuzi wa vipuri vya injini vinavyojulikana kwa jina la Traction Motor, na mitambo (Excavator, Dumper Track na Drill Rig) ya kusaidia uzalishaji wa kokoto na mataruma ya zege katika mgodi wa Kongolo unaendelea ambapo Drill Rig iliwasili mwezi Aprili 2019.

(iii)          Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Kununuliwa kwa ndege sita ambazo zimeshawasili nchini ambapo moja (1) ni aina ya Boeing 787 – 8 Dreamliner, tatu (3) ni Bombardier Dash 8 – Q400 na mbili (2) ni Airbus A220-300; kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja (1) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na moja (1) Bombardier Dash 8 – Q400 zinazotarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwaka 2019; kugharamia Mafunzo ya marubani (51), wahandisi (14) na wahudumu (66); na kuanza kwa ukarabati wa Karakana ya Matengenezo ya Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Kutokana na kuboreshwa kwa ATCL: idadi ya abiria imeongezeka kutoka 49,854 mwaka 2015/16 hadi 242,668 mwaka 2018/19; kuongezeka kwa idadi ya miruko (flights) kutoka 672 hadi 3,808 mwaka 2018/19; kuongezeka kwa idadi ya mikoa iliyofikiwa kwa huduma kutoka mikoa 3

hadi mikoa 11; kuongezeka kwa idadi ya vituo vya nje kutoka kimoja (Hahaya - Comoro) hadi vituo 5 (Hahaya, Bujumbura, Entebbe, Harare, na Lusaka); kuongezeka kwa idadi ya ajira kutoka 134 hadi 448; na kuongezeka kwa mapato ya Shirika kutoka Shilingi 11,756,709,000 hadi Shilingi 45,632,442,000. Vile vile, kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania kumechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2016 hadi watalii 1,505,702 mwaka 2018 ambao wameliingizia Taifa mapato ya dola za Marekani bilioni 2.4. Hivi karibuni ATCL inatarajia kuanza safari za moja kwa moja kwenda Mumbai (India), Guangzhou (China) na Johannesburg (Afrika Kusini).

(iv)         Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Mto Rufiji (Rufiji Hydro Power Project) – MW 2,115: Mkandarasi wa mradi wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto Rufiji ambaye ni Kampuni ya Ubia kati ya Arab Contractors na Elsewedy Electric S.A.E kutoka Misri amepatikana ambapo mkataba wa ujenzi umesainiwa na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi mwezi Februari 2019 na kwa sasa anaendelea na utekelezaji wa kazi za awali. Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ikijumuisha: njia ya kusafirisha umeme wa MW 8 yenye msongo wa kV 33 kutoka Msamvu, Morogoro hadi eneo la mradi yenye urefu wa kilomita 170; barabara za kiwango cha changarawe za Ubena – Zomozi na Kibiti – Mloka hadi eneo la mradi; mifumo ya maji; mawasiliano ya simu; na nyumba za kuishi Mkandarasi. Kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa njia ya pili ya umeme msongo wa kV 33 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Gongo la Mboto kupitia Kisarawe hadi eneo la mradi urefu wa kilomita 245 itakayosafirisha umeme wa MW 22. Aidha, ujenzi wa mradi huu utakapokamilika kutaifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika na gharama nafuu na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi;

(v)          Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania): kukamilika kwa tathmini ya fidia kwa maeneo ya kipaumbele (camps and coating yard) na eneo lote la mkuza. Kazi zinazoendelea ni pamoja na majadiliano ya mkataba kati ya kampuni ya mradi na Nchi Hodhi.

(vi)         Viwanja vya Ndege: kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) na miundombinu yake yenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Kilimanjaro, Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Kiwanja  cha Ndege cha Tabora (Awamu ya I na ya II) na Kiwanja cha Ndege cha Bukoba. Kazi zinazoendelea ni: ufungaji wa rada nne za kuongozea ndege za kiraia JNIA, KIA Mwanza na Songwe ambapo JNIA umefikia asilimia 95, KIA asilimia 90 na Mwanza asilimia 50; ukarabati wa Kiwanja cha Mwanza ambapo utelezaji umefikia asilimia 75, Kiwanja cha Ndege cha Songwe asilimia 70 na Kiwanja cha  Ndege cha Geita umefikia asilimia 72. Maboresho na ukarabati huu wa viwanja vya ndege unatarajiwa kuchochea ukuaji wa miji na shughuli za kiuchumi kwenye maeneo husika, kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta ndogo ya usafiri wa anga (aviation industry), kusaidia katika juhudi za kulifufua Shirika la Ndege (ATCL) kwa kufanya ndege za shirika ziweze kufika maeneo mengi (hivyo kuongeza route za shirika) na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini.

