Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza jambo wakati wa kufunga mafunzo ya
Wadadisi na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na
Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, mjini Dodoma, utakaohusisha
kaya binafsi 10,460.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa
maelezo kuhusu namna utafiti wa Mapato
na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara utakao gharimu shilingi bilioni 10,
wakati wa kufunga mafunzo ya wadadisi na uzinduzi wa wa zoezi la ukusanyaji
takwimu za utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, Mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara Fedha na
Mipango Dkt. Khatibu Kazungu akimkaribisha
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kufunga
mafunzo ya Wadadisi, na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa
Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, Mjini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, anayeshughulikia TEHAMA Bw. Baltazar Kibola, akieleza mikakati ya Ofisi
yake katika kusaidia kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za utafiti wa
Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, uzinduzi huo
umefanyika mjini Dodoma.
Wadadisi wa Takwimu
za Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya
Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018, wakifuatilia matukio mbalimbali wakati
wa hafla ya uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), Mjini Dodoma.
Meza Kuu
(Walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na Wasimamizi wa zoezi la ukusanyaji
wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka
2017/2018, mjini Dodoma. Utafiti huo utahusisha kaya binafsi 10,460.
BENNY MWAIPAJA
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango,
amezindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya
kaya binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, utakaogharimu shilingi bilioni 10
zilizotolewa na... Benki ya Dunia.
Lengo la utafiti huo utakaofanywa na Ofisi Kuu ya
Taifa ya Takwimu (NBS) ni kupata takwimu zinazohusu shughuli za kijamii na
kiuchumi, mapato na matumizi, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali katika
ngazi ya kaya.
Dkt. Mpango alisema kuwa Utafiti huo utaiwezesha
Serikali kupima kiwango cha hali ya umaskini wa kipato, chakula na pengo baina
ya matajiri na maskini kuanzia kipindi cha mwaka 2013 hadi sasa.
“Takwimu zilizopo hivi sasa zinaonesha kwamba kiwango
cha umasikini wa kipato ulipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi kufikia
asilimia 28.2 mwaka 2012” Alisema Dkt. Mpango.
Alisema pamoja na takwimu hizo, bado kiwango cha
umasikini ni kikubwa na kwamba Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau
mbalimbali inahakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za msingi za kijamii
kwa kadri uchumi unavyokua hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la
umasikini.
“Nimefurahi kuelezwa kuwa utafiti huu utakusanya
takwimu katika kaya binafsi 10,460 kwa Tanzania Bara kuanzia Novemba 2017 hadi
Novemba 2018 na kwamba kupitia zoezi hili, Serikali ya Awamu ya Tano imetoa
ajira kwa vijana wapata 620 katika maeneo ya vijijini na mijini” alieleza Dkt.
Mpango.
Aliwaasa wadadisi hao kufanyakazi zao kwa umakini na
weredi mkubwa ili takwimu zitakazopatikana ziwe sahihi na kuonya kuwa Serikali
haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaojaribu kuvuruga zoezi
hili.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Dkt. Albina Chuwa alieleza kuwa ukusanyaji wa Takwimu za utafiti wa mapato na
matumizi ya kaya binafsi utafanyika katika maeneo 754 yaliyochaguliwa kitaalamu
kwa kutumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.
“Utafiti huu utakuwa wa saba tangu Tanzania ipate
uhuru wake mwaka 1961, ambapo tafuti nyngine zilifanyika 1969, 1991/92, 2001,
20117 na mwaka 2011/12” aliongeza Dkt. Chuwa.
Alisema kuwa utafiti huo mpya utafanyika kwa kutumia
teknolojia ya kisasa ijulikanayo kama Survey Solution (CAPI) na kwamba matokeo
ya awali ya utafiti huo yanatarajiwa kutolewa ndani ya miezi sita ijayo ili
nchi iweze kufahamu kiwango cha umasikini uliopo katika jamii hivi sasa baada
ya kufanyika kwa utafiti kama huo miaka mitano iliyopita.
“Utafiti wa mwisho uliofanyika mwaka 2011/2012
uliotumia karatasi uligharimu shilingi bilioni 20 lakini kwa kutumia teknolojia
mpya, utafiti huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 10 pekee” alisisitiza
Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa alisema kuwa anaamini matokeo ya utafiti
huo yatakuwa chachu ya kupata takwimu za msingi kwa ajili ya kufuatilia na
kutathimini utekelezaji wa program mbalimbali za kitaifa na kimataifa zenye
kulenga kupunguza kiwango cha umasikini nchini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais TAMISEMI
anayeshughulikia miundombinu ya TEHAMA Bw. Baltazar Kibola alisema kuwa watatoa
ushirikiano wakutosha kwa wadadisi hao katika ngazi zote kuanzia Mikoa, Wilaya,
Halmashauri, Kata, Vijiji na Vitongoji ikiwemo kufanyia marekebisho
vitendeakazi vya kukusanyia takwimu hizo vikipata hitililafu ili azma ya
Serikali ya kupata takwimu sahihi itimie kama ilivyopangwa.
No comments :
Post a Comment