Tuesday, April 17, 2018

MBUNGE COSATO CHUMI AKABIDHI MSAADA WA VITANDA KWA KITUO CHA AFYA


Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akiongea na baadhi ya wananchi waliokuwa wamehudhuria katika hafla ya kukabidhi vifaa na gari la kubebea wagonjwa kwa lengo la kuendelea kuboresha sekta ya afya katika jimbo hilo 
Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akikabidhi vitanda kwa ajili ya kituo hicho
Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akikabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa ajili ya kituo hicho 


NA FREDY MGUNDA, MUFINDI
 
MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi ametoa msaada wa
vitanda kumi kwa kituo cha afya cha Ihongole kilichokuwa kinakabiliwa na
upungufu wa vitanda katika wodi ya wazazi. 
 
Akizungumza wakati kukabidhi vitanda hivyo sambamba na
kukabidhi gari ndogo ya kubebea wagonjwa iliyotolewa na serikali, Chumi alisema
kuwa msaada huo wa vitanda utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto
katika kituo hicho cha afya ambacho kinachohudumia wakazi zaidi ya 20000 wa
jimbo la Mafinga mjini. 
 
Alisema kuwa ushirikiano katika kuondoa changamoto na
kuchukulia mapungufu ndio njia pekee ya kuendelea kuinyanyua Mafinga hasa
katika sekta ya afya ambayo imekuwa ikikabiliana na changomoto nyingi.
 
Chumi alisema kuwa msaada wa vitanda vimetolewa na mmoja
wa wahisani wanaolisaidia jimbo la Mafinga kuondokana na changamoto mbalimbali
katika sekta ya afya ambayo imekuwa na ikikabiliwa na mapungufu mbalimbali
ikiwemo ukosefu wa miundo mbinu bora.
  
Alisema changamoto za sekta ya afya katika jimbo hilo na
wilaya ya Mufindi kwa ujumla zitakashughulikiwa kupitia serikali na wadau wake
mbalimbali wanaotakiwa kujitokeza kuboresha huduma zake 
 
Akizungumzia Gari hiyo ambayo imetolewa na Serikali Chumi
alisema kuwa itatumika kubeba wagonjwa ambao watalazimika kukimbizwa kwenye
Hospitali ya Mafinga ambapo awali ilikuwa vigumu kwa wagonjwa pindi wakizidiwa
kwenda kutibiwa. 
 
Mbali na msaada huo, mbunge huyo ambaye mbali na ahadi
mbalimbali kwa wapiga kura wake, aliahidi kuboresha huduma za afya katika jimbo
hilo amekwishatoa msaada vitanda, magodoro, viti vya kubeba wagonjwa na vifaa
tiba mbalimbali katika hospitali ya Mafinga. 
 
Akipokea na kushukuru kwa msaada huo, Kaimu Mganga Mkuu wa
kituo cha Ihongole, Bernad Makupa alisema msaada huo wa vitanda na gari ya
kubebea wagonjwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahudumia wananchi katika vijiji
mbalimbali vinavyopata huduma katika kituo hicho.
 
 
Kwa niaba ya halmashauri ya Mafinga Mjini, mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Charles Makoga alimshukuru Chumi kwa ushiriki wake katika
kuchangia maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo kabla na baada ya kuingia
madarakani na akamuomba endelee na moyo huo.

No comments :

Post a Comment