(vii)        Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: ujenzi wa gati Na.1 umekamilika na kuanza kutumika; ujenzi wa gati la Ro-Ro (gati la Magari) upo katika hatua ya ujenzi wa sakafu ngumu ya gati na ujenzi wa gati Na. 2 sambamba na kuongeza kina chake umeanza. Vile vile, upanuzi wa bandari za Tanga na Mtwara umefikia asilimia 86 na 50 kwa mtiririko huo. Kukamilika kwa upanuzi wa gati katika bandari ya Dar es Salaam kutaongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia magari kati ya 300,000 hadi 500,000 kwa mwaka; muda wa kupakua magari utapungua na hivyo kuongeza ufanisi wa bandari. Hatua hiyo itaongeza mapato ya Serikali na kuiwezesha bandari yetu kuhimili ushindani kutoka bandari za nchi jirani. Aidha, kwa upande wa Bandari za Maziwa Makuu: Ziwa Victoria: ujenzi wa gati za Nyamirembe Chato na Magarine unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 30 na 54 kwa mtiririko huo. Ziwa Tanganyika: ujenzi wa gati la Kalya/Sibwesa unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 93. Vile vile, Serikali inakamilisha majadiliano na JICA kwa ajili ya kugharamia upanuzi wa bandari ya Kigoma. Aidha, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati la Karema, umekamilika. Ziwa Nyasa: ujenzi wa gati la Ndumbi unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 37.

(viii)       Barabara na Madaraja: Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika kujenga na kukarabati barabara nchini ili kuhakikisha maeneo yote yanafikika kwa uhakika mwaka mzima. Juhudi hizi zitasaidia sana kuchochea kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji mali kwa kurahisisha usambazaji wa pembejeo na malighafi kwenda maeneo ya uzalishaji pamoja na usafirishaji wa mazao na bidhaa zingine katika maeneo mbalimbali ya masoko nchini. Barabara zilizokamilika ni pamoja na: Mfugale Flyover – TAZARA (mita 1,998); Same – Mkumbara (km 96); Barabara ya Nzega - Tabora sehemu ya Nzega – Puge (km 58.8); Tunduru - Nakapanya - Mangaka - Mtambaswala (km 202.5); Namtumbo - Kilimasera - Matemanga – Tunduru (km 193); Bariadi-Lamadi (km 71.8); Sumbawanga - Kanazi - Kizi – Kibaoni (km 151.6); Kyaka - Bugene (km 59.1); Usagara - Kisesa Bypass (km 17); Magole - Turiani (km 48.6); Dodoma - Mayamaya - Mela - Bonga (km 231.85); KIA - Mererani (km 26); Mwigumbi - Maswa (km 50.3); Uyovu - Bwanga (km 45); Kaliua - Kazilambwa (km 58.9); Tabora - Nyahua

- Chaya sehemu ya Tabora – Nyahua (km 85); Sitalike – Mpanda (km 36.90); Ndono - Urambo (km

52); na Tabora - Usesula (km 30). Vile vile, madaraja yaliyokamilika ni pamoja na Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero na barabara unganishi (m 9,523); Daraja la Kavuu – Katavi (mita 85.3); Daraja  la waenda kwa miguu la Furahisha – Mwanza (mita 45). Aidha, ujenzi wa barabara na madaraja unaendelea katika maeneo mbalimbali ikujumuisha: Ubungo interchange; barabara ya Kimara – Kibaha (km 19) kuwa njia nane; daraja jipya la Selander ikijumuisha barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2; Makutano - Natta - Mugumu/Liliondo - Mto wa Mbu sehemu ya Makutano – Sanzate (km 50); Kidatu

–             Ifakara – Lupilo - Mahenge /Malinyi - Londo - Lumecha/Songea, km 499; Kigoma – Kidahwe – Uvinza – Kaliua - Tabora (km 389.7); Sumbawanga - Matai – Kasanga Port (km 112); na Kidahwe – Kasulu

–             Kibondo – Nyakanazi (Nyakanazi – Kakonko (Kabingo) km 413.

