Madaktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada
(IIRO) ya nchini Saudi Arabia wamefanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya
moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia
mtambo wa Cathlab kwa wagonjwa 33.
Kwa
mara ya kwanza tangu Taasisi imeanza kutoa huduma ya matibabu ya
upasuaji wa Moyo bila ya kufungua kifua tumefanya upasuaji wa kuzibua
mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono. Upasuaji tuliokuwa
tunaufanya kwa wagonjwa wetu ni wa kutumia mishipa ya paja.
Upasuaji
wa moyo unaofanyika katika kambi hii ambayo imeanza Jumatano tarehe
15/11/2017 hadi Jumamosi tarehe 18/11/2017 ni ya upasuaji wa bila
kufungua kifua kwa watu wazima. Upasuaji uliofanyika ni wa kuzibua
mishipa ya moyo iliyoziba.
Faida
ya upasuaji uliofanyika ni kumwezesha mgonjwa kutoka ...
chumba cha
upasuaji akiwa anatembea na baada ya masaa manne kama hali yake
inaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa. Tofauti na upasuaji wa kutumia
mshipa wa paja ambao tulikuwa tunaufanya, baada ya upasuaji mgonjwa ni
lazima akae Hospitali kwa zaidi ya masaa 24 ili kuangalia maendeleo ya
afya yake.
Kambi
hii imeenda sambamba na utoaji wa elimu na kubadilishana ujuzi wa
kazi kati ya wafanyakazi wa Taasisi hizi mbili ikiwemo aina mpya ya
upasuaji uliofanyika kitu ambacho kimewajengea uwezo zaidi wafanyakazi
wetu. Aidha wageni nao wamepata muda wa kujifunza vitu vingi na kupata
uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia ambayo
katika nchi yao hakuna.
Tunaendelea
kuwasisitiza wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara
hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na hivyo kupata
tiba kwa wakati. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo katika matibabu
ya wagonjwa wetu ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa
katika hali nzuri.
Kama
mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea
kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao
utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji
kupata matibabu.
Kwa
namna ya kipekee tunaishukuru sana Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu
ya Misaada (IIRO) kwa kutuma wataalam wake wa magonjwa ya moyo kuja
hapa nchini kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wetu.
No comments :
Post a Comment