Monday, October 23, 2017

Ujue mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni

Ujue mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni

Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa GEPF Joyce Shaidi akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi millioni 500 kwa Meneja wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Sukari mkoani Kagera Robert Mshoki

Na CHRISTIAN GAYA, MTANZANIA, ALHAMISI OKTOBA 19, 2017
Takwimu zilizotolewa mwaka 2012 zinaonesha ya kuwa ni watu milioni 1.7 tu ndio waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii wakati idadi ya watanzania wote ni milioni 44.9 hii ikiwa ni asilimia 6.5 tu ya nguvu kazi yote ya watu milioni 23.7. Pia pensheni zinazotolewa na mifuko iliyopo hapa nchini hazitoshelezi mahitaji ya watanzania wakiwemo wastaafu na
familia zao. 
Hifadhi ya Jamii ni haki ya kila Mtanzania. Haki hii imeanishwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003. Haki hii pia imeiainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu wa mwaka 1948 pamoja na mikataba ya shirika la kazi duniani (ILO) ibara ya 102 ya mwaka 1952.
Na ndiyo maana Mfuko wa Mafao ya Kustaafu GEPF mwaka 2009 walianzisha mpango wa hiari wa kujiwekea akiba ya uzeeni kwa lengo la kuwawezesha watu wote wenye uwezo wa kuzalisha kipato kujiwekea akiba ili kuwasaidia kutimiza malengo yao katika maisha kama vile kuanzisha au kukuza biashara, matibabu, ujenzi, kulipa ada za shule na kukabiliana na majanga mbali mbali, hasa pale uwezo au nguvu ya kuzalisha kipato inapopungua.
Majanga yapo ya aina nyingi kama vile moto, mafuriko, ukame, ajali na magonjwa mbali mbali yanayosababisha binadamu asiweze kukabiliana nayo kwa haraka pindi yanapotokea.
Mtu yeyote mwenye uwezo wa kuzalisha kipato anaweza kujiunga na mpango huu, awe ameajiriwa na anachangia kwenye mfuko wowote wa hifadhi ya jamii au amejiajiri mwenyewe kama vile; Mkulima,  Mvuvi, Mama Lishe, Dereva boda boda, Mjasiriamali yoyote. Kujiunga na mpango huu wa kujiwekea akiba ya uzeeni ni bure
Kiwango chochote kinaruhusiwa kuanza kujiwekea akiba kulingana na uwezo wa mwanachama. Mwanachama anaweza kuweka akiba wakati wowote, iwe kila siku, kila wiki, kila mwezi au kwa msimu.
Mwanachama anaweza kujiwekea akiba kwa kwa njia ya Simu ya Kiganjani (M-pesa, Tigo pesa au Airtel Money), benki kama vile CRDB, NMB, NBC au benki yoyote mwanachama anakotunza fedha zake, Mawakala waliothibitishwa na GEPF, Kuwasilisha moja kwa  moja kwenye Ofisi za Mfuko wa GEPF zilizo Mikoani au Makao Makuu.
Wanachama wa mpango wa hiari wa kujiwekea akiba hulipwa riba kutokana na michango yao. Wengi wa wanachama hawa hawakidhi vigezo vya kulipwa pensheni hivyo wanasalia katika utaratibu wa akiba.  Pamoja na wanachama wa mpango wa hiari kuna baadhi ya wanachama walioko katika mpango wa lazima ambao hawatakidhi kulipwa pensheni hivyo nao pia watalipwa michango yao pamoja na riba. Kwa sasa Mfuko unatoa riba ya 7.5%. Kiasi hiki kinatolewa ili kulinda thamani ya michango ya wanachama.
Faida za kujiunga na Mpango wa Hiari wa kujiwekea Akiba ya Uzeeni,ni kwamba hakuna gharama yoyote inayotozwa wakati wa kuweka akiba, gawio kubwa la mapato linaloongezeka kila mwaka linalotokana na uwekezaji kwenye vitega uchumi mbali mbali, mwanachama anaweza kuchukua sehemu ya akiba yake wakati wowote wa dharura bila kutozwa fedha yoyote, kupata malipo bila usumbufu ndani ya siku saba za kazi, michango ya mwanachama inamuwezesha kulipwa pensheni endapo ataweka kiasi na muda unaofuzu vigezo vya kulipwa pensheni, mikopo kupitia SACCOS au vikundi vilivyojisajili vya wanachama, kupatiwa pembejeo za kilimo kwa wakulima wanaozalisha kwa wingi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu  +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment