Mfanyabiashara
maarufu Mohamed yusufali na mfanyakazi wake Arital Maliwala wamefikishwa
katika mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 601
likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya bilioni 14.
Washtakiwa hao
wamesomewa mashtaka yao na jopo la mawakili wa kutoka Takukuru
wakiongozwa na Hashimu Ngole, Pendo Makondo, Leornad Swai ambao walikuwa
wakisaidiana na wakili wa serikali Patrick Mwita mbele ya hakimu Mkazi
Mkuu Wilbard Mashauri.
Katika mashtaka hayo,
washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kughushi,
kuwasilisha taarifa za mwezi za mahesabu ya uongo kwa TRA, kukwepa kodi
na kuisababishia serikali hasara ya sh. 14,987,707,044.58
Katika shtaka la
kuisababishia serikali hasara, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la
kusabisha hasara ambayo imetokana na kukwepa kodi ya serikali kwa
kipindi cha mwaka 2008 hadi 2015 kupitia kampuni ya Pamplant ltd
iliyokuwa inamilikiwa na mshtakiwa Yusufali ambapo mshtakiwa Paliwala
alikuwa mfanyakazi wake.
Imeendelea kudaiwa
kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo wakiwa wanatumia stakabadhi za
kughushi pamoja na kutumia makampuni ya kughushi wakidai kuwa wamenunua
vitu kutoka katika makampuni mbali mbali wakati wakijua baadhi ya
kampuni hizo ni za kughushi huku zikiwa hazijasajiliwa brella.
Pia imedaiwa kampuni
hizo zina majina ya makampuni ambayo hayapo brella na yana namba za
usajili ambazo brella haijazifikia huku pia wakiwa wanaghushi stakabadhi
za malipo.
Hata hivyo washtakiwa
hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu
uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP.
Kwa mujibu wa upande
wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umeishakamilika na kesi hiyo
itakuja tena mahakamani hapo January 24 mwaka huu kwa ajili ya
washtakiwa kusomewa maelezo yao (commital).
No comments :
Post a Comment