Saturday, August 18, 2018

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Kampuni ya Merck waandaa mkutano wa kwanza wa kutathimini magonjwa ya moyo nchini

picha no. 1 (1)
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Delila Kimambo akielezea jinsi mashine ya kupima moyo  (Echocardiogram) inavyofanya kazi  ya kutambua matatizo yaliyopo  katika moyo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika  leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo  Jijini Dar es Salaam.
Picha no. 2 (2)
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani Prof.Matthew Sackett akielezea jinsi  mtambo wa Cathlab  unavyotumika kutibu na kupima magonjwa ya moyo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo uliofanyika  leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
Picha no. 3 (2)
Baadhi ya Madaktari wa Magonjwa ya Moyo  kutoka Hospitali mbalimbali za  mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mada ya jinsi ya kumtambua mgonjwa mwenye matatizo ya moyo kwa kupitia kipimo cha ECHO wakati wa Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  uliopo jijini Dar es Salaam.
Na Salome Majaliwa – JKCI
17/08/2018 Madaktari wa Hospitali za Rufaa nchini wameshauriwa  kuwatuma mapema wagonjwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pindi wanapowapima na kugundulika  kuwa na ugonjwa   huo ili waweze kupatiwa matibabu mapema.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo  kutoka JKCI Delila Kimambo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika   katika ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo.
Dkt. Delila alisema  wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Hospitali mbalimbali hapa nchini rufaa yao huwa ni Taasisi ya Moyo hivyo basi ni muhimu wagonjwa hao wakafika katika Hospitali hiyo kwa wakati.
“Wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao huwa imechoka, kama wagonjwa hawa wangefika  mapema kwetu wangepata matibabu madogo  kuliko kupatiwa matibabu makubwa ya upasuaji wa kifua au bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo”.
“Kutokana na wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitalini ama kutokupata matibabu ya moyo kwa wakati, tumeona tuwe na mafunzo haya hii itawasaidia  madaktari wengi kupata ujuzi zaidi  na kuweza kutambua wagonjwa kwa wakati”, alisema Dkt. Delila.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo Dkt. Delila alisema  lengo ni kuwapatia madaktari ujuzi hususani wa namna ya kupima moyo kwa kutumia mashine za ECHO na umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG).
Kwa upande wake Daktari kutoka hospitali ya Amana Natalius Kapilima alisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata ujuzi utakaowawezesha kuwatambua wagonjwa wa moyo kupitia vipimo vya ECHO na ECG.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka hospitali ya Aga Khan Prof. Mustafa Bapuma aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuona mbali na kuwezesha  kufanyika kwa mafunzo hayo kwa madaktari. Kupitia mafunzo hayo wataweza kutibu wagonjwa wa moyo kwa ustadi na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Kampuni ya Merck ambapo jumla ya washiriki 80 kutoka Hospitali mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam walishiriki.

No comments :

Post a Comment