Saturday, September 9, 2017

VITA YA UCHUMI YAPAMBA MOTO; VIGOGO KADHAA WATIWA MBARONI, SHEHENA YA ALMASI YATAIFISHWA NA SERIKALI




NAIBU Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP, Lazaro Mambosasawamesema tayari watu kadhaa {vigogo), waliotajwa kwenye ripoti ya vito vya almasi na madini mengine, wanashikiliwa na kuhojwia kuhusiana na uhusika wao kwenye kashfa hiyo.
Viongozi hao wa vyombo vya dola, wamedokeza kukamatwa kwa vigogo hao, wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokuwa akipokea ripoti ya kukamatwa kwa almasi kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, hivi karibuni.
“Nikuhakikishie tu Mhe. Waziri, watu wetu wako kazini na hivi sasa tunapozungumza watu kadhaa wamekwishakamatwa kwa sababu za kiupelelezi, siwezi kutaja majina yao kwa sasa lakini nikuhakikishie tu kwamba wanahojiwa ili kujua uhusika wao katika sakata hili na kasha tuandae mashtaka dhidi yao,” alisema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema, licha ya kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, pia anamuwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, na kwamba na wao wako kazini na tayari “wamewadaka” watu kadhaa na wako kwenye mahojiano ili kujua namna walivyoshiriki kwenye njama ya kushusha thamani ya madini hayo ya Almasi.Madini hayo yalizuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, saa chache kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
“Mheshimiwa Waziri, bila shaka maelekezo haya uliyoyatoa ni maelekezo ya Mhe Rais, kwa hivyo sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama hatutakaa kimya kuvumilia uyoroshwaji wa mali zetu na hivyo kulifanya taifa kuwa ombaomba kila wakati.” Aisema, Kamanda Mambosasa.
AwaliWaziri wa Fedha na Mipango, ambaye alifika uwanjani hapo kukagua madini yaliyozuiwa na serikali baada ya kugundulika kuwa yalipewa thamani pungufu ya ile halisi.
Waziri alsiema, taifa limepoteza mamilioni ya dola za kimarekani katika udanganyifu huo.
“Niwaagize ninyi vyombo vya ulinzi na usalama, watu wote kuanzia kule mgodini hadi hapa, walioshiriki au waliokuwa wakishiriki kufanya vitendo hivi watiwe mbaroni, wachunguzwe na mali zao zikamatwe mara moja,” alisema Dkt. Mpango kwa hasira.
Dkt. Mpango pia alionya ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali kutokuwa uchochoro wa kushindwa kwenye kesi na kwamba ushahidi wote uko wazi.
“Lazima mali za watanzania zirudi kwa watanzania wenyewe, na sio kwa watu wachache.” Alisema Dkt.Mpango.
Akijibu maelezo hayo ya Mhe. Waziri, Mkurugenzi wa Mashataka, (DPP), Bw. Biswalo Mganga, alimuhakikishia Waziri Mpango, kuwa wote waliotajwa, kwa mujibu wa sheria, mali zao zitataifishwa kama watapatikana na hatia. 
 Katika hatua ningine, Waziri Mpango alipata fursa ya kukagua almasi iliyokamatwa na kupewa thamani ya chini ambapo Kamishna wa TRA, Bw. Kichere alsiema, kwa mujibu wa sheria kufanya udanganyifu wa mali chini ya sheria ya forodha ya Afrika Mashariki, mali hiyo inataifishwa na inakuwa mali ya serikali.
Alamsi hiyo inatoka mgodi wa Mwadui mkoani Shinyanga.

No comments :

Post a Comment