(ix)         Ununuzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu: Ziwa Victoria: Kuendelea na Ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama. Aidha, makandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli za MV Umoja na MV Serengeti zilizopo katika ziwa Victoria

wamepatikana na uandaaji wa mikataba kwa ajili ya ukarabati wa meli tajwa umekamilika. Ziwa Tanganyika: mikataba ya ujenzi wa Meli Mpya moja yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 na ukarabati wa meli ya MV Liemba imekamilika. Ziwa Nyasa: ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika Ziwa Nyasa unaendelea ambapo utekelezaji umefikia asilimia 86. Aidha, ujenzi wa matishari mawili katika Ziwa Nyasa umekamilika.

(x)          Nishati: uzalishaji wa umeme umeongezeka kutoka GWh 7,092.13 mwaka 2015/16 hadi GWh 7,374 mwaka 2018/19 ambao umewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika; kuongezeka kwa kasi ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi kufikia Mei, 2019 jumla ya vijiji 7,127 vimeunganishiwa umeme ambapo jumla ya  taasisi za elimu 3,165, maeneo ya biashara 3,451, pampu za maji 210, taasisi za afya 1,211 na nyumba za ibada 984 zimeunganishiwa umeme; kufikishwa umeme katika vijiji vya Wilaya na Halmashauri 15  ambazo ni Mafia, Iringa Vijijini (Isimani), Pangani, Rufiji, Bahi, Siha, Moshi, Hai, Mwanga, Rombo, Madaba, Buhigwe, Makambako, Korogwe Mjini na Mafinga; ujenzi wa njia za kusambaza umeme za Msongo wa

kV 33 zenye urefu wa kilomita 18,227; ujenzi wa Vituo Vidogo vya kupoza na kusambaza umeme 4,100; na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme zenye urefu wa kilomita 30,797.

(xi)         Kilimo: kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo kiliongezeka kufikia asilimia 5.3 mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2016. Ukuaji huu umewezesha kuongezeka kwa usalama wa chakula, kupungua kwa mfumuko wa bei ya chakula kufikia asilimia 2.7 Aprili 2019 ikilinganishwa na asilimia 7.3 Aprili 2016 na kuongezeka kwa mapato ya mauzo ya bidhaa asilia nje ya nchi kutoka dola za Marekani milioni 793.4 mwaka 2015 hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,020.7 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 28.6. Vile vile, upatikanaji wa mbegu bora uliongezeka na kufikia tani 49,040.66 mwaka 2018/19 kutoka tani 36,482 mwaka 2015/16, na tani 492,394 za mbolea zilinunuliwa na kusambazwa katika mwaka 2018/19 ikilinganishwa na tani 302,450 zilizonunuliwa katika mwaka 2015/16. Aidha, katika kuimarisha Ushirika na Masoko ya Mazao, Vyama vya Ushirika viliongezeka kutoka 7,888 mwaka 2015 hadi 11,331 mwaka 2018. Vile vile, Serikali imeendelea na ujenzi wa vihenge na maghala vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 250,000

na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 unaendelea katika mikoa ya Ruvuma (Songea), Njombe (Makambako), Songwe (Mbozi), Rukwa (Sumbawanga), Katavi (Mpanda), Shinyanga, Manyara (Babati) na Dodoma. Utoshelevu wa Chakula kwa mwaka 2018/19 umefikia asilimia 124. Aidha, Serikali imeanza utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) na mkazo umewekwa katika kuendeleza mazao ya kimkakati yakiwemo Kahawa, Pamba, Chai, Korosho, Tumbaku, Alizeti, Michikichi, Mpunga na Mahindi.

Vile vile, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo. Tangu kuanzishwa kwa Mfuko huu mwaka 1994, jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi 82,103,746,770 imetolewa na katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo 33 yenye thamani ya Shilingi 1,495,362,060 ikiwemo 22 ya mitambo ya mashambani, sita (6) ya pembejeo za kilimo na mitano (5) ya umwagiliaji imetolewa. Aidha, utoaji wa mikopo hii unaenda sanjari na ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo ya nyuma ambapo katika mwaka 2018/19, shilingi 1,842,698,117.73

zimerejeshwa. Juhudi hizi zinalenga kuwawezesha wakulima kuongeza matumizi ya zana bora na za kisasa katika kilimo ili zisaidie kuongeza tija katika uzalishaji hasa ikizingatiwa kilimo chetu bado kinakabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo kutokana na matumizi ya zana duni.

