Tuesday, April 23, 2019

SUZA ni chombo chakutatua changamoto zilizomo katika jamii- Dkt Shein

Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kina dhima kubwa ya kutoa taaluma bora inayoambatana na kufanya tafiti kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizomo katika jamii. Dk. Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)  aliyasema hayo leo 
katika Mahafali ya 14  ya Chuo Kikuu hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo ndani ya Kampasi ya Chuo hicho kiliopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kufanya tafiti mbali mbali ni miongoni mwa majukumu ya msingi ya vyuo vikuu jambo ambalo hutoa mchango wa chuo kitaaluma na kupandisha hadhi ya ubora wa chuo chenyewe.
Alikihimiza Chuo Kikuu hicho kiendelee kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania (COSTECH), ambayo ina wajibu wa kuwawezesha watafiti mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar kufanya tafiti wanazozikusudia.
Dk. Shein aliongeza kuwa Chuo Kikuu hicho kina wajibu wa kutafuta fedha za kufanya tafiti kutoka vyanzo mbali mbali kwani utafiti ni miongoni mwa majukumu ya chuo hicho hasa ikizingatiwa kuwa hakuna maendeleo bila ya utafiti.
Alieleza kuwa utafiti ni ngazi muhimu kwa Wanachuo wa mafunzo ya Uzamili na Uzamivu ambao huwasaidia kuhitimu masomo yao, na kukihimiza chuo hicho kujiandaa kuchapisha majarida ya kitaaluma ambayo wahadhiri na wanachuo wa ngazi ya Uzamili na Uzamivu watapata fursa ya kutuma makala zao zinazotokana na tafiti walizofanya.
Aidha, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Chuo hicho kuwaweka sawa baadhi ya wahadhiri wachache ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo pamoja na wafanyakazi wote wanaojaribu kufanya kazi zao kinyume na utaratibu.
Alisema kuwa Wahadhiri, walimu na wafanyakazi wa namna hiyo hawatimizi wajibu wao vizuri na hawachagii maendeleo ya Chuo kwani wafanyakazi wa namna hiyo hawana uzalendo “Si wazalendo na hawastahiki wajigambe kuwa ni wahadhiri wa SUZA. SUZA ni chuo cha watu wenye kuyapenda maendeleo ya viongozi wa baadae”,alisisitiza Dk. Shein.
Alisisitiza kuwa ili mafanikio yapatikane ni vyema kukadumishwa umoja na mshikamano uliopo baina ya wahadhiri, wafanyakazi, wanafunzi na washirika wote wa chuo hicho huku akiwataka kujiepusha na mambo yanayoweza kuleta mifarakano.
Rais Dk. Shein alieleza  mategemeo yake kuwa uongozi wa Wizara ya Afya utaendelea na utaratibu wa kuwaajiri madaktari wazalendo kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi Serikalini kwa lengo la kuzimarisha huduma za afya ikiwemo kupunguza tatizo la uhaba wa madaktari katika hopsitali za hapa nchini.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Wizara hiyo ya Afya kwa kutekeleza agizo lake alilowataka wahakikishe kuwa Hospitali ya Mnazi Mmmoja inatumika kwa kufanya mafunzo ya mazoezi ya madaktari wanaohitimu yaani “Internship” kama ilivyoamuliwa tangu mwaka 1977.
Akitoa nasaha zake Dk. Shein alisisitiza haja ya kuitumia vyema rasilimali ya kuandaa wataalmu wa Shahada za Juu za Lugha ya Kiswahili kwa kuwashirikisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje kuweka mikakati maalum ya kuikuza lugha ya Kiswahili na kubainisha uwezo wa kuwafundisha watu wa mataifa mengine.
Rais Dk. Shein aliwataka wahitimu na wataalamu wa Kiswahili kufanya jitihada ili wajiandae kwa kuzitafuta fursa zilizopo za mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili badala ya kukaa na kusubiri Serikali kwuatafutia fursa hizo.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa  Chuo Kikuu hicho kwa mwaka huu wa masomo ambapo Chuo Kitazindua udahili wa programu mpya mbili katika ngazi ya Shahada ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Uuguzi (DSc. Nursing) na Shahada ya Sayansi za Kilimo.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake kwa kusikia taarifa za Makamu Mkuu wa Chuo hicho kuwa upo mpango wa kuyafanyia matengenezo makubwa majengo ya Chuo kwa asilimia 75 na kujenga majengo mapya 12 ambapo Serikali imejiandaa kutekeleza Mpango huo ili ufanikiwe.
Dk. Sheinj aliongeza kuwa uongozi wa Chuo ni vyema ukaongeza kasi katika kufuatilia utekelezaji wa Nyaraka za Maelewano (MoU) wanazoingia na Taasisi nyengine kwani chuo hicho kimekwua kikishirikiana na vyuo mbali mbali duniani na kutiliana saini za Maelelewano katika kushirikiana huko.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutimiza wajibu wake ili iweze kuyafanikisha malengo yaliyowekwa kwa kutumia fedha za Bajeti na mipango mengine ambayo imeungwa mkono na nchi marafiki na washirika wa maendeleo.
Aidha, Dk. Shein aliuhimiza uongozi na wanachuo wa Chuo Kikuu hicho kuendeleza masuala ya michezo pamoja na uendelezaji wa midahalo kwani masuala hayo ni muhimu katika vyuo kwa lengo la kuimarisha afya za wanachuo na kuwaongezea maarifa na masuala mbali mbali ya kitaaluma.
Pia, Dk. Shein aliwahimiza wahitimu wa Mahafali hiyo kuzichangamkia fursa zilizoandaliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi na Mipango mengine ili waweze kujiajiri wenyewe na kuwataka kuwa na ndoto kubwa zaidi ya kujiajiri kuliko kusubiri kuajiriwa na Serikalini.
Alieleza kuwa matajiri na watu maarufu zaidi duniani wengi wao ni watu waliojiajiri wenyewe kwa kujishughulisha na biashara, sanaa, michezo na shughuli mbali mbali za ujasiriamali ambapo na wao wakiamua wanaweza kuwa miongoni mwa watu hao.
Katika Mahafali ya mwaka huu ya Chuo Kikuu hicho zipo jumla ya fani za masomo 56 zenye wahitimu 1940 ambapo asilimia 58 ya wahitimu wote ni wanawake na asilimia 42 wanaume ambapo pia kwa mara nyengine tena mwanamke ametokea kuwa mwanafunzi bora.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments :

Post a Comment