Saturday, November 18, 2017

WAJASIRIAMALI WAASWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA MTANDAONI KUKUZA BIASHARA ZAO

Hayo yalisemwa kwenye semina kuhusu “Biashara za Mtandaoni” ikiwa na lengo la ‘kuongeza ufikiaji wa soko na kukuza mbinu za kibiashara kupitia mtandaoni,’ katika mkutano wa pili wa Maonyesho ya Afrika ya Mashariki ya Biashara na Ujasiriamali mwaka 2017 (EABECE) uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 14 mpaka Novemba 16.
Akizungumza kama mmojawapo wa jopo la wazungumzaji wakati wa semina hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Jumia Tanzania, kampuni ambayo inajihusisha na biashara ya manunuzi na uuzaji wa bidhaa mtandaoni, Bw. Albany James amesema kuwa changamoto kubwa wanayopambana nayo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba inawashawishi wafanyabiashara wote kuhamia kwenye mfumo wa mtandaoni ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
“Kikubwa tunachokifanya ni kuwakutanisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali na wateja mtandaoni. Kupitia uwekezaji mkubwa wa teknolojia tulioufanya, tumedhamiria kuwapatia wauzaji na wanunuaji urahisi mkubwa sawasawa na kama wanavyokwenda madukani,” alisema na kuhitimisha Bw. James, “Tunafahamu kwamba kwenye biashara ili kufikia soko kwa urahisi ni lazima uwajue wateja wako na namna ya kuwafikia ambapo mara nyingi ni kwa njia ya matangazo. 

Lakini sio wafanyabiashara wote wanaweza kulimudu ukizingatia wengi ndio wanaanza na hawana mitaji au faida kubwa ya kuwekeza kwenye matangazo. Hivyo basi, Jumia tunachokifanya ni kuwapatia fursa ya kujitangaza kwa njia ya mtandao bila ya gharama yoyote kwani ndipo kwenye idadi kubwa ya watu kwa hivi sasa.”
Naye kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Umma na Masoko wa Jumia Travel Tanzania, Bw. Kijanga Geofrey, kampuni dada ya Jumia Tanzania ambayo yenyewe inajihusisha na utoaji wa huduma za hoteli mtandaoni nchini na barani Afrika kwa ujumla, ameongezea kuwa fursa iliyopo kwa wafanyabiashara kuhamia mtandaoni ni kubwa na haina gharama kama wengi wanavyofikiri.
“Wafanyabishara wengi bado ni waoga wa kutumia teknolojia kwenye kukuza na kurahisisha biashara zao. Ripoti zinaonyesha kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi 20 zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani ambao kwa kiasi kikubwa unachangiwa na sekta za utalii, ujenzi, fedha na biashara ukiacha na nyinginezo. Lakini kikubwa zaidi ni ukuaji wa TEHAMA ambapo takwimu zinaonyesha 40% ya watanzania wamefikiwa na mtandao wa intaneti ambapo wameongezeka na kufikia milioni 19.86 mwaka 2016 kutoka milioni 17.26 mwaka 2015. Takwimu hiyo pia imechochea kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi na kufikia milioni 40.17 mwaka 2016,” alisema Bw, Geofrey.
“Hilo ni sawa na ongezeko la 0.9% kwa mwaka na ukuaji wa ueneaji kwa 83% kwenye nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 50. Hii ni dhahiri kwamba kuna mustakabali mkubwa kwa ukuaji wa biashara za mtandaoni kwenye sekta mbalimbali. Kwa sasa mawasiliano ya simu ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa kasi nchini Tanzania na inatoa mchango mkubwa katika kuwaunganisha watanzania kwenye mfumo wa kifedha. Kwa kuongezea, idadi ya watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu nayo imeongozeka na kufikia milioni 18.08 mwaka 2016 kutoka milioni 17.63 mwaka 2015. Hizi zote ni ishara kwamba watanzania wapo tayari kwa biashara za mtandaoni kitaalamu na kisaikolojia,” alihitimisha Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma na Masoko wa Jumia Travel Tanzania.
SOMA ZAIDI »

No comments :

Post a Comment