(xii)        Huduma za Afya: Kununuliwa kwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kupitia Bohari ya Dawa na kusambazwa katika vituo vya umma vya kutolea huduma nchini ambapo upatikanaji wa dawa muhimu (Tracer Medicine) katika vituo vya kutolea huduma za afya umefikia asilimia 94.4 na kusambazwa lita 239,020 za viuadudu (biolarvicides) vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika maeneo ya mazalia ulifanyika katika Halmashauri zote nchini; kuongeza utoaji wa chanjo kufikia asilimia 98; kununuliwa mashine za X-ray 36 (28 za kidigitali na 8 za huduma ya kinywa); kuendelea na ujenzi wa hospitali za wilaya (67) Vituo  vya kutolea huduma za Afya (352) na nyumba za watumishi wa afya 318; kuajiriwa kwa watumishi wa sekta ya afya 7,680; bajeti ya ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 260 mwaka 2018/19; kuanza kutoa huduma ya kupandikiza figo

kwa wagonjwa 45 (wagonjwa 38 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na wagonjwa 7 katika Hospitali ya Benjamini Mkapa – Dodoma) na hivyo kupunguza gharama kwa wastani kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 20 kwa mgonjwa mmoja endapo angepelekwa nje ya nchi; Vile vile, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi kufuatia kuimarika kwa huduma katika hospitali za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi – Mloganzila. Kuimarika kwa huduma za kibingwa nchini kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu kwa wananchi ambao awali walikuwa wakipewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

(xiii)       Huduma za Maji: kukamilika kwa miradi 1,659 ya maji hivyo kuongeza vituo vya kuchotea maji kufikia 131,370 vyenye uwezo wa kuhudumia wananchi 25,359,290; upatikanaji wa huduma za maji jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa

mingine asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8; kuendelea kujenga  na kukarabati ofisi za maji za mabonde na maabara za maji katika mabonde mbalimbali ambapo hatua zilizofikiwa ni: Ruvuma na Pwani ya Kusini (asilimia 90), Ziwa Nyasa (asilimia 50), Rufiji (asilimia 65 Mkoji na Kimani), Ziwa Rukwa (asilimia 65) na Bonde la Kanda ya Kati (asilimia 95); kuendelea na ujenzi, ukarabati, na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya Kitaifa; mradi wa huduma za maji katika miji mikuu ya mikoa mipya unaendelea kutekelezwa ambapo kwa mkoa wa Geita umekamilika, Njombe umefikia asilimia 95 na Songwe asilimia 90; kuendelea na ulazaji wa bomba la kusambazia maji kwenye mradi wa maji wa Ziwa Victoria - Kahama Shinyanga katika miji ya Kagongwa na Isaka  ambapo utekelezaji umefikia asilimia 87 na ujenzi wa miundombinu ya maji katika miji ya Tabora, Igunga, Uyui na Nzega pamoja na vijiji 89 vilivyo pembezoni mwa bomba kuu umefikia asilimia 68.5. Vile vile, mradi wa maji Same – Mwanga – Korogwe umeendelea kutekelezwa ambapo miundombinu ya msingi ikiwemo bomba kuu la kusafirisha maji, kitekeo cha maji, mtambo wa kusafisha maji na matanki ya kuhifadhi maji, maabara na eneo la

kuhifadhia dawa za kutibu maji vimekamilika. Kukamilika kwa miradi hii ya maji kutawanufaisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali na kuwakinga na maradhi hususan katika maeneo ya vijijini.

(xiv)       Viwanda: Serikali iliendelea kusimamia utekelezaji wa azma yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo viwanda vipya zaidi ya 3,530 vilijengwa katika mikoa mbalimbali ikijumuisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za ujenzi (saruji, marumaru, nondo) na kilimo, hususan, kusindika matunda, mafuta na ngozi. Ujenzi wa viwanda vipya umechangia kupatikana kwa ajira mpya takribani 482,601 nchi zima. Aidha, ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF) imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.264 na kuzalisha ajira mpya takriban 186,138 kutokana na mikopo 91,584. Serikali imeendelea kuunganisha matrekta katika Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta – TAMCO, Kibaha ambapo Jumla ya matrekta 822 aina ya URSUS yameingizwa nchini kutoka Poland yakiwa katika vipande (semi knocked down) ambapo matrekta 571 yameunganishwa na matrekta 399 yameuzwa. Mafanikio haya yamewezesha jumla ya ekari 85,464 kulimwa kwa kutumia matrekta hayo hadi Aprili 2019. Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini – CAMARTEC: kutengeneza zana zikijumuisha mashine 64 za kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha mbogamboga na kukata majani pamoja na ujenzi wa mitambo 55 ya biogas; SIDO: kuendelea na ujenzi wa majengo ya viwanda 11 katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Manyara, Mtwara na Simiyu na ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya ya Geita na Katavi. Aidha, Serikali inaendelea na uendelezaji wa kanda Maalum za Kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini ambapo Kanda Maalum za Kiuchumi za Kigoma na Mtwara uwekezaji umeanza.

