Monday, May 22, 2017

MAJAJI NA MAHAKIMU WATAKIWA KUWA NA MTAZAMO CHANYA WANAPOTEKELEZA MAJUKUMU YAO




NA MAGRETH KINABO –MAHAKAMA YA TANZANIA.
JAJI Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali, (pichani kushoto), amewataka Majaji na Mahakimu kuzingatia maadili ya Uhakimu na Utumishi wa Umma na kutenda haki wakati wanapotimiza majukumu yao.
Aidha, Jaji huyo alisema Majaji na mahakimu wanapotimiza majukumu yao wanapaswa kuzingatia kanuni za utendaji wao na za utumishi wa umma hatua ambayo itawafanya kukidhi matakwa ya wananchi wanaowahudumia.
Kauli hiyo, imetolewa na Mhe. Jaji huyo   wakati akizungumza na baadhi ya Majaji na Mahakimu  mbalimbali katika kikao  kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi mndogo wa Bunge uliopo jijini Dar es Salaam.
“Suala la maadili lilianza tangu enzi za kale, jamii ilikuwa inajiwekea maadili, uwepo wa maadili ni heshima na utii, tabia ya uaminifu, uwajibikaji na kufuata  utaratibu kila unapotekeleza kazi,” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi huku akisema masuala yalizishazungumziwa na baadhi ya viongozi wa kitaifa, akiwemo Baba wa Taifa mwaka  Machi 15, mwaka 1984 na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa Novemba 27, mwaka 2011.
Aliongeza kuwa suala la maadili ni muhimu katika kupambana na rushwa, pia linafanya Jaji na Hakimu awe na tabia njema mbele ya jamii, hivyo kazi hizo zinahitaji uadilifu na mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Beatrice Mutungi akifungua kikao hicho, alisema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili changamoto za kada hizo na kubadilishana uzoefu wakati wa kutatua changamoto hizo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

No comments :

Post a Comment