Mkazi wa Kata ya Maramba Wilaya
ya Mkinga Mkoani Tanga, Julius Benjamin akimweleza Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa (mbele) kuhusu
changamoto ya miundombinu ya barabara katika eneo hilo jana Jumamosi
(Februari 17, 2018) wakati wa ziara ya Naibu Waziri kukagua miundombinu
ya barabara katika Mkoa wa Tanga.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Julius Kwandikwa akizungumza na wananchi wa Kata ya
Maramba Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga kuhusu mikakati na ahadi ya
Serikali kujenga miundombinu ya barabara Mkoani Tanga ikiwemo barabara
ya eneo la Maramba wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya
barabara Mkoani humo jana Jumamosi (Februari 17, 2018).
………………………………………………………………………………………
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Mkinga
18.2.2018
WANANCHI wa Kata ya Maramba
Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wameiomba Serikali kupitia Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwajengea barabara ya kiwango cha lami
katika Kata hiyo kwa kuwa eneo hilo kwa sasa limekuwa tegemeo kubwa
katika kutoa huduma za kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Tanga.
Wakiwasilisha malalamiko yao
mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Elias
Kwandikwa jana Jumamosi Februari 16, 2018 aliyekuwa katika ziara ya
kukagua miradi ya barabara katika Mkoa wa Tanga, wananchi hao walisema
eneo hilo limekuwa vigumu kupitika wakati wa mvua za masika na hivyo
kusababisha kero kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi hao, Bw.
Julius Benjamin alisema tangu kuanzishwa kwa mji huo mwaka 2004,
kumekuwepo na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, pamoja na
eneo hilo kuwa kiunganishi cha Wilaya za Mkinga, Korogwe na Muheza
Mkoani humo.
“Hata ukitazama katika ramani
utaona kuwa eneo la marimba lipo tangu mwaka 1919 na lilikuwa maarufu
sana katika shughuli za uchimbaji wa madini, lakini pamoja na kuwa ni
eneo la kihistoria miundombinu ya barabara katika eneo letu limekuwa ni
tatizo kubwa hususani kipindi cha mvua za masika” alisema Julius.
Aidha aliongeza kuwa pamoja na
jitihada mbalimbali zilizofanywa na wananchi wa eneo hilo kwa ajili ya
kufikisha kilio chao, eneo hilo bado limeendelea kuwa na tatizo la
barabara, hivyo ujio wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
katika Kata hiyo unatarajia kulipatia ufumbuzi jambo hilo.
Naye Bw. Juma Ahmed alisema
pamoja na eneo hilo kuwa tegemeo la kiuchumi katika Mkoa wa Tanga, kwa
kipindi kirefu Serikali imeshindwa kutengeneza miundombinu ya uhakika
wa barabara ambazo zitawawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika
shughuli za kiuchumi.
Anaongeza kuwa barabara hiyo pia
imekuwa ni nyembamba pamoja na kuwa na pilikapilika mbalimbali za huduma
za kijamii na kiuchumi, hivyo kuiomba Serikali kuitazama kwa jicho la
tatu eneo hilo kwa kuwapatia miundombinu ya uhakika nma hivyo kumaliza
kilio cha muda mrefu kwa wananchi hao.
Akijibu hoja za wananchi hao,
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alisema
Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya
uhakika katika Mkoa wa Tanga ikiwemo ujenzi wa barabara hatua
inayolenga kuinua uchumi wa Mkoa na kipato cha wananchi kwa ujumla wake.
“Serikali ya Awamu ya Tano
inafanya kazi usiku na mchana katika kumaliza changamoto mbalimbali za
wananchi wake ikiwemob uimarishaji wa miundombinu ya huduma za kijamii
na kiuchumi ikiwemo barabara, hivyo tumejipanga kuwatumikia” alisema
Kwandikwa.
Aliongeza Serikali ipo mbioni
kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya Maramba ikiwemo kuanza zoezi la
upembuzi yakinifu na kuanza michoro ya eneo hilo kwa ajili ya kutambua
mahitaji yake na baadaye kuanza mara moja ujenzi wake.
Kwa mujibu wa Kwandikwa
kukamilika kwa barabara hiyo kutaweza kuharakisha shughuli mbalimbali za
maendeleo ikiwemo uzalishaji wa mazao na usafirishaji wa pembejeo za
kilimo na hivyo kufungua fursa kwa wakazi wa eneo hilo kujiimarisha
kiuchumi.
No comments :
Post a Comment