(xv)        Kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma: Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka katika jiji la Dar es Salaam kuja katika jiji la Dodoma ambapo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Watumishi wa Umma 8,883 kutoka Wizara na Taasisi wamehamia  Dodoma. Aidha, Ujenzi wa Ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba umekamilika na kuzinduliwa rasmi ambapo Wizara zote zimehamia na kuanza kutoa huduma katika eneo la mji wa Serikali.

(xvi)       Madini: kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa jengo la wafanyabiashara wa madini (Brokers house) na kuendelea na ujenzi wa kituo cha pamoja (one stop centre) eneo la Mirerani ambapo uwekezaji huo utaimarisha upatikanaji wa takwimu na kudhibiti utoroshaji wa madini ya tanzanite; ujenzi wa jengo la taaluma la Chuo cha Madini (MRI) Dodoma; uanzishwaji wa masoko ya madini mikoani katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wa madini wanapata masoko rasmi na Serikali kupata mapato stahiki; ufungwaji wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwenye vituo vya mfano vya Lwamgasha na Katente (Geita) na Itumbi (Mbeya) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini, afya, usalama migodini na utunzaji wa mazingira. Vituo hivi vitawezesha wachimbaji wadogo kujifunza kwa vitendo ili waweze kuwekeza na kufunga mitambo ambayo haitumii kemikali za zebaki (mercury); ujenzi na ukarabati wa ofisi za madini Moshi na Nachingwea; ujenzi wa vituo Saba (7) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Bukoba, Musoma, Handeni, Mpanda, Chunya na Songea

vitakavyotumika kutoa mafunzo na maarifa kuhusu ujasiriamali, utafutaji na uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo ambapo kati ya hivyo, vituo vya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni vimekamilika; na mapitio ya Sheria za Madini ili kuiwezesha Serikali kunufaika zaidi na rasilimali za madini. Aidha, Serikali ilikamilisha ujenzi wa ukuta wenye mzingo wa km 24.5 kuzunguka migodi ya Tanzanite Mirerani na uwekaji wa mfumo wa ulinzi wa kidigitali ambao umewezesha kupunguza utoroshwaji wa madini. Juhudi hizi na nyinginezo ziliwezesha kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli yanayotokana na madini kutoka Shilingi bilioni 194.4 mwaka 2016/17 hadi Shilingi bilioni

244.3 kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.

(xvii)      Elimu: Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa  na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mwenyekiti wa CCM, ilianzisha na imeendelea kutekeleza utaratibu wa kutoa elimumsingi bila ada kwa kutoa Shilingi bilioni 24.4 kila mwezi. Juhudi hizi zimechangia ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi wanafunzi 1,670,919 mwaka 2019, na kidato cha kwanza kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi

710,436 mwaka 2019. Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na: ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa shule za msingi 219 na sekondari

285 katika mikoa yote; ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya vyuo 7 vya ualimu; ununuzi wa kemikali na vifaa vya maabara kwa shule za sekondari 1,696; kuimarisha ubora wa elimu ya msingi na sekondari kwa kuboresha na kuchapa vitabu vya shule ya msingi na sekondari; kuimarisha ufundishaji kwa vitendo kwa kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Dodoma; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya  kufundishia na kujifunzia ikijumuisha madarasa 938, matundu ya vyoo 2,141, mabweni 210, mabwalo 76; ukarabati wa shule kongwe 17; kukamilisha maboma ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu 39; ukarabati wa vyuo 20 kati ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kukamilika kwa ukarabati wa mabweni sita (6) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu vya Sokoine na  Dar es Salaam; na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya  juu  122,734;  uimarishaji  wa  miundombinu  ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya ufundi stadi na kukuza ujuzi kwa vijana; na kukamilika kwa ujenzi wa shule ya sekondari maalum ya Patandi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 640. Mafanikio haya yamechangia kupunguza gharama za elimu msingi nchini na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wetu pamoja kuchochea mwamko wa elimu kwa wananchi.

