Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde,akizungumza na wafanyakazi wa Hospital ya Mkoa wa Dodoma hii leo.
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony
Mavunde,akibonyeza kitufe wakati wa kuzindua matumizi ya mfumo wa
Biometrics na kamera za CCTV katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma.
MBUNGE wa Dodoma mjini Anthony
Mavunde ameendelea kutatua kero katika sekta ya Afya jimboni humo
ambapo leo amezindua matumizi ya mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,kufuatia hali hiyo wagonjwa
wengi waliokuwepo hospital hapo walionekana wenye furaha na kuunga mkono
jitihada za mbunge wao katika kusaidia kuboresha huduma za Afya katika
hospital hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa
matumizi ya vifaa hivyo, Mavunde amesema ufungaji wa mifumo hiyo ni
miongoni mwa jitihada zake za kuhakikisha huduma za afya katika jimbo
hilo zinatolewa ipasavyo.
Mavunde ambaye ni Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Vijana amesema mfumo huo umefungwa na
Ofisi ya Mbunge wa Dodoma na amelazimika kufunga vifaa hivyo kutokana
na malalamiko ya muda mrefu ya wagonjwa kuwa wamekuwa wakitolewa lugha
chafu na wauguzi.
Amesema pamoja na kamera hizo,
pia umefungwa mfumo wa Biometrics(uchukuaji alama za dole gumba) ili
kudhibiti watumishi ambao wamekuwa wakiondoka kabla ya muda na
kuchelewa kuingia kazini.
“Kamera hizi zinarekodi sauti
na kuchukua video ili kuondokana na malalamiko yaliyotolewa na wananchi
na itakuwa ni rahisi kumbaini mtu atakayelalamikiwa na mgonjwa,”amesema
Mavunde
Mavunde amesema fedha
alizotumia kununulia Kamera hizo na mfumo wa Biometrics amezipata kwa
kujibana katika mshahara wake lengo likiwa ni kutekeleza ahadi yake
aliyowaahidi wananchi wakati wa Kampeni kutatua kero za afya.
Aidha amesema hatua hiyo
itasaidia kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi hasa ukizingatia
kwasasa Dodoma kuna ongezeko la watu kutokana na serikali kuhamia mkoani
humo.
“Baadaye pia tutaweka mfumo wa
kuhifadhi mafaili, hii yote ni kurahisisha utendaji kazi katika
hospitali hii ili wananchi wetu waweze kupata huduma za afya
ipasavyo.pia nimeomba vifaa mbalimbali vya kisasa Ujerumani kwa ajili ya
hospitali hii tukipatiwa itasaidia sana utoaji huduma za
afya,”amesisitiza Mavunde
Amesema ameahidi kutatua
changamoto katika sekta ya afya ambapo mbali na ufungaji vifaa hivyo
alishakabidhi vitanda katika Zahanati na Vituo vya afya 35.
“Nimetoa madawa kwenye kituo
cha afya cha Makole yenye thamani ya Sh. Milioni 15,nimefunga umeme wa
jua katika vituo vya Afya 17 pamoja na huduma za macho kwa watu 7000 na
watu 3000 walipata huduma za upasuaji bure,”amesema
Naye, Mganga Mfawidhi wa
Hospitali hiyo,Dk.Caroline Damiani amemshukuru Mbunge huyo huku akidai
kuwa matunda ya ufungaji wa kamera yameanza kuonekana kwa watumishi
kufanya kazi zao kwa ufanisi wa hali ya juu tofauti na awali.
“Kumekuwa na kero nyingi kutoka
kwa wagonjwa sasa Kamera za CCTV zitatusaidia kutatua kero hizi na
kudhibiti wale wanaotoka kabla ya muda wa kazi kuisha au kuchelewa
kazini,”amesema Mganga huyo
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Ufundi wa Kampuni ya Entersoft Limited,Keneth Yindi amesema wamefunga
Kamera 4 pamoja na mfumo wa Biometrics katika hospitali hiyo na ina
uwezo wa kurekodi matukio kwa miezi tisa mfululizo.
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony
Mavunde,akizungumza na wafanyakazi wa Hospital ya Mkoa wa Dodoma hii
leo,wakati wa uzinduzi mfumo wa Biometrics na kamera za CCTV katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.
No comments :
Post a Comment