Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Serikali imesema kuwa hakuna
akiba ya fedha iliyowekwa katika mfuko maalum kwa ajili ya kulipia Deni
la Taifa kwa sababu deni hilo linajumlisha Deni la Serikali na Deni la
Sekta Binafsi, lakini Serikali inalipa deni lake pekee bila kuhusisha
deni la Sekta Binafsi.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
alipokuwa Akijibu maswali ya Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah
Salim aliyetaka kujua Deni la Taifa limefikia kiasi gani na namna
mchanganuo wa fedha zilizowekwa
akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo
ulivyo.
“Fedha kwa ajili ya malipo ya
Deni la Serikali inatengwa kwa kuzingatia taratibu za kawaida za
kibajeti kupitia Fungu 22, katika Mwaka wa Fedha 2017/18, Serikali
ilitenga kiasi cha Sh. trilioni 1.262 kwa ajili ya malipo ya deni la
ndani na Sh. bilioni 685.06 kwa deni la nje”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema hadi kufikia Aprili 30,
mwaka huu Deni la Taifa limefikia Dola za Marekani milioni 26,161.02
sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 59.4
Akijibu swali la nyongeza la
Mbunge huyo aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha Deni la
Taifa linahakikiwa ili kujua kama Serikali inakopesheka au la, Dkt.
Kijaji alilihakikishia Bunge kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Deni la
Taifa litahakikiwa kama nchi nyingine zinavyofanya kwani mkataba wa
kuhakiki deni hilo upo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hatua
za mwisho.
Waziri huyo alisema kuwa Deni la
Taifa ni himilivu na Serikali imekuwa makini katika ulipaji kwa
kuhakikisha inalipa kila mwezi madeni katika Taasisi zote ilizokopa hali
inayoifanya nchi kuaminika na Taasisi mbalimbali za kitaifa na
kimataifa
Aidha, Mhe. Kijaji alifafanua
kuwa fedha zote zinazokopwa zinapelekwa katika shughuli za maendeleo ya
kiuchumi ili kuendelea kuinua uchumi wa nchi hususani katika kipindi
hiki cha uchumi wa viwanda.
No comments :
Post a Comment