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2019/20

Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa Mwaka 2019/20

34.          Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 umezingatia shabaha kuu za uchumi jumla zifuatazo:

(a)          Kukua kwa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2019 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2018;

(b)          Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi asilimia 4.5;

(c)           Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka 2018/19;

(d)          Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20; na

(e)          Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa asilimia 2.3 mwaka 2019/20.

Miradi ya Kipaumbele 2019/20

35.          Mheshimiwa Spika, miradi na shughuli za kipaumbele kwa  waka 2019/20 ni mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Miradi itaelekezwa katika maeneo ya kipaumbele ni kama ifuatavyo:

(a)          Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: Eneo hili litatilia mkazo ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini. Miradi mahsusi katika eneo hili itajumuisha:

(i)            Uendelezaji wa Viwanda: kuendeleza kongane za viwanda – TAMCO (Kibaha); Kongane ya viwanda vya ngozi (Dodoma); maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bunda, Dodoma na Benjamin William Mkapa; na kuendeleza vituo vya utafiti wa teknolojia na bidhaa za viwandani vya CAMARTEC, TIRDO, TEMDO na SIDO;

(ii)           Kilimo: kuongeza tija katika uzalishaji kwa

kuwezesha upatikanaji wa mbegu na pembejeo, huduma za ugani, maghala na masoko kwa mazao ya kimkakati ya kahawa, pamba, chai, mpunga, tumbaku na miwa; Serikali itaendeleza juhudi katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji; na kuimarisha utafiti wa mbegu bora na magonjwa ya mazao;

(iii)          Mifugo: kuimarisha mashamba ya kuzalisha mitamba na vituo vya uhamilishaji mifugo na kuhamasisha matumizi ya teknolojia sahihi ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa mitamba na madume kwa ajili ya maziwa na nyama, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa mlipuko kwa mifugo ili kuongeza uzalishaji na kukidhi ubora wa malighafi zitokanazo na mifugo kwa viwanda vinavyoendelea kujengwa nchini, kupima na kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo ili kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine.

(iv)         Uvuvi: kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli kubwa za uvuvi; kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania - TAFICO ili kuimarisha uwekezaji katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu;

kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi katika Ukanda wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Ukanda wa Pwani ili kuongeza udhibiti na kukomesha biashara haramu ya mazao ya uvuvi; na

(v)          Madini: kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; uendelezaji wa masoko ya madini; kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kuyeyusha madini (smelter) na vituo vya umahiri; kuwezesha shughuli za utafiti wa madini ili kuongeza taarifa za kijiolojia na kuvutia uwekezaji; kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu za rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia na; usimamizi wa masuala ya mazingira, afya na usalama migodini.

(b)          Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa katika mwaka 2019/20 itajielekeza katika maeneo yafuatayo:

(i)            Elimu: kuendelea kusomesha kwa wingi wataalam kwenye ujuzi na fani adimu kama vile udaktari, mafuta na gesi; kuendelea kugharamia utoaji wa elimu msingi bila ada; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika shule na vyuo vya ualimu; kuimarisha vyuo vya ufundi stadi kwa kukarabati, kujenga na kuweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia; kuboresha na kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule 500 za sekondari ili kuziwezesha kuwa vituo vya mafunzo kazini kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha; kujenga ofisi 55 za wathibiti ubora wa shule; kuongeza utoaji wa mikopo ya elimu ya juu na kusimamia marejesho yake; na kuendeleza shughuli za utafiti kwa maendeleo. Utekelezaji wa shughuli hizi utaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na hivyo kuongeza ufaulu wa watoto wetu.

(ii)           Afya: kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika Hospitali za Rufaa za mikoa, kanda na Taifa; kuimarisha usambazaji wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya; kuimarisha hali ya lishe na usafi wa mazingira; kuimarisha huduma katika taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI); kuendeleza ujenzi wa

Hospitali za Wilaya na vituo vya afya; ujenzi na ukarabati wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii; kuimarisha huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto walio katika mazingira hatarishi; na kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Utekelezaji wa shughuli hizi utaboresha upatikanaji wa huduma za afya katika ngazi mbalimbali nchini na hivyo kuimarisha afya za wananchi.

