Monday, June 18, 2018

Ujue mpango “wastaafu loan” unavyowanufaisha wastaafu wa ZSSF.

Sabra Machano, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa ZSSF 

Na Christian Gaya
Mpango wa kupatiwa mikopo wastaafu kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF) ulioanzishwa mwaka 2014 na ZSSF kwa kushirikiana na benki ya posta tanzania (tpb) umekuwa ukombozi mkubwa kwa wastaafu nchini kwa kukuza uchumi wao binafsi ...
na kuongeza pato la Taifa kwa ujumla.

Wastaafu wengi wamekuwa wakihangaika kujikimu wakitegemea malipo yao ya pensheni ndogo ambayo hutolewa kila mwezi. Fedha za malipo ya pensheni tu haziwezi kukidhi mahitaji yao ya lazima kimaisha kama kusomesha watoto, gharama za matibabu na kuanzisha miradi ya kujiendeleza. Matokeo yake wastaafu wengi wamekuwa wakiishi kwa kuunga unga tu bila ya kuwa na vyanzo vya fedha vyenye uhakika.
Mpango huu unaojulikana kama 'Wastaafu Loan' na unalenga kukidhi mahitaji halisi ya fedha kwa wastaafu kwa kuwapa mikopo ya matibabu, ada za shule, kuendesha biashara na miradi mbalimbali.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonesha kuwa wastaafu wanaingiza kiasi kikubwa cha fedha katika uchumi kutokana na mafao wanayolipwa, ambapo kama watawekewa mfumo mzuri wanaweza kujiinua kiuchumi
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa ZSSF, Sabra Issa Machano  anasema, wastaafu wanaweza kuchangia uchumi kama vile kuongeza uwezo wa kifedha kwa wajasiriamali mbalimbali nchini kwa kununua bidhaa zao na katika taasisi za kifedha, kuongeza ajira, kukuza kipato, na hivyo kupunguza umaskini na pia katika kudumisha utulivu nchini. 
Anasema, kabla ya mpango huu, wastaafu wa ZSSF walikuwa hawana fursa ya kupewa mikopo kutokana na ama taasisi za fedha kuwa na hofu ya usalama wa mikopo yenyewe, kwa imani kuwa wastaafu ni wazee, hawana umri mrefu wa kuendelea kuishi tena au wakati mwingine kwa wastaafu wenyewe kutokuwa na elimu ya kuendesha miradi inayoweza kuwapatia faida na kurejesha mikopo hiyo. 
“Na hivyo taasisi za hifadhi ya jamii, taasisi za fedha pamoja na wataalam wa uwekezaji wanatakiwa kubuni njia na mipango ya kuwasaidia wastaafu ambao wana kiasi kikubwa cha fedha kitakachoweza kuchangia maendeleo ya Tanzania,” Machano anakumbusha.
Hasan Khamis ambaye ni mkazi wa Jumbi ni mmojawapo wa wastaafu wanaonufaika na mpango huu wa “wastaafu loan” anatoa ushuhuda wa kuanzisha shughuli zake za kuendesha kilimo maeneo ya Jumbi Mkoa wa Kusini Unguja na mstaafu wa mwaka 2015.  
“Kwa sasa nina mpango wa kutaka kuongeza kukopa zaidi ili niweze kununua gari ndogo ya mizigo ili kustawisha biashara zangu zaidi, kwa kweli ZSSF ni ufunguo wa maisha”mzee Khamis anasema.
Tangu mpango huu uanzishwe mwaka 2014 yaani miaka mitatu iliyopita umeshawanufaisha zaidi ya wastaafu wapatao 500. 
“Lengo la kuanzisha mpango huo ni kuwajali wanachama wetu hata wakiwa katika ustaafu wao na hiyo inakwenda sambamba na kauli mbiu yetu ya ‘ZSSF’ ni ufunguo wa maisha,”Machano ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa ZSSF anasema. 
Mikopo hii inawasaidia wastaafu kujikwamua kiuchumi na kuweza kuishi maisha bora au pengine zaidi ya yale waliyoishi kabla ya kustaafu na miongoni mwa mahitaji makubwa ya fedha za wastaafu ni gharama za matibabu, ada ya shule, kuendesha biashara au miradi mbalimbali na wakati huo huo mstaafu anapata nafuu, kwani ataendelea kupata pensheni yake kama kawaida huku akiendelea kulipia deni la mkopo.
 “Tunauona mpango huo ni ukombozi mkubwa kwa wastaafu, kinachotakiwa ni kwa wastaafu kupewa mafunzo ili kuwawezesha na kuwashauri namna bora ya kuwekeza na miradi ipi ya kufanya ambayo haina hasara kubwa wala shinikizo,”anafafanua zaidi.
Anasema, mkopo huu unawasaidia wastaafu kwani hauna dhamana na kuongeza kuwa mkopaji anaweza kukopa kuanzia shilingi 500,000/= hadi milioni 20 kwa kiwango cha riba kilicho chini ya kile kinachotolewa katika soko na taasisi zingine za kifedha nchini, zinazolipwa kupitia pensheni yake ya mwezi ndani ya mwaka mmoja hadi mitatu. 
Na faida nyingine ya mstaafu loan, ni pale mstaafu anapokuwa na fursa ya kuongeza kukopa hata kama hajamaliza mkopo wake ili mradi anamwendelezo mzuri wa kulipa mkopo wake.  
Machano anasema mkopo huu ambao ni wa kwanza katika soko la mabenki nchini, umeshaanza kuwanufanyisha kwa kuwawezesha wastaafu kuanzisha na kuendeleza biashara zao na kutimiza malengo yao na kujiongezea kipato.
“Hili litamwondoa mstaafu kwenye uwezekano wa kuwa tegemezi kwa ndugu au watoto, pia kumwezesha kuchangia kwenye uchumi wa nchi yetu,” anasema. 
Kwa kumalizia Machano anasema mstaafu anayehitaji mkopo hahitaji kuwa na dhamana, kwani mkopo huo una bima na endapo mkopaji atafariki familia yake haitadaiwa.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea  www.hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu +255 655 13 13 41 info@hakipensheni.co.tz

No comments :

Post a Comment