Monday, July 16, 2018

Wahasibu TTCL wadaiwa kuiba vocha za mil.44/-

PichaFrancisca Emmanuel
WAHASIBU watatu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi, kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 57.7.

Washitakiwa hao ni Mercy Semwenda maarufu Mercy Lema (49) mkazi wa Mwananyamala; Flora Bwahawa (54), mkazi wa Mbagala na Hawa Tabuyanjaa (54) mkazi wa Mwenge.
Wanakabiliwa na mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwezile.
Wakili wa serikali mwandamizi, Patrick Mwita amedai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ya wizi na kuisababishia serikali hasara katika kesi namba 50/2018.
Mwita amedai katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi na Septemba 21, 2017 jijini Dar es Salaam, waliiba vocha za muda wa maongezi zenye thamani ya Sh milioni 44.
Pia amedai kuwa, washitakiwa hao waliiba fedha za mauzo ambazo ni Sh milioni 5.9, na fedha taslimu Sh milioni 8.5 ambavyo vyote kwa pamoja ni Sh milioni 57.7.
Wanadaiwa ndani ya jiji hilo walisababishia TTCL hasara ya Sh milioni 57.7.
Hakimu Rwezile amesema washitakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote, kwa kuwa mashitaka hayo ni ya uhujumu uchumi.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Wakili wa utetezi, Thimotheo Wandiba alidai kuwa wanafanya utaratibu wa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 24, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana.

No comments :

Post a Comment