(iii)          Maji: kuimarisha upatikanaji wa maji mijini na vijijini; kuendelea na ujenzi wa miradi ya maji ikiwemo Makonde (Mtwara), Wanging’ombe (Njombe), Chalinze (Pwani), Mugango/Kiabakari – Butiama (Mara); maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Tabora, Nzega, Igunga, Sikonge na vijiji 89 vilivyo pembezoni mwa bomba kuu na kuanza ujenzi kupeleka maji katika miji ya Busega, Bariadi, Lagangabilili na Mwanhuzi; na kuendeleza rasilimali za maji nchini na maabara za maji.

(c)           Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya

kurahisisha ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi. Miradi katika eneo hili itajumuisha: kuendelea na Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Mto Rufiji – MW 2,115; na Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania. Miradi mingine ni pamoja na: Kuboresha miundombinu ya reli za TAZARA, Tanga – Arusha, usafiri wa reli Dar es Salaam pamoja na kuboresha injini na mabehewa ya treni; kuendelea na ujenzi wa barabara zikijumuisha barabara za Kigoma - Kidahwe - Uvinza – Kaliua - Tabora (km 389.7), Mtwara – Mingoyo – Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 1,470.9), Barabara ya Kidahwe - Kasulu – Kibondo - Nyakanazi (km 413),  Usagara - Geita -  Buzirayombo

– Kyamyorwa (km 230); madaraja ya Sibiti (Singida), New Wami (Pwani); Daraja la Kigongo/Busisi (Mwanza), Daraja la Mtera (Dodoma), Simiyu (Mwanza), Selander (Dar es Salaam); ujenzi na ukarabati wa vivuko; usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA; miradi mikubwa ya njia za kusambaza umeme wa msongo mkubwa ikijumuisha njia ya umeme wa msongo wa kV 400 ya Rufiji – Chalinze – Dodoma (km 512); uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara; na miundombinu  ya  viwanja  vya  Ndege;  kuimarisha

upatikanaji wa ardhi na huduma za fedha kwa ajili ya mitaji ya uwekezaji; na kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji ikijumuisha kuhuisha  mfumo, viwango na idadi ya kodi, ushuru na tozo; na mifumo ya kitaasisi, kisera na kisheria ili kuvutia uwekezaji; na

(d)          Kuimarisha Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango: Miradi inayotekelezwa katika eneo hili inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango, kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji. Miradi hii itajumuisha ile ya Utawala Bora hususan utoaji Haki na Huduma za Kisheria, Kuimarisha Mifuko ya Mahakama na Bunge, kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuvipatia vitendea kazi na mafunzo pamoja na kuimarisha Usajili wa Vizazi na Vifo.

36.          Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Miradi ya Kipaumbele yapo katika Sura ya Nne ya Kitabu cha Mpango.

Vihatarishi Vya Utekelezaji wa Mpango 2019/20

37.          Mheshimiwa Spika, Vipo vihatarishi mbalimbali ambavyo endapo vitajitokeza vitaathiri utekelezaji wa Mpango. Vihatarishi hivyo vinajumuisha vihatarishi vya ndani na nje. Vihatarishi vya ndani ni pamoja na upungufu wa rasilimali fedha, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, umiliki wa ardhi na utatuzi wa migogoro, uharibifu wa mazingira na usalama mtandaoni. Vihatarishi vya nje ni pamoja na mtikisiko wa kiuchumi kikanda na kimataifa, matukio asilia, migogoro ya ndani na ya kimataifa na mabadiliko ya tabia nchi.

38.          Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vihatarishi vya utekelezaji wa Mpango, Serikali ya awamu ya tano itachukua hatua mbalimbali ikijumuisha: kuharakisha urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili iweze kuingizwa kwenye wigo wa kodi; kuimarisha nidhamu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo; kuendelea kuboresha mazingira wezeshi ya biashara ili kupunguza gharama za uwekezaji; kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa kuandaa na kuimarisha Mipango Miji ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii; na kuendelea kuimarisha mifumo ya kutabiri majanga na kuchukua tahadhari pamoja na kutekeleza miradi ya kuhimili athari za matukio asilia.

Ugharamiaji wa Mpango 2019/20

39.          Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga Shilingi bilioni 12,248.6, kwa ajili ya kugharamaia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20, ambapo shilingi bilioni 9,737.7 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 2,510.9 ni fedha za nje. Fedha hii ya maendeleo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2019/20, kiwango kinachoshabihiana na lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano la kutenga kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Serikali inatarajia kugharamia Mpango kutokana na vyanzo mbalimbali vikijumuisha mapato ya kodi, mikopo na misaada ya Washirika wa Maendeleo, Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Uwekezaji wa Moja kwa Moja kutoka Nje na Mifuko ya Kimataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi.

