Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili
katika kituo cha kupoza umeme cha Mbagala kilichopo jijini Dar es Saalam
tarehe 22 Machi, 2018. Kulia ni Mhandisi Mkuu wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Alex Adam
Mhandisi Mkuu wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Alex Adam (wa pili kushoto)
akielezea shughuli zinazofanywa na kituo cha kupoza umeme cha Mbagala
kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) katika ziara
hiyo.
Mafundi wa kampuni ya Sengerema
Engineering wakikamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa ajili ya
kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa katika kijiji cha Kinyanya kilichopo
wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (kulia) akibonyeza kitufe kuashiria uwashaji wa umeme katika
kijiji cha Kinyanya kilichopo wilayani Kibiti mkoani Pwani.
……………….
Na Greyson Mwase, Pwani
Machi 23, 2018
Wilaya za Mkuranga, Kibiti na
wilaya ya Rufiji katika kata ya Ikwiriri zimeanza kupata nishati ya
uhakika ya umeme mara baada ya kuunganishwa katika Gridi ya Taifa na
kukamilika kwa kituo cha kupozea umeme cha Mbagala kilichopo jijini Dar
es Salaam.
Hayo yalielezwa na Waziri wa
Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wa Ikwiriri
wilayani Rufiji mkoani Pwani katika ziara yake ya siku moja jana
(tarehe 22 Machi, 2018) ya kukagua miundombinu ya umeme iliyounganishwa
na Gridi ya
Taifa kutokea katika kituo cha kupoza umeme cha Mbagala hadi
Ikwiriri na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme
vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Dkt. Kalemani alisema lengo la
kuunganisha wilaya hizo na Gridi ya taifa ni kuhakikisha wananchi
wanapata nishati ya umeme wa uhakika na kuondokana na umeme unaotokana
na mitambo ya mafuta ya Somangafungu ambayo imekuwa ikiharibika mara
kwa mara.
Alisema awali kabla ya wilaya hizo
kuunganishwa na Gridi ya Taifa, kulikuwepo na changamoto ya kukatika
kwa umeme katika wilaya hizo kutokana na mitambo kuhitaji matengenezo ya
mara kwa mara.
Alisema ili kukabiliana na
changamoto hiyo, Serikali iliamua kuunganisha wilaya hizo kwenye Gridi
ya Taifa ili kuwepo na umeme wa uhakika ambao mbali na matumizi ya
majumbani unategemewa na viwanda vilivyopo katika mkoa wa Pwani
Katika hatua nyingine akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Kinyanya kilichopo katika wilaya ya Kibiti
mkoani Pwani ambapo aliwasha rasmi umeme, Waziri Kalemani aliwataka
wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kupitia REA kuhakikisha vijiji
vyote na vitongoji vyake vinapata umeme wa uhakika.
Aliwataka wakandarasi hao
kuhakikisha sehemu za huduma muhimu za jamii kama vile vituo vya afya,
shule, kanisa na misikiti zinapata umeme wa uhakika.
Waziri Kalemani pia aliwataka wananchi kuanza kutandaza mifumo ya umeme (wiring) majumbani pamoja na kulipia shilingi 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa na huduma ya umeme.
Alielekeza Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kuhakikisha umeme haukatiki na kufungua ofisi karibu
na wananchi ili kuepuka adha ya wananchi kwenda mbali kufuata huduma ya
kuunganishiwa umeme.
“ TANESCO ni lazima mhakikishe
mnawafuata wananchi na kukusanya fedha kwa ajili ya kuunganishiwa na
huduma ya umeme, hata kama ni chini ya mwembe badala ya wananchi
kutumia gharama kubwa kwenda mjini kuwafuata,” alisema Dkt. Kalemani
Wakati huohuo wakizungumza
kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho waliishukuru Serikali kwa
kuwafikishia huduma ya umeme na kuongeza kuwa uchumi wa wilaya ya Kibiti
utaanza kukua kutokana na ajira kuongezeka.
Hamisi Mkwera akizungumza kwa
niaba ya wananchi wenzake alisema uwepo wa umeme wa uhakika kwenye
wilaya yao utachochea ukuaji wa viwanda na kuongezeka kwa fursa za
ajira kwa wakazi waishio karibu na viwanda husika
No comments :
Post a Comment