Monday, February 19, 2018

KAMBI YA MATIBABU YA MOYO KUFANYIKA ZANZIBAR MWEZI JUNE


1
Waziri wa AfYa Mahmoud Thabiti Kombo akimkaribisha Daktari bingwa wa maradhi ya moyo Duniani Dkt Ramakanta Panda alipomtembelea Ofisini kwake Mnazimmoja Zanzibar kuhusu kambi wanayotarajia kuifanya ya matibabu ya Moyo mwezi June.
2
Daktari bingwa wa maradhi ya moyo Duniani Ramakanta Panda kutoka Taasisi ya Moyo ya Asia akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani Wizara ya Afya kuhusu Kambi ya Matibabu ya Moyo inayotarajiwa kufanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya mwezi June. Kushoto yake ni Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo.
Picha na Abdalla Omari-Habari Maelezo Zanzibar
……………..
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Kufuatia ongezeko la maradhi ya moyo Zanzibar Taasisi ya Moyo ya Asia yenye makao yake nchini India kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar inatarajia kuweka Kambi ya
Matibabu ya Moyo kwa kipindi cha wiki moja.
Kambi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi wa Juni ambapo Wataalam wa Tiba za Moyo watakuja na kufanya uchunguzi wa afya kwa Wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza na Waandishi wa habari Waziri wa Afya wa Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amesema kwa wastan Wizara ya Afya inapokea wagonjwa wa Moyo 160 hadi 180 kwa mwaka.
Amesema idadi hiyo ni ya Wananchi ambao hujitokeza kwa hiari kupima afya zao na kwamba kuna uwezekano idadi kuongezeka siku hadi siku.
“Hawa wagonjwa 160-180 tunaowabaini na maradhi ya moyo ni wale tu ambao wamekuja kupima inawezekana ikawa kuna idadi kubwa ya wagonjwa ambao bado hawajaenda Hospital kupima afya zao” alisema Waziri Kombo.
Waziri Kombo amesema wagonjwa watakaobainika na maradhi ya Moyo watafanyiwa matibabu na wale watakaolazimika kufanyiwa upasuaji watapewa maelekezo ya wapi waafanyiwe upasuaji.
Amesema nchini India wagonjwa wengi hawalazimiki kufanyiwa upasuaji badala yake hupatiwa Dawa kwa vile tu wanawahi mapema kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.
Hivyo Waziri huyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwa wastani wa mara moja kwa mwezi ili kujiweka katika mazingira mazuri kiafya.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Asia Ramakanta Panda amesema kwa kipindi cha mwaka Taasisi yao itatuma timu ya wataalam wa maradhi ya Moyo kuja Zanzibar kufanya kambi mara mbili kwa lengo la kukagua afya za Wagonjwa wa Moyo Unguja na Pemba.
Mbali na Kambi, Taasisi hiyo imekubali kuwasomesha Madaktari wawili kutoka Zanzibar ambao wataenda nchini India kujifunza zaidi kuhusu maradhi ya Moyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Dkt. Panda amesema yupo tayari kushirikiana moja kwa moja na Serikali ya mapinduzi ili kusaidia ujenzi wa kituo cha matibabu ya Moyo maeneo ya Binguni Wilaya ya Kusini Unguja.
Aidha Waziri Kombo amemuonesha Dkt. Bingwa huyo michoro mbali mbali ya kituo cha Taasisi ya Moyo Zanzibar ambacho kitasaidia pakubwa katika mapambano dhidi ya maradhi ya Moyo.
Madakatari hao watakuja kufanya uchunguzi wa Moyo kwa wananchi mbali mbali kupitia vifaa mbali mbali na kutoa ushauri wa kitaalamu namna bora ya kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo Moyo.
 IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments :

Post a Comment