Uwekezaji wa Moja kwa Moja kutoka Nje

40.          Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji wa kimataifa hususan uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDIs) katika maeneo ya kipaumbele ya Mpango ikijumuisha viwanda, kilimo, maliasili, gesi, mafuta, madini, mawasiliano, ujenzi na utalii. Maboresho hayo yatajumuisha ujenzi wa miundombinu ya msingi, utengaji wa maeneo maalum ya uwekezaji na kuweka miundombinu wezeshi, kuhuisha sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwekezaji pamoja na kuhamasisha sekta binafsi ya ndani ya nchi kuwekeza kwa ubia na sekta binafsi ya nje.

Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi

41.          Mheshimiwa Spika, Serikali itatoa elimu kuhusu uwekezaji wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ikijumuisha hatua za uibuaji, maandalizi na utekelezaji wa miradi ya ubia. Vile vile, Serikali itaendelea kutafuta wabia wa kimkakati katika miradi ya kipaumbele kwa utaratibu wa PPP.

Mifuko ya Kimataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi

42.          Mheshimiwa Spika, Vile vile, Serikali itaendelea kutumia mifuko mbalimbali ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi katika ufadhili wa miradi ya maendeleo hususan ile ya mazingira. Hatua mbalimbali zitakazochukuliwa zitahusisha majadiliano na Washirika wa Maendeleo na wadau mbalimbali ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kutoka mifuko hiyo kama vile Least Developed Countries Fund (LDCF); Global Environmental Facility (GEF); Adaptation Fund (AF); United National Environmental Programme (UNEP) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji

43.          Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha kuwa ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Mpango 2019/20 unazingatia Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuzingatia viashiria vya utekelezaji vilivyoainishwa katika maeneo ya kipaumbele ya Mpango. Aidha, ufuatiliaji na tathmini utazingatia taarifa ya tathmini ya muda wa kati wa utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano hususan hatua halisi ya utekelezaji, changamoto na mapendekezo ya hatua za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

44.          Mheshimiwa Spika, katika kila robo ya mwaka 2019/20 Wizara ya Fedha na Mipango itafuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo, kimkakati na inayotekelezwa na sekta binafsi ili kujua mafanikio na upungufu utakaojitokeza wa utekelezaji wa miradi katika maeneo ya kipaumbele ya Mpango. Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, SURA 439. Taarifa za utekelezaji zitasaidia Serikali katika kufanya maamuzi na kuhamasisha jamii kujituma zaidi katika kufikia malengo ya Mpango.

MAJUMUISHO NA HITIMISHO MAJUMUISHO

45.          Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kujenga uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Pamoja na jitihada nyingine katika kufanikisha lengo hili, Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu wezeshi ya undelezaji wa viwanda na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vitakavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan mazao ya kilimo, madini na gesi asilia.

46.          Mheshimiwa Spika, vile vile katika kufanikisha ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kukusanya mapato kutoka vyanzo bunifu vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kuhakikisha mipango na bajeti inawekewa viashiria, vigezo na shabaha bayana ambavyo usimamizi wa utekelezaji utazingatia, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi hususan katika sekta ya viwanda na kutekeleza maoni na ushauri unaotolewa na Bunge juu ya utekelezaji wa mipango na bajeti.

HITIMISHO

47.          Mheshimiwa Spika, tunapokaribia kuhitimisha kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wenye dhima ya “Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu”, niwaombe Viongozi wa Serikali, Waheshimiwa Wabunge na wananchi kushirikiana wote kwa pamoja katika kuleta ufanisi wa utekelezaji wa Mpango.

48.          Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali  ninaomba niwashukuru wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi na wananchi kwa ujumla kwa michango yao katika kuleta mafanikio katika ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Mpango.

49.          Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mhe. Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara zinazojitegemea na Taasisi kwa ushirikiano wao katika kutayarisha taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20. Aidha, ninawashukuru pia watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto M. James kwa kusimamia vizuri kazi za kila siku za Wizara.

50.          Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na vitabu vya Taarifa ya Uchumi ya mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz.

51.          Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Waheshimiwa Wabunge wapokee, wajadili na kupitisha Taarifa ya Hali ya Uchumi Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20.

52.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

No comments :

Post a Comment