Tuesday, November 21, 2017

Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) na mkutano mkuu wa wadau



Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Masha Mshomba, akifafanua baadhi ya mambo yanayohusiana na Mfuko kwa waandishi wa habari.
 
Na CHRISTIAN GAYA

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unategemea kuwa na Mkutano Mkuu wa kwanza wa mwaka wa wadau mbalimbali wa sekta ya hifadhi ya jamii utakafanyika kuanzia tarehe 29 mpaka 30 Novemba  2017 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Simba AICC Arusha. Kauli mbiu ya mkutano huu ni "Mafao ya Fidia: Haki ya Mfanyakazi na chachu katika kukuza Uchumi wa Viwanda". Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa.

Ikumbukwe ya kuwa njia mojawapo ya wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni kufuatilia na kujua utendaji wa mifuko hii inayosimamiwa na bodi za wadhamini kwa njia ya mikutano mikuu inayofanyika kila mwaka.
Hivyo hii itakuwa nafasi ya kipekee na muhimu sana kwa wadau wa Mfuko wa WCF kuhudhuria kwa ajili ya kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa  afya na ustawi wa Mfuko zinazohusiana na taarifa za ukaguzi wa mahesabu za mwaka ili kujua nafasi, uwezo wa Mfuko kifedha na kutathmini maendeleo na changamoto zinazoukabili Mfuko na kupokea maoni ya kuboresha huduma za Mfuko na kuondoa dukuduku miongoni mwa wadau juu ya Mfuko.
Ni wajibu wa bodi ya wadhamini ya WCF kuhakikisha ya kuwa taarifa za kuwapasha wadau zinawafikia wadau wa mfuko huu juu ya kufanyika mkutano mkuu wa mwaka kwa muda muafaka. Maswali ya kujiuliza ni kama vile taarifa hizo zinazotolewa na WCF zina ubora gani na je zimewafikia wadau wanaohusika kwa muda muafaka?
Kuwawezesha wadau kutekeleza haki, wajibu na nguvu walizopewa katika mkutano mkuu wa mwaka kama huu wanatakiwa kuandaliwa mapema kwa muda muafaka na kupewa habari bora na za hali ya juu na isipofanyika hivyo basi uwezo wa nguvu wa kisheria waliopewa unakuwa hauna nguvu yeyote kwa wadau.
Na kwa upande mwingine mtu anaweza kujiuliza ya kwamba chukulia ya kuwa mwanachama amepelekewa habari na kupata taarifa mapema juu ya kuhudhuria mkutano mkuu wa kwanza na wadau wa WCF. Je baada ya hapo inafuatiliwa ili kuhakikisha ya kuwa hawa wadau watakaochaguliwa kuwawakilisha wenzao kwenye mkutano huo watawajibika kama inavyotakiwa.
Hivyo kwa upande mwingine unaweza kusema ya kuwa wadau kupatiwa taarifa na bora kwa muda muda muafaka hiyo haitoshi kabisa  kinachotakiwa hapa ni kwa hali na mali mdau kuwa tayari kujua au kuelewa kilichoandaliwa kwenye makabrasha ambalo ni jambo linaloonekana kuwa ni tatizo kubwa kwa wanachama na wadau wengi.
Mtu mwingine anaweza kuwa na mashaka na kilichopo ndani ya makabrasha kama siyo pambo tu la kuvutia Mfuko kwa idadi kubwa ya wadau.
Kwa upande mwingine wanachama mara nyingi wameonekana kuwa ni kundi ambalo halina nguvu kabisa kwa kusimamia utendaji na uendeshaji wa mifuko ya hifadhi hii ya jamii ikiwemo kufuatilia tabia na utaratibu wa utendaji wa wadhamini au bodi hizi za hifadhi ya jamii  na hata inaonekana wanatofautiana katika mitazamo kwa upande mwingine
Hapa ikumbuka kwamba uhai na ustawi wa mifuko ya hifadhi ya jamii siyo kweli ya kwamba inategemewa na mikutano mikuu ya mwaka ya mifuko kama huu utakaofanyika huko Arusha na WCF ingawa ni mojawapo ya mlango muhimu wa ufahamu kama mfuko wa pensheni wa hifadhi ya jamii.
Wadau wa Mfuko wametawanyika karibu mikoa yote ya Tanzania kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Wilaya, Kimkoa na hadi Kitaifa hivyo kwa maana hii inalazimisha kuwepo na uwakilishi katika kuhudhuria kwenye mkutano mkuu huu wa mwaka.
Kutokana na msambaratiko huu wa wadau na hatimaye kuwakilishwa na watu wachache kutoka kila kampuni za umma na  za watu binafsi, na taasisi mbalimbali za serikali kwa hiyo hata mahudhuria ya wadau kwenye mkutano mkuu wa mwaka umekuwa wa matatizo kwa kuhudhuriwa na wadau wachache wawakilishi. Kwa sababu hii imesababisa mpaka kuwepo na uwakilishi katika mkutano mkuu wa kila mwaka badala ya wadau wote kuhudhuria.
Jambo la kujiuliza ni kwamba je hawa wawakilishi kutoka kwa waajiri mbalimbali wanakutana na wafanyakazi wenzao  au kama ni mwajiri je naye anahakikishaje kutoa taarifa kwa ukamilifu na ubora ule ule uliotolewa wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wadau
Kwa kifupi ni kwamba je wanachama hupewa taarifa na wawakilishi mara tu baada ya kutoka kwenye mahudhurio ya mkutano mkuu? Na kama hawapewi kunakuwepo na maana gani ya kuwa na mwakilishi wa wafanyakazi wenzao?
Hivyo kuna haja ya kuwa na malengo na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha ya kuwa waajiri, wafanyakazi, na taasisi mbalimbali kuchagua mwakilishi ambaye atakuwa ni mtu ambaye atashiriki kwa malengo ya kuelewa na kujua mambo muhimu ya mkutano mkuu hasa yanayogusa uhai, afya na ustawi wa Mfuko kwa malengo ya kuboresha huduma kwa wafanyakazi ambao wataumia, wataugua ama watafariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.
Mfuko wa WCF ni Taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263 marejeo ya mwaka 2015). Lengo kuu la kuanzishwa kwa Mfuko huu ni kushughulikia masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wanaumia, wanaugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao
.
Mwandishi wa